KAMPUNI ZAPINGA MAHAKAMA ZUIO LA VIROBA

Serikali imetangaza kwamba kuanzia kesho itaanza operesheni kukagua utekelezaji zuio la utengenezaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali, zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba) huku ikibainisha kuwa itatoa adhabu zikiwemo faini za hadi Sh milioni tano au jela au vyote kwa pamoja, kwa watakaokiuka marufuku hiyo.
Serikali imetangaza kupiga marufuku utengenezaji, uuzaji au utumiaji wa pombe kali zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba), kwa kuwa zimebainika kwamba mbali ya kuikosesha mapato serikali yanayofikia Sh bilioni 600 kwa mwaka, zimekuwa zikitumiwa isivyo kutokana na ufungashaji wake wa kirahisi.
Aidha, wakati serikali ikitoa agizo hilo, kampuni tano zimeifungulia kesi serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hatua ya utekelezwaji wa agizo la kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vya pombe kali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji wa uingizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya pombe hizo.
“Operesheni hii itafanyika Machi 2, 2017 nchi nzima, kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mitaa... Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Tamisemi na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais,” alieleza January.
Alisema utekelezaji wa katazo hilo utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230(2)(f) cha sheria hiyo na Sheria ya Leseni za Vileo namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012.
“Kanuni namba saba ndio inatoa makosa na adhabu ambapo anayeingiza viroba faini itakuwa si chini ya shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote kwa pamoja, kuzalisha faini itakuwa isiyopungua milioni mbili au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote kwa pamoja,” alieleza January.
Alisema kwa watakaokutwa wakiuza, kuhifadhi au kusambaza faini itakuwa isiyopungua Sh 100,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote na kwa watakaokutwa wakimiliki kiroba, kuwa nacho na kukitumia kiroba faini itakuwa isiyopungua Sh 50,000 au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Alisema serikali ilitoa muda wa kutosha katika suala hilo ambapo kwenye Bunge la Mei mwaka jana lilizungumzwa na kutangazwa kwamba viroba na mifuko ya plastiki imepigwa marufuku na mwisho ilitangazwa kuwa ingekuwa Januari mwaka huu.
Alieleza kuwa kama kuna mtu aliagiza mzigo baada ya hapo au kuzalisha ni kwamba aliipuuza serikali na hoja zao hazina mashiko kwa sababu walikaidi.
“Iwapo baada ya taarifa hizo za serikali kuna mzalishaji ameagiza malighafi au kutengeneza au kuhifadhi pombe za viroba au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo atakuwa amefanya hivyo akijua madhara yake.
“Kwa ambao wanataka kwenda mahakamani sisi tunaamini kama serikali tupo kwenye mstari sahihi. Hoja zote za kisheria zipo upande wetu, kwa kuwa hoja kubwa wanasema ni muda ila ushahidi upo kabisa kwamba tulitangaza tangu Mei mwaka jana na tulisema mwisho ingekuwa ni Januari mwaka huu,” alifafanua.
Alisema, “serikali ina wajibu wa kutoa utaratibu mambo yaendeshwe vipi katika jamii, hivyo unapoenda mahakamani kushitaki ili serikali isilinde watu wake sidhani kama utafanikiwa sana, hivyo sisi tutaendelea kufanya yale tunayotegemewa nayo na tuna uhakika muda ulikuwa ni wa kutosha sana.”
Alisema serikali ina malengo matatu katika operesheni hiyo ikiwemo usafi wa mazingira, kuangalia afya ya jamii ambapo wamegundua kwamba upatikanaji wa pombe kali kwa bei rahisi kwa wakati wote ni janga kwa jamii na hiyo inatokana na ufungashaji wake, hivyo vikiondolewa vifungashio hivyo itasaidia kuondoa upatikanaji wa rahisi.
“Uhalifu na ajali zinaongezeka barabarani kwa sababu ya pombe za viroba. Asilimia 68 ya wanaopata ajali za pikipiki wanakuwa wamekunywa viroba...serikali inapoteza bilioni 600 kwa mwaka kutokana na uzalishaji wa viroba. Tunataka kiwango cha pombe kinachonywewa kiendane na kodi inayolipwa,” alibainisha.
Alisema Februari 24, mwaka huu, kiliitishwa kikao cha mawaziri na viongozi wa taasisi za serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hilo ambapo wizara na taasisi za serikali zilipewa majukumu mbalimbali.
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki.
Aidha, alisema TRA itahakikisha wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa.
"Tangazo letu la Februari 20, 2017 lilionesha muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa na watahitaji muda mchache kufanya hivyo na ambao watatimiza masharti wangepata kibali maalum kabla ya Februari 28, 2017,” alisema.
Alisema kutokana na tangazo hilo, serikali ilipokea maombi ya wazalishaji tisa pekee na watatangaza endapo kuna waliokidhi masharti au la.
Pia alisema wamepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hilo limekuja ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala, lakini ukweli ni kwamba serikali ilishatangaza na imekuwa ikikumbusha mara kadhaa kuhusu hatua hizo.
Alitoa mwito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa operesheni hiyo ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki. Alisema zawadi zitatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.
Kuhusu mifuko ya plastiki, alisema kanuni za udhibiti zinaandaliwa na zuio litatangazwa wakati wowote na kuwaasa wazalishaji, waingizaji na wauzaji nao kujiandaa.
Wakati serikali ikitoa agizo hilo, kampuni tano zimeifungulia kesi serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hatua ya utekelezwaji wa agizo la kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vya pombe kali.
Kampuni hizo ni Pama Group Ltd, Triple S Investment Ltd, Canon General Supplies Ltd, Mwanza Lake Line Industries Ltd na Kichuri Investment Ltd, ambazo zimefungua kesi dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Wakili wa wadai, Salim Mushi alidai wamefungua kesi hiyo namba 18/2017 katika Mahakama Kuu kanda hiyo, kupinga utekelezaji wa agizo hilo unaotakiwa kuanza leo.
Mushi amedai kuwa kesi hiyo inatarajiwa kupangiwa jaji leo kwa ajili ya kupanga tarehe ya usikilizwaji.
Alieleza kuwa katika hati hiyo ya madai, wateja wake wanaiomba mahakama kuzuia mpango wa serikali kutekeleza mpango wake wa kupiga marufuku matumizi ya viroba.
Pia anadai kuwa wateja wake wanalalamika kuwa wadau hawajawahi kupewa nafasi ya kusikilizwa, pamoja na kuwa na vibali vyote vya biashara. Aidha, anadai kuwa hakuna sheria yoyote ambayo inazuia suala hilo la matumizi ya viroba.
Chanzo:HabariLeo 03/01/2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post