Featured Posts

Most selected posts are waiting for you. Check this out

MAJINA YA MADIWANI WA VITI MAALUM WALIOTEULIWA LEO NA TUME YA UCHAGUZI (NEC)

MAJINA YA MADIWANI WA VITI MAALUM WALIOTEULIWA LEO NA TUME YA UCHAGUZI (NEC)

Kwa Mujibu wa Kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika leo tarehe 21 Agosti, 2017 na baada ya kushauriana na Vyama vya Siasa imewateua Madiwani Wanawake wa Viti Maalum kumi na wawili (12) kujaza nafasi wazi za Madiwani katika Halmashauri mbalimbali Tanzania Bara.
Madiwani Wanawake wa Viti Maalumu walioteuliwa ni kama ifuatavyo:
NA.JINACHAMAHALMASHAURI
  1. 1
Ndugu Saida Idrisa KiliulaCUFHalmashauri ya Wilaya ya Kilwa
Ndugu Sophia Charokiwa MsangiCCMHalmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Ndugu Shahara Selemani NduvaruvaCCMHalmashauri ya Wilaya ya Mbarali
Ndugu Neema K. NyangaliloCCMHalmashauri ya Manispaa ya Ilala
Ndugu Farida Zaharani MohamedCCMHalmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Ndugu Lucia Silanda KadimuCCMHalmashauri ya Wilaya ya Tabora (Uyui)
Ndugu Amina Ramshi MbairaCCMHalmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu
Ndugu Janeth John KaayaCHADEMAHalmashauri ya Wilaya ya Meru
Ndugu Sara Abdallah KatangaCHADEMAHalmashauri ya Manispaa ya Ilala
Ndugu Ikunda MassaweCHADEMAHalmashauri ya Wilaya ya Hai
Ndugu Tumaini Wilson MasakiCHADEMAHalmashauri ya Wilaya ya Siha
Ndugu Elizaberth Andrea BayyoCHADEMAHalmashauri ya Mji wa Mbulu
Uteuzi huu umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 alitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi uwepo wa nafasi hizo wazi.
Imetolewa leo tarehe 21 Agosti, 2017
Kailima, R. K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
MAMBO YA KUJIFUNZA KUTOKANA NA UTENDAJI KAZI WA WATU WENYE MAFANIKIO

MAMBO YA KUJIFUNZA KUTOKANA NA UTENDAJI KAZI WA WATU WENYE MAFANIKIO

Jinsi gani watu wanaacha meza zao wanapokwenda nyumbani baada ya kumaliza kazi yaweza ikawa ishara tosha ya kuwaelezea jinsi walivyo. Je, meza zao zinakuwa na makaratasi mengi lakini yaliyopangwa, yenye mipango mipya ya kuhakikisha wanafanikiwa? Kuna picha za familia au matukio yenye kumbukumbu maalumu? Au zinakuwa zimesafishwa vizuri na kupangiliwa?
Mazingira anayofanyia kazi mtu pamoja na ratiba yake katika kuhakikisha anafanya kazi kwa ufanisi akiwa ofisini vinaweza kutusaidia kujua ni kwenye hali gani wanakuwa na matokeo makubwa – na hii itakuvutia zaidi unapoangalia mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu wenye mafanikio makubwa sana duniani:
Hapa tutaangalia tabia za kufanya kazi, ratiba za mara kwa mara pamoja na mpangilio wa meza wa Albert Einstein (alikuwa mgunduzi wa dhana mbalimbali za kisayansi), Arianna Huffington (muanzilishimwenza wa jarida maarufu la The Huffington), Elon Musk (muanzilishi wa kampuni inayotengeneza makombora ya SpaceX na kampuni ya magari ya Tesla), na Mark Zuckerberg (muanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook).
Yafuatayo ni baadhi ya mafunzo tunayoweza kuyapata kutokana na kuangalia tabia za watu hawa wakiwa kwenye ofisi zao:
Mark Zuckerberg (mwanzilishi wa mtandao wa Facebook)
Hana ofisi maalumu kwa ajili yake, badala yake anaendelea kufanya kazi kwenye meza iliyopangwa pamoja na wafanyakazi wake wa kampuni ya Facebook.
Funzo: Kama kiongozi mkuu, jinsi unavyoweka maeneo yako ya kufanyia kazi inasaidia kuwaonesha watu wa nje ni mambo yapi ya msingi zaidi kwenye kampuni yako. Mark Zuckerberg anaweka mazingira yake kuwa ya kawaida sana ili aweze kufanya kazi zake kwa umakini mkubwa katika kutatua matatizo yanayojitokeza na dira yake inawaongoza wafanyakazi wote wa Facebook kwani wanajua kwamba hawahitaji ofisi nzuri sana ili kuweza kufanya mambo makubwa duniani.
Elon Musk (mmiliki wa kampuni ya magari ya Tesla)
katika ofisi za Tesla, Elon Musk ameweka meza yake anayofanyia kazi karibu kabisa na sehemu yanapotolewa magari yaliyomaliza kutengenezwa ili aweze kukagua kila gari linatolewa kutoka kiwandani.
Funzo: Unapofanya jambo kubwa sana, ni lazima uwe unakagua kila kitu kuhakikisha kwamba kazi iliyokamilika inakidhi viwango mlivyojiwekea kabla ya huduma au bidhaa hiyo kumfikia mteja. Elon angeweza kabisa kuweka ofisi yake kwenye ghorofa akiwa anaangalia mandhari nzuri sana, lakini kwa kuweka meza yake sehemu anayoweza kuona kila gari lililotengenezwa, anapata uhakika kwamba magari yote yanayokamilika yanakuwa na ubora unaotarajiwa.
Arianna Huffington (muanzilishi wa jarida la Huffington Post)
Kwa yeyote aliyewahi kusoma kitabu chake cha “Sleep Revolution,” ni wazi kabisa kwamba lazima ameona kwamba Arianna Huffington anaamini kwamba watu wengi huwa hawalali kama inavyotakiwa. Kwa sababu hii, anahamasisha watu waweze kupata japo muda mdogo sana wa kulala ofisini ili kuboresha uzalishaji maofisini. Yeye mwenyewe huwa analala ofisini kwake kila akichoka na kuamka akiwa na nguvu mpya ya kufanya kazi.
Funzo: Arianna Huffington ni shuhuda kwamba kama tunaweza kusisitiza wafanyakazi wawe na tabia fulani zinazoweza kuongeza kiwango cha ufanyaji kazi, basi ni bora tuzisimamie kwakuwa ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya kampuni.
Albert Einstein (mgunduzi wa kisayansi)
Einstein alikuwa aliamini kwamba meza ikiwa na vitu vingi ni ishara ya kwamba mtu ana mambo mengi ya kufanya na kufikiria pia. Kwa sababu hiyo, alikuwa anashangaa ni nini kinachoendelea kwenye akili za watu ambao meza zao maofisini ni safi muda wote!
Einstein alikuwa akifikiria pia kwamba kutumia mawazo yatokanayo na dhana mbili, tatu au zaidi zisizofanana na kutengeneza dhana nyingine kabisa – ndio siri kubwa ya wabunifu wengi duniani.
Funzo: Tafiti zinaonesha kuwa meza za wabunifu wengi sana huwa zinakuwa na vitu vingi juu yake – kitu ambacho Einstein alikihitaji sana kutatua “matatizo ambayo hajawahi kukutana nayo kabla” kwenye fizikia.
Muongozo huu unaonesha kwamba watu wenye mafanikio makubwa sana duniani wameweza kugundua nini cha kufanya ili waweze kuhakikisha kazi wanazofanya zinaleta matokeo mazuri muda wote, kwao binafsi na kwa kampuni nzima vilevile. Ni muhimu hata wewe kujua hili pia…angalia ni nini kikifanyika kitachangia kuleta matokeo mazuri kazini kwako na ufanye hicho siku zote.
IFAHAMU NJIA YA UZAZI WA MPANGO INAYOTUMIWA ZAIDI NA WANAUME WA DAR

IFAHAMU NJIA YA UZAZI WA MPANGO INAYOTUMIWA ZAIDI NA WANAUME WA DAR

Jamii nyingi za mijini na vijiji nchini Tanzania zimezidi kuwa na uwelewa kuhusu matumizi ya njia za kupanga uzazi ili kuhakikisha hawapati mtoto ambaye hakutarajiwa na pia wanapata muda mzuri wa kumlea mtoto waliyenaye kwa wati huo.
Katika kupanga uzazi, kuna njia mbalimbali ambapo kuna njia za kisasa na za asili zinazoweza kutumika kama vile kutumia mipira (condoms), kumwaga manii nje (pull out/withdrawal), kupandikiza vijiti, kutumia video, kitanzi au kufuata mzunguko wa hedhi.
Wanaume wa Dar es Salaam imebainika kuwa hutumia zaidi njia ya asili ya kumwaga manii nje kuliko njia nyingine yeyote. Katika uchunguzi huo ulionyesha kuwa asilimia 18 hutumia njia hiyo kuliko nyingine.
Hayo ni matokeo ya uchunguzi wa UNFPA uliokuwa ukichunguza kuhusu wingi wa watu na afya ya uzazi kwa Tanzania ambapo ripoti hiyo ni ya mwaka 2015/2016.
Hii ni moja ya njia za kupanga uzazi (uzazi wa mpango) ambapo mwanaume anatakiwa kutoa uume wake nje na kuwaga manii nje ya uke wakati wa kujamiiana ili kuhakikisha kuwa mwenza wake hapati ujauzito. Unatakiwa kuhakikisha uume wote upo nje kabla ili kuzuia mbegu zako kwenda kurubisha yai la mwanamke na kutungwa mimba.
Njia hii hufanya kazi kwa ubora zaidi endapo itatumika sambamba na njia nyingine kama vile kutumia mpira wa kiume (condom) wakati wa kujamiina.
Ni muhimu kwa mwanaume kuhakikisha hakuna hata mbegu moja ya kiume itakayotoka wakati uume wake upo ndani yake uke kwani itatosha kubadilisha matokeo.
Njia hii ya uzazi wa mpango ni ngumu kuifanya kwa usahihi kwani humuhitaji mwanaume kuujua mwili wake vizuri.
Angali njia hii inazuia utungwaji wa mimba, haizuii maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwani mengi huambukizwa kwa mgusano wa ngozi wakati wa kujamiana. Kama huna uhakika na afya ya mwenza wako, unashauriwa kutumia mpira wa kiume ili kujikinga na magonjwa hayo.
Lakini pia, unashauriwa kuwa na vidonge vya kuzuia utungwaji mimba, maarufu morning after pills karibu endapo ulishindwa kufanya njia hii kwa usahihi na ukamwaga mwanii ndani ya uke wa mweza wako.
Katika ripoti hiyo, Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro imeonyesha uwepo wa watu wengi wanaotumia njia za uzazi wa mpango.
Aidha, wanawake wa Tanzania Bara walioolewa, wameonekana kutumia zaidi njia za uzazi wa mpango kuliko wanawake wa Zanzibar walioolewa.
MAITI 15 ZAOPOLEWA ZIKIWA KWENYE VIROBA

MAITI 15 ZAOPOLEWA ZIKIWA KWENYE VIROBA

Kuwapo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kuingiwa na hofu ya kuja kutakiwa kuisadia polisi katika uchunguzi wa mauaji hayo, pindi wanapogundua na kutoa taarifa za maiti hizo. Hofu hiyo imesababisha baadhi ya wavuvi kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema kuwa miili iliyookotwa ni mitatu na haikuwa kwenye viroba. “Hadi sasa taarifa za miili mingi kama hiyo kuokotwa nazisikia tu,” alisema Kamanda Mkondya. “Hao watu watueleze nasi tutachukua hatua, hatuna taarifa za miili iliyofungwa kwenye viroba au sandarusi. “Miili mitatu iliyookotwa Kunduchi iko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na haijatambuliwa, wananchi wafike kuitambua.”

Lakini wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maeneo hayo ya uvuvi jana, wavuvi walisema wamepokea taarifa kutoka wenzao wa eneo la Kizimkazi, Zanzibar, kwamba huko nako pia zimeokotwa maiti tano. Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema siku mbili zilizopita ziliokotwa maiti tano katika eneo la Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Dar es Salaam. Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba miguuni, kichwani na tumboni. “Zote zilikuwa zimeharibika na sura hazitambuliki,” alisema na kueleza kuwa zilichukuliwa na polisi baada ya kutaarifiwa. Alisema polisi waliochukua miili hiyo ni wa mkoa wa Kinondoni kutoka vituo vya Kawe ambayo ni wilaya ya kipolisi na Wazo Hill.

“Jamaa zetu wa Feri waliokota maiti sita wiki mbili zilizopita (na) kati yake mbili zimefungwa pamoja na katika hizo moja ni mwanamke. “Tulichozoea wavuvi ni kuokota maiti za wavuvi wenzetu ambaye alizama au kupotea, na zinakuwa na nguo zake za kawaida, lakini hizi ni za kuandaliwa.”

Kwa mujibu wa wavuvi hao, maiti hizo zinatoka maeneo ya ama Dar es Salaam, Pwani, Lindi au Mtwara. Walipoulizwa wamejuaje, walisema bahari ina pepo kuu mbili ambazo ni za Kaskazini na Kusini na kwamba kila mmoja unavyopiga ndivyo vitu au maiti inaweza kusafiri na kukutwa katika eneo fulani. Kwa mujibu wa chanzo hicho, upepo wa sasa hivi unavuma kutoka kusini kwenda Kaskazini, hivyo maiti hizo zisingeweza kuwa zinatokea Tanga ama Kenya, kwa mfano. “Hakuna kinachotoka Kaskazini kuja kusini, ukiona kimekuja huko kimevushwa na upepo kutoka kusini kuja huku,” alisema mmoja wa wavuvi.
HT @ Nipashe
DAR: SERIKALI YAKAMATA MENO YA TEMBO YENYE KILO 376

DAR: SERIKALI YAKAMATA MENO YA TEMBO YENYE KILO 376

Waziri wa Maliasli na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema serikali imefanikiwa kukamata jumla ya meno ya tembo 28 katika ghala moja lililopo Mbezi Beach jijini Dar es salaam, yenye uzito wa takribani kilo 376.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Maghembe amesema meno hayo yaliyokamatwa tarehe 13 na 14 mwezi wa nane mwaka huu yanaonekana ni ya tembo waliouawa miaka ya nyuma ikikadiriwa kuuawa miaka ya 2013 au 2014 na wahalifu hao kuyaweka majumbani mwao huku wakiendelea kutafuta masoko.
MENO YA TEMBOWaziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe akizungumza na waandishi wa habari wakati alipokuwa akiwaonesha jumla ya  meno ya tembo 28 yakiwa na takribani kilo 376  yaliyokamatwa kwenye ghala katika eneo la Mbezi Beach hivi karibuni. Jumla ya watuhumiwa wa ujangili wapatao 6  tayari wameshakamatwa akiwemo Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na Imam wa msikiti wa Huda  wa Mbezi Beach, Aboubakar Zuberi Segumi ( Picha na Lusungu Helela- WMU)
Waziri Maghembe amesema tayari hadi hivi sasa watuhumiwa sita wa ujangili wameshakamtwa akiwemo Mohamedi Yahya Mohamed, almaarufu Mpemba, Aboubakar Zuberi Seguni mkazi wa Mbezi Beach ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali za mtaa na imamu wa msikiti wa Huda uliopo Mbezi, Juma Saleh Jebo mkazi wa Manzese jijini Dar es salaam, Hamisi Rashid Omary mkazi wa Mbezi, Amir Bakari Shelukindo Mkazi wa Gairo Morogoro na Ahmed Shabani Bakari mkazi wa Mkuranga.
Wakati akiwataja watuhumiwa hao,  Waziri Maghembe alisema vita dhidi ya ujangili ni ngumu kwa vile hata baadhi ya watu wasiotegemewa katika jamii kujihusisha nayo  nao wamo, akitolea mfano wa mtuhumiwa, Bakari Zuberi Seguni mkazi wa Mbezi Beach ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali za mtaa na imamu wa msikiti wa Huda uliopo Mbezi  kuwa yeye ni  mfano katika jamii kwa kuwa ni kiongozi wa kiserikali lakini pia ni mtu wa Mungu ambaye ni ngumu kufikiria  ni miongoni mwa  washirika wa biashara hiyo haramu.
Aliongeza kuwa, Tanzania kupitia Wizara yake inataka kufuta kabisa biashara ya meno ya tembo kama China walivyofanya licha ya kuwa uuzaji wa meno ya tembo kwa sasa mara baada ya kufuta soko la wazi imekuwa ikiendelea kwa njia ya mtandao.
Katika hatua nyingine , Waziri Maghemba  alipaza sauti kwa mataifa kama vile Vietnam na Thailand kuacha kujihusisha na biashara hiyo na kuiomba jumuiya ya Kimataifa kuingilia ili tembo waendelee kuwepo kwa faida ya kizazi kijacho na badae na dunia kwa ujumla.
Aidha, Waziri Maghembe amesema Tanzania na Dunia kwa ujumla imepata pigo kubwa baada ya kutokea kwa  mauaji ya Mkurugenzi wa Palm Foundation, Wayne Lotter raia wa Afrika Kusini yaliyotokea usiku wa jana Masaki jijini Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele katika kuisaidia serikali katika vita dhidi ya Ujangili.
MWISHO WA LUGUMI WAWADIA, MAGHOROFA YAKE KUPIGWA MNADA NA SERIKALI

MWISHO WA LUGUMI WAWADIA, MAGHOROFA YAKE KUPIGWA MNADA NA SERIKALI

Kampuni ya Udalali ya Yono imetangaza kupiga mnada majengo matatu ya ghorofa yanayomilikiwa na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Agosti 20 mwaka huu katika gazeti la Sunday News lilitolewa tangazo la mnada wa majengo hayo ambayo ni mali ya Lugumi yanayotarajiwa kupigwa mnada Septemba 9 mwaka huu. Ghorofa moja lipo eneo la Upanga na kwa mujibu wa tangazo hilo, jengo hilo linafaa kwa ofisi na makazi, na majengo mawili ya Mbweni JKT yanafaa kwa makazi.
Scholastica Christian Kevela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono alisema kuwa miezi minne iliyopita nyuma walifungia mali za Lugumi wakimtaka alipe malimbikizo ya kodi aliyokuwa akidaiwa, lakini hadi sasa hajafanya hivyo.
Kiongozi huyo wa Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ni wakala wa serikali wa kukusanya kodi kwa wadiwa sugu ambapo hushirikiana na TRA alisema mdaiwa huyo hajalipa mabilioni ya kodi anayodaiwa na hivyo wao wamepewa amri halali ya kuzipiga mnada nyumba hizo wananzozishikilia.
Kevela alikataa kutaja kiwango cha fedha ambacho Lugumi anadaiwa na TRA akabaki akisisitiza kwamba ni mabilioni ya shilingi na kwamba TRA ndio wanajua kiwango halisi. Hata hivyo hakutangaza thamani ya majengo hayo akisema kwamba, kila mtanzania aje na fedha aliyonayo kwani wao kama madalali hawana kiwango maalum.
Aidha, Kevela aliwataka wananchi kulipa kodi bila shuruti kuepuka nyumba zao kupigwa mnada huku akisema kwamba wasipofanya hivyo na deni lao likafika kwa Yono, wao watafanya kazi yao kiukamilifu.
MAMBO MATATU TUNAYOJIDANGANYA ZAIDI KUHUSU FURAHA NA MAFANIKIO MAISHANI

MAMBO MATATU TUNAYOJIDANGANYA ZAIDI KUHUSU FURAHA NA MAFANIKIO MAISHANI

Ili uwe na maisha mazuri, ni lazima utapitia maisha magumu, yenye mabalaa na misukosuko, bila kujali neno mafanikio au ‘maisha mazuri’ kwako linamaanisha nini. Hutaweza kuishi maisha mazuri mpaka utakapopata ujasiri wa kuweza kuwa mkweli na nafsi yako. Si lazima kuwa mkweli kwa nafsi yako kwa asilimia mia moja, lakini kila unapozidi kuwa mkweli kwa nafsi yako ujue wazi kwamba unazidi kuyasogelea malengo uliyojiwekea.
Watu wenye “mafanikio ” huwa wanazungumza na nafsi zao mara kwa mara – mazungumzo yanayolenga kumnyoosha mustakabali wa maisha yao kuyaelekea malengo waliyojiwekea, na katika mazungumzo haya ya mtu na nafsi yake – wengi wanabaini uongo, na kauli zenye ukweli nusu wanazojiambia wenyewe.
Hakuna anayeweza kuotea mafanikio yanamaanisha nini kwako, lakini kama unaona umekwama kwa sasa, yawezekana kabisa ukawa unakwepa ukweli wa maisha kwa namna moja ama nyingine. Hujayaangalia maisha yako kiundani na kuanza kuihoji nafsi yako.
Zifuatazo ni baadhi ya kauli tunazojiambia ili kujiridhisha na hali tulizonazo hata kama hazituridhishi au tungetamani kuwa kwenye hali ya juu zaidi ya tuliyonayo sasa:

1. Nikipata “x” nitajisikia “y”

Ni jambo gumu sana kuamini kwamba una kila kitu unachohitaji ili kukufanya uwe mwenye maisha ya furaha na ni rahisi sana kujikuta umeingia kwenye mtego wa kufikiria kwamba mafanikio yako yanayofata yatakufanya ujisikie vizuri zaidi. Unajidanganya.
Mafanikio ni matokeo yanayokuja kwa wewe kuridhika kwakuwa unafanya shughuli unayoipenda kutoka moyoni. Mafanikio hayaendi kwa mtu anayefanya kinyume cha hayo (kwa asiyeridhika au kwa anayefanya shughuli asiyoipenda kwa dhati). Hii ni moja ya njiapanda kuu kabisa kimaisha.
Linapokuja swala la maisha yako, bila shaka unafikiria kwamba yanahitaji kurekebishwa kwakuwa kuna jambo haliendi sawa. Unadhani kwamba kuna jambo tofauti na wewe linalohitaji kurekebishwa ili ujisikie vizuri.
Mabadiliko yanatakiwa yaanzie ndani kuja nje (kwamba wewe mwenyewe ndio ubadilike kwanza ndipo uwaze kubadili mambo ya nje). Kuna baadhi ya hatua unazotakiwa kuchukua kwa kiasi kikubwa, mabadiliko yanatokea pale unapobadili mtazamo wako na nini unachohitaji uwe na furaha, ambacho si kingine bali utashi wako mwenyewe.

2. Nataka/naomba ‘x’

Sisi sote ni wabinafsi. Kila mmoja anataka mafanikio, furaha, pesa nyingi, uhuru na muda, mapenzi, afya nzuri — na kila kilicho kizuri maishani, tunakitaka. Kutaka yote haya si vibaya na haiepukiki, lakini kudhani kwamba yanatakiwa yashushwe kwako na wewe uanze kufaidi itakusababishia msongo wa mawazo hasa pale utapoyakosa.
Mara nyingine ukiulizwa swali kwanini unaona unastahili jambo fulani, unaweza kujikuta ukakwama na kushindwa kutoa jibu la kushawishi.
Unasema kwamba unastahili kupata mafanikio na utajiri — kwanini? Nini ulichofanya kinachokupa uhakika kwamba unastahili mafanikio na utajiri huo? Umefanya kazi kwa muda gani kuhakikisha lengo hilo linatimia? Umeyafanyia kazi malengo hayo?
Unadhani kwamba unastahili uhusiano mzuri na wenye utulivu — kwanini? Unaishi vipi na watu wengine? Ni kwa kiasi gani umeweka juhudi kuhakikisha tabia na mienendo yako inaweza kukubalika na watu wa aina unayopenda kuanzisha uhusiano nao badala ya kutaka watu wengine waendane na matakwa na tabia zako?
Haiwezekani kwenda benki kutoa pesa kabla ya kwanza kufungua akaunti na kuweka pesa zako kwenye akaunti hiyo – huu ndio utaratibu wa kimaisha. Huwezi kutarajia kupokea faida tu kama wewe mwenyewe hukufanya uwekezaji kabla. Utakapojua ukweli juu ya hili hutapata tabu unapokosa kitu. Usipoujua ukweli huu au kuamua kuudharau, basi kila mara utaona unaonewa au kutaka kila mtu awe anakutimizia mahitaji yako wewe tu.

3. Mpaka nilipofikia sasa, hakuna ninachoweza kufanya tena

Kuna wengine wanaweza kuona kwamba wamechelewa sana kufanya maamuzi katika ujana wao mpaka walipofikia sasa wanajiona wamechelewa. “Kwa sasa nina miaka 50, sio kijana kama wewe. Ningekuwa na nguvu ningeweza kufanya hayo unayosema, sasa hivi umri umeshakwenda sana.” Kauli kama hizi tumeshazisikia sana na ni kauli zenye uzito.
Lakini kuna mambo mawili yanasahauliwa au watu wenye umri kama huu wanashindwa kuyazingatia. Kwanza ni kwamba inaonesha kuwa tayari wameshakata tamaa kwenye maisha yao. Kana kwamba kufikisha miaka 50 ni sawa na kuvuka mstari wa mwisho kwenye mbio za marathon, kila kitu kinatakiwa kufikia tamati na kuanza kuhuzunika juu ya fursa ambazo ulishindwa kuzitumia maishani.
Pili ni watu wa umri huu kushindwa kujiuliza swali la msingi sana, kwa sasa nina miaka 50 – vipi ikiwa nitajaliwa umri mrefu na kuishi miaka 40 zaidi, maisha yangu yatakuwaje? Labda ukiona kwamba yawezekana ukawa na muda wa kuishi zaidi ndio utajua kwamba inabidi uweke mipango thabiti na kuanza kuitekeleza – bila kujali umechelewa kiasi gani.
VIJUE VITU TISA VILIVYOGUNDULIWA MUDA MREFU ZAIDI YA ULIVYODHANI

VIJUE VITU TISA VILIVYOGUNDULIWA MUDA MREFU ZAIDI YA ULIVYODHANI

Kugundua jambo ni swala linalochukua muda mrefu, na ugunduzi wa mambo au vitu vingi unavyovijua sasa ulifanyika miaka mingi sana iliyopita tofauti na ambavyo wengi wanavyoweza kufikiria. Hii ni kwa sababu ni rahisi sana kufikiria kwakuwa sasa teknolojia imekuwa, basi mambo yamegunduliwa kipindi cha hivi karibuni.
Ukweli ni kwamba maendeleo makubwa ya teknolojia yanayoonekana leo ziligunduliwa na kutengenezwa miaka mingi sana iliyopita.
Zifuatazo ni baadhi ya gunduzi za teknolojia muhimu sana ambazo zilifanyika kabla ya wengi wetu hatujazaliwa.

Kinga ya ugonjwa wa Tetekuwanga – mwaka 1796

Vaccination - 1796
Mwanasayansi Edward Jenner aligundua kinga ya ugonjwa wa Tetekuwanga katika kabla ya karne ya 19 — hii ilikuwa ni awamu ya kwanza tu ya toleo la kinga ya ugonjwa huu.
Mfanyakazi aliyekuwa akihudumia mifugo kwa jina la Sarah Nelmes alimfata Jenner baada ya kuugua tetekuwanga mikononi mwake aliyoambukizwa na ng’ombe aliokuwa akiwahudumia. Jenner alitumia sindano kuchukua majimaji yaliyokuwa ndani ya vimbe hizo na kisha kuyapakaza maji hayo kwenye ngozi ya mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8 ambaye alikuwa mtu wake wa kwanza kumfanyia majaribio ya kinga aliyotengeneza.
Ingawa mtoto huyu alipata homa mwanzoni, ugonjwa wake ulipona haraka sana. Mwanasayansi huyu alipomchoma sindano yenye virusi vya tetekuwanga baada ya kupewa kinga – mtoto huyo hakuugua kabisa.

Betri – mwaka 1800

Battery - 1800
Mnamo Machi 20 mwaka 1800, mgunduzi wa maswala ya teknolojia raia wa Italia aliyejulikana kwa jina la Alessandro Volta alitengeneza betri ya kwanza kutumika duniani. Kwa sasa kampuni hii ya kutengeneza betri mbalimbali ina miaka 217 toka kuanzishwa kwake.
Wakati anazindua beetri hii ya kwanza, Volta aliipa jina la “kifaa cha kubuni cha kutoa umeme” alipoamua kupingana na dhana iliyokuwa kipindi hicho kwamba ilikuwa ni lazima tishu ya mnyama itumike ili kuweza kutengeneza umeme.
Badala yake, alitumia vipande vya chuma na nguo chakavu zilizoloweshwa kwenye maji. Hivi vilitosha kupitisha umeme na ndio ukawa mwanzo wa betri ya kwanza duniani.

Kipaza sauti – mwaka 1876

Microphone - 1876
Muda mfupi baada ya mgunduzi wa kisayansi Alexander Graham Bell kutambulisha ugunduzi wake mpya wa simu, karani wa kijerumani, Emile Berliner aligundua kwamba transmita ya simu hiyo ilikuwa na uwezo mdogo sana. Kwahiyo, akiwa na elimu ndogo sana kuhusu umeme, alianza kufanyia kazi kifaa hicho ambacho alikitumia kukuza sauti inayotoka kwenye simu iliyotenge
Viongozi wa kampuni ya Bell walifurahishwa na maboresho haya hivyo kumuajiri moja kwa moja kwenye maabara ya ubunifu wa kampuni hiyo.

Vioo vya lensi vya kuvaa kwenye macho (Contact lense) – mwaka 1887

Contact lenses - 1887

Katika mabadiliko yaliyokuwa yanafanyika ili watu wanaosumbuliwa na macho wasivae miwani, vioo hivi vilivyotengenezwa katika karne ya 19 vilitengenezwa na kioo kitupu na ilikuwa ni lazima mtu avae kioo hiki kwenye jicho lote.
Mwanzo vilikuwa vinajulikana kama “scleral lenses,” wakimaanisha sehemu nyeupe ya jicho, na viligunduliwa na mtengenezaji wa vifaa bandia vya macho, F.A. Mueller.
Zilikuwa ni kubwa sana lakini wanasema ni bora kwakuwa zilikuwa zikipatikana kirahisi zikiangushwa, tofauti na hizi za sasa.

Ngazi ya umeme – mwaka 1891

Escalator - 1891
Historia inaonesha kuwa ngazi za umeme zilianza kutumika muda mfupi kabla ya kuanza kwa karne ya 20 na mgunduzi alikuwa ni mkazi wa jijini New York nchini Marekani, Jesse Reno.
Aina ya kwanza iliyotengenezwa na Reno ilifungwa kwenye Kisiwa cha Coney kwenye jengo lilikuwa na nguzo pekee ili kuijaribu. Ugunduzi huu ulikubalika mara moja kwa waliokuwa na viwanda na migodi ya madini ambao walikuwa sasa hawalazimiki tena kupanda ngazi kwa miguu wawapo viwandani au kwenye migodi hiyo.

Redio ya gari – mwaka 1919

Hizo zinazoonekana juu ya gari kwenye picha ni waya za redio zinazoning’inia kutoka mbele ya gari hadi nyuma.
Mtengenezaji wa redio hii alikuwa ni fundi mkazi wa jijini New York – Marekani, A. H. Grebe ambaye alijaribu toleo la kwanza la redio ya aina hii ambapo baadaye ilisababisha kuweka mfumo wa redio ndani ya gari kuanzia mwanzoni mwa mwaka 1920.

Moyo wa bandia – mwaka 1961

Artificial heart - 1961
Kwa msaada wa Daktari Henry Heimlich, msanii wa uchekeshaji Paul Winchell alisajili ugunduzi wake wa kubuni mchoro wa kwanza wa moyo wa bandia kwa ajili ya binadamu mwaka 1961.
Kifaa hiki kinajumuisha betri ndogo inayoweza inayoweza kuning’inizwa au kuishika kwa mikono ambayo kazi yake ilikuwa ni kuratibu mdundo na msukumo wa moyo kwa ndani.
Ingawa mamlaka ziliuthibitisha ugunduzi huu miaka miwili baadaye, ilibidi kusubiri mpaka mwaka 1982 pale ugunduzi wa kifaa hiki ulioboreshwa na Dkt. Robert Jarvik’s ulipata ruhusa ya kufanyiwa jaribio la kwanza lenye mafanikio kwenye mwili wa binadamu.

Ndege zisizo na rubani ndani (drone) – mwaka 1964

Drone - 1964

Ndege ya kwanza iliyogunduliwa na kurushwa bila kuwa na rubani ndani yake ni aina ya Lockheed D-21B. Ndege aina hii ya kijeshi ilitumiwa na Jeshi la Marekani kufanya safari za kipelelezi ikiwa kupiga picha kwenye anga la China kati ya mwaka 1969 na 1971 lakini ikaja kusitishwa matumizi yake kutokana na kuanguka mara kwa mara na pia kwakuwa Rais wa Marekani wa kipindi hicho, Richard Nixon kuzindua mfumo mpya wa satelaiti ambao ulikuwa ni mzuri azidi kupiga picha.

Simu za mkononi – mwaka 1973

Cell phone - 1973
Aina ya kwanza kabisa ya simu za mkononi iligunduliwa na mtafiti wa kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Motorola, Martin Cooper (pichani). Simu hizi za toleo la kwanza zilikuwa zinamuwezesha mtumiaji kuongea kwa muda wa sekunde thelathini tu na ilihitaji kuchajiwa kwa muda wa saa kumi hadi kujaa, na ilikuwa na uzito wa kilo 1.3.
ZITTO ADAIWA KUIHUJUMU NDEGE MPYA SERIKALI NCHINI CANADA

ZITTO ADAIWA KUIHUJUMU NDEGE MPYA SERIKALI NCHINI CANADA

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekanusha vikali taarifa zinazosambazwa kwamba ameshiriki katika kuhakikisha ndege mpya ya serikali iliyonunuliwa nchini Canada inashikiliwa kufuatia deni ambalo serikali inadaiwa.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Zitto amesema kwamba madai hayo nitakata zinazotengenezwa na wapika propganda.
“Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi Sana ‘My Country, Right or Wrong’. Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda.
Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo alisema kwamba, suala la ndege ya serikali kuzuiwa Canada lisifanywe ni la ushabiki kama ushabiki wa mpira. Ni suala la Nchi hili na mjadala wake uwe na hadhi hiyo. Kitendo cha Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto. Hakuna mwanasiasa anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi.
Alisema wao kaka vyama vya upinzani ambavyo vipo nje ya serikali wajibu wao ni kuhoji jambo lolo na pia ni haki yao kupata taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali.
“Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa. Majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo. Hili ni suala la kisheria na suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele,” alisema Zitto.
Kuhusu ndege ya serikali kuzuiliwa kutokana na deni inalodaiwa, Zitto alisema, nchi kudaiwa sio dhambi. Hata mataifa makubwa duniani yanadaiwa. Watu binafsi tunadaiwa sembuse Serikali? Mimi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa na wengine wamenipeleka mahakamani. Sio dhambi kudaiwa. Muhimu ni 1) Deni limetokana na nini? Ni maamuzi mabovu ya kisiasa? 2) unalipa deni hilo au kuweka mikakati ya kulipa?
Serikali yetu inafahamu kuwa nchi yetu ina madeni mengi na miongoni mwa madeni hayo yameshaamuliwa na mahakama. Kinachopaswa ni kuwa na maarifa ya kupita ili kuzuia mali zetu nje kuzuiwa kama ilivyo kwa ndege hii. Serikali iwe wazi kuhusu suala hili la ndege. Je! Ile ya Boeing (Terrible Teen) ipo salama? Madeni mengine yenye amri ya mahakama ni yepi? Kwanini Serikali inasubiri kuhojiwa ndio itoe taarifa? aliandika Zitto Kabwe.
Zitto ameitaka serikali kuelezea nini kimetokea na iachane na tabia ya kutafuta mchawi kwamba wanasiasa ndio waliosababisha ndege hiyo kuzuiwa.
Kwa mujibu wa Tundu Lissu, ndege hiyo imezuiliwa nchini Canada na Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd inayoidai serikali USD 38.7 milioni (Tsh 87 bilioni). Ndege hiyo mpya ya serikali ina thamani ya Tsh 70.4 bilioni.
NDEGE NDOGO (DRONE) YAMPELEKA MZEE WA GHANA KUHIJI MAKA

NDEGE NDOGO (DRONE) YAMPELEKA MZEE WA GHANA KUHIJI MAKA

Mzee Al-Hassan Abdullah ni mzee masikini anayeishi kijijini nchini Ghana. Hadithi yake ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini Uturuki baada ya mzee huyo kuwauliza wafanyakazi wa kituo cha runinga cha nchini Uturuki waliokuwa wakirekodi kipindi nchini Ghana iwapo ndege ndogo isiyokuwa na rubani (drone) iliyokuwa inatumiwa na wafanyakazi hao kurekodi “kama ndege hiyo inaweza kumpeleka Makka kuhiji” amesafirishwa kwenda Mji huo Mtakatifu kwa imani ya Uislam kwa gharama za Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na michango iliyotolewa na raia mbalimbali nchini Uturuki walioguswa na alichokisema Mzee Abdullah.
Kilichotokea ni kwamba ndege hiyo ilidondoka karibu kabisa na nyumba ya Mzee Abdullah wakati waandishi hao wanarekodi kipindi maalum. Mzee huyu baada ya kuiona ndege hiyo aliiokota na kumsubiri rubani wake aliyekuwa anaifata aichukue. Akiwa anamkabidhi rubani ndege hiyo, ndipo Mzee Abdullah akamuuliza iwapo wana ndege nyingine kubwa zaidi ya hiyo inayoweza kumpeleka mpaka Makka ili akatimize ibada ya kuhiji kama walivyo mamilioni ya waumini wengine watakaohiji mwaka huu. Rubani huyo aliamua kupimga picha mzee huyu na kuandika maneno aliyoulizwa kisha kuituma kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii. Ujumbe huu ulisambaa mara moja na kuwagusa wengi kiasi cha Serikali ya nchi hiyo kuamua kulipia safari yake. Wananchi walioguswa pia waliweza kutoa mchango wao kama sadaka kumuwezesha kwenda kutimiza ibada hiyo.
Ujumbe wake uliposambaa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini Uturuki, Waziri wa Nchi za Nje, Mevlüt Çavuşoğlu aliguswa na kushughulikia safari ya mzee Abdullah ambaye ni masikini wa kutupwa kwenda Makka. Mzee Abdullah aliwasili jijini Istanbul, Uturuki juzi Ijumaa akitokea Accra, Ghana na alipokewa na Shirika la Misaada nchini Uturuki ambalo limelenga kusaidi nchi ya Ghana.
Mzee Al-Hassan Abdullah: Kushoto alipokuwa anamkabidhi rubani ndege ndogo baada ya kuanguka karibu na nyumba yake Kulia ni katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa Istanbul, Uturuki
Abdullah aliliambia Shirika la Utangazaji la Anadolu la jijini Ankara, Uturuki kuwa amefurahi kuwa jijini Istanbul na kwamba ni Mungu ndiye aliyembariki kuweza kupata msaada kutoka Serikali ya Uturuki. “Namshukuru Mungu na namuombea kila aliyenisaidia kutimiza ndoto yangu. Msaada wa Serikali ya uturuki ni wa muhimu sana kwangu na ninaamini utakuwa ni uthibitisho wa urafiki kati ya mataifa yetu na kuonesha udugu kwa waislam,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya misaada iliyompokea mzee huyu, Cihad Gökdemir amesema kwamba ujumbe wa Mzee Abdullah ulisambaa zaidi kwenye vyombo vyote vya habari nchini humo baada ya mfanyakazi wa kituo hicho cha runinga kuweka picha ya mzee huyo kupitia mtandao wa Twitter. “Hapo ndipo watu wengi walipoanza kuwasiliana na mfanyakazi huyo awaongoze jinsi ya kumsaidia Mzee Abdullah, watu wote – wafanyabiashara hadi makampuni. Mwisho, Ofisa wa Polisi kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini Ghana akawasiliana naye. Anawashukuru sana watu wa Uturuki,” alisema Gökdemir.