KITUO CHA EATV NA HAWA FOUNDATION WAZINDUA KAMPENI YA KUCHANGISHA FEDHA KUWASAIDIA WASICHANA WANAFUNZI WA SHULE ZA SEKONDARI WAKATI WA HEDHI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA), Joyce Kiria akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) mapema leo Jijini Dar, kuhusiana na uzinduzi wa Kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wasichana na wanafunzi wa shule za sekondari nchini Tanzania, kulia kwake Afisa Masoko wa EATV, Brendansia Kileo.
Kituo namba moja kwa vijana nchini cha East Africa Television LTD (EATV) kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) kimeanzisha kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya wasichana wanafunzi wa Shule za Sekondari nchini Tanzania kwa ajili ya kununulia taulo za hedhi (Pedi) ili kuwastiri na kulinda utu wao.

Kampeni hii inayozinduliwa leo inafanyika wakati huu ambao tukielekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, nasi kama kituo cha habari kinachofanya biashara zake nchini tumeona tunawajibu wa kutumia vituo vyetu vya EATV na East Africa Radio kuhamasisha jamii kuwachangia watoto wetu wa kike kutatua tatizo hili.

Kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria shule kwa kati ya siku tano hadi saba kutokana na kukosa pedi za kujisitiri wakati wa hedhi, ambapo kwa mwaka inakadiriwa mwanafunzi wa kike hukosa kuhudhuria shule kwa siku 60 hadi 70 kutokana na kukosa pedi tu, hali ambayo inachangia kutofanya vizuri kimasomo.

Wengi wa wanafunzi wa kike pia wamekuwa wakihatarisha afya zao kwa kutumia matambara kwa ajili ya kujisitiri wakati wa hedhi, hali ambayo pia imekuwa ikiwasababishia aibu pale vitambaa hivyo vinapovujisha damu ya hedhi na kubainika na wanafunzi wenzake shuleni.

Katika kampeni hii ya kumuwezesha mtoto wa kike kuhudhuria shule bila ya kukosa kwa sababu ya hedhi, fedha zote zitakazokusanywa katika kampeni hii zitatumika kununulia pedi na kusambazwa kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari zitakazo chaguliwa nchini Tanzania kwa mwaka mmoja.

Ili kuchangia kampeni hii tunatarajia kila mwananchi atakayeguswa na tatizo hili kuchangia kiasi cha kuanzia shilingi 5,000 tu, na fedha zitakazopatikana zitasaidia kuwawezesha watoto wakike wengi ipasavyo nchini kupata pedi na kuhudhuria shule kwa mwaka mzima bila kuwa na hofu wakati wa siku zake za hedhi.

Katika kampeni hii EATV na East Africa Radio itahamasisha uchangiaji wa fedha na Taasisi ya Haki za Wanawake, (HAWA Foundation) iliyosajiliwa kwa mujibu wa taratibu za nchi mwaka 2011, itahusika na kupokea na kusimamia fedha zote zitakazochangishwa na kusimamia ununuzi na usambazaji wa pedi hizo mashuleni.

Tatizo la wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria shuleni kutokana na kukosa pedi za kujisitiri ni la kwetu sote tuungane pamoja kuwasaidia watoto wetu wa kike ili kuhudhuria masomo bila kukosa.

Jinsi ya kuchangia unaweza kutuma fedha hizo kupitia kwa M-PESA Code Namba 5530307 ama kupitia akaunti ya CRDB Namba 0150258750600.


#Namthamini
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post