ASKOFU MOKIWA AFUTA KESI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imefuta kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa dhidi ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Dk Jacob Chimeledya na Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo, akiomba mahakama imtangaze kuwa askofu halali.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Wakili wa mdai, Mathew Kabunga kudai kuwa yeye na mteja wake wamejadiliana na kwamba Dk Mokiwa ameomba kesi hiyo ifutwe.
Wakili wa wadaiwa, Emmanuel Nkoma alidai hawana pingamizi na hoja zilizotolewa na upande wa mdai kuhusu kufutwa kwa kesi hiyo kwa sababu yeye ndiye aliyefungua shauri hilo.
Pia alidai mdaiwa wa kwanza na wa pili, wameingia gharama za kuweka mawakili katika kesi hiyo kwa ajili ya kujibu madai yao, hivyo mahakama itoe oda ya gharama zilizotumika na usumbufu uliojitokeza kwa wadaiwa hao.
Hakimu Simba alisema shauri hilo linaondolewa mahakamani kama ilivyoombwa na kwamba suala la gharama watajadiliana ni kiasi gani kimetumika ili walipe.
Hata hivyo, Hakimu Simba alitaka kujua kuhusu maombi mengine namba 35 yaliyofunguliwa na Dk Mokiwa ambapo Wakili Kabunga alieleza kuwa maombi hayo hayajapelekwa kwa wadaiwa, hivyo yamepitwa na wakati.
Februari 22, mwaka huu, mawakili wa wadaiwa Gabriel Masingwa na Nkoma walifika mahakamani hapo na kuieleza mahakama kuwa Wakili Kabunga amewapatia barua ya kuomba kufutwa kesi hiyo.
Kwa mujibu wa barua hiyo kutoka kwa wakili wa Dk Mokiwa iliyowasilishwa tarehe hiyo, ilieleza kuwa wanaomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo (Februari 28), irudishwe nyuma kwa kuwa kuna juhudi za kutatua mgogoro katika nyumba ya maaskofu. Barua hiyo ilieleza kuwa mteja wake ana nia ya kuondoa shauri hilo mahakamani kwa kuwa utaratibu wa kumaliza mgogoro huo hauwezi kufanyika iwapo kesi inaendelea mahakamani.
Dk Mokiwa alifungua kesi hiyo namba 20/2017 kupitia Kampuni ya Uwakili ya M. B Kabunga and Co. Advocates, alipinga kuvuliwa uaskofu wake.
Baada ya kufungua kesi hiyo, mawakili wa kanisa hilo, waliamua kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao, wakiiomba kuitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kuisikiliza.
Katika hati yao ya majibu, walalamikiwa hao wanadai hati ya madai haipo sahihi mahakamani hapo, kwa kuwa haina uwezo wa kuingilia masuala ya kiimani kwani yanapaswa kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwenye vyombo vya kidini.
Aidha, wanadai kitendo cha Dk Mokiwa kufungua kesi hiyo mahakamani ni kwenda kinyume na Katiba ya Kanisa la Anglikana ya mwaka 1970 ambayo ilifanyiwa marekebisho Oktoba, 2014.
Hata hivyo, Dk Mokiwa katika hati yake ya madai, anadai kwamba waumini takribani 28 wa kanisa hilo, waliandika barua ikiwa na mashitaka 10 dhidi yake, lakini barua hiyo haikuwasilishwa kwake na kwake ilionesha kuna nakala.
Anadai kwamba Desemba 20, mwaka jana, mlalamikiwa wa kwanza (Dk Chimeledya) alimuandikia barua kumtaka kustaafu mwenyewe katika nafasi yake bila ya kueleza sababu na kumpa nafasi ya kuweza kujibu tuhuma.
Kwa kupitia hati yake ya madai, Dk Mokiwa anadai kwamba tuhuma hizo hazina vielelezo vyovyote vya kuthibitisha tuhuma hizo, bali ni mambo ya kupika kumharibia askofu huyo.
Kutokana na hayo, anaiomba mahakama kuamuru Dk Mokiwa ni askofu halali, kumlipa gharama za kesi na kutoa amri nyingine inazoona zinafaa.
Aidha, Januari 7, mwaka huu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Chimeledya alimvua uaskofu mkuu Dk Mokiwa kutokana na mashitaka 10 aliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa.
Uamuzi wa kumvua uaskofu ulichukuliwa baada ya Dk Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.
Hata hivyo, Dk Mokiwa aliugomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.
Dk Mokiwa alikuwa akituhumiwa kwa mashitaka 10 ikiwemo kuzuia Dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume cha Katiba ya dayosisi.
Chanzo:HabariLeo 01/03/2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post