LUKUVI AMBANA ALIYEMPA ARDHI MAKONDA

MFANYABISHARA Mohamed Ikbal, aliyemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda eneo la ekari 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo ameibuka na kudai kuwa eneo hilo ni lake na anavidhibitisho vyote vya umiliki.
Kauli ya mfanyabiashara huyo imekuja baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutangaza kumchukulia hatua mfanyabiashara huyo kwa kutangaza kutoa eneo hilo wakati linamilikiwa na serikali na si mali yake.
Hata hivyo Waziri Lukuvi akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana aliendelea kushikilia msimamo wa serikali kuwa eneo hilo si la mfanyabiashara huyo kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama, ambayo ilitupilia mbali shauri lake kutokana na kushindwa kuwasilisha ushahidi wa umiliki wake halali wa eneo hilo.
Waziri Lukuvi amesema katika mazungumzo hayo kuwa shauri la mahakama huenda kwa kukata rufaa na si nje na kama hakuwa ameridhika na maamuzi alistahili kukata rufaa.
“Uamuzi kuwa eneo lile si mali ya Ikbal ulitolewa na Mahakama, na kama inavyofahamika uamuzi wa Mahakama unahojiwa mahakamani na si nje ya Mahakama. Kama ni eneo lake na vielelezo anavyo, ni kwanini hakuviwasilisha mahakamani hadi akashindwa kesi?” alihoji Lukuvi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Ikbal jana, Kamugisha Katabaro alisema, Ikbal ni mmiliki wa eneo la ekari 3,500 lililopo Lingato, Kisarawe II, Kigamboni ambalo alilinunua tangu mwanzoni mwa mwaka 2005 kutoka kwa wananchi wa eneo hilo ambao waliuza kwa hiyari yao wenyewe kwa kufuata taratibu zote za kisheria za ununuzi na umiliki wa ardhi.
“Ushahidi wa nakala za barua ya mawasiliano kati ya ofisi ya serikali ya mtaa wa Lingato, mihutasari ya kikao ya maamuzi ya serikali ya mtaa na mikutano ya wananchi waliokuwa wamiliki wa maeneo hayo ipo,” alisema Katabaro.
Aidha aliongeza kuwa nakala za risiti za malipo ya ushuru wa serikali kama sheria inavyotaka, mikataba ya mauziano ya ardhi sambamba na picha za wamiliki wa maeneo wakipokea pesa za mauziano ya ardhi zipo na zitawekwa bayana pale itakapohitajika.
Alisema miaka michache baada ya mauziano ya ardhi baadhi ya wauzaji walianza kuingiwa na tamaa kutokana na kupanda kwa thamani ya ardhi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wasio waaminifu, na kuanza kuvamia eneo lake, na baadaye waliwasilisha malalamiko yao kwa Kamishna wa Ardhi kwamba wananyanyaswa katika ardhi yao na kwamba hawakuuza maeneo yao kwa hiari yao.
Katabaro alisema mchakato wa kulipitia eneo hilo ili kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda ulizingatia taratibu zote lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza viwanda.
Pamoja na maelezo hayo Lukuvi alisema kwamba Mkuu wa mkoa Paul Makonda ataendelea na mpango wa uwekezaji kama alivyosema katika kikao cha mwisho na waandishi wa habari kwamba serikali itaendelea na uwekezaji katika eneo hilo ambalo si la Ikbal.
Alisema kwamba Yeye na Makonda wameshazungumza na wote wawili wanatekeleza maagizo ya serikali. Waziri huyo akizungumzia mipango ya uwekezaji wa viwanda katika eneo hilo kama ilivyoelezwa na Mkuu wa Mkoa Makonda, Lukuvi alisema; “
Hilo nililisema tangu siku ile, Makonda anatekeleza mipango ya serikali na mimi natekeleza mipango ya serikali, hivyo ni lazima tusimamie kwa pamoja ili kuhakikisha mipango ya serikali inatekelezwa,” alisema Lukuvi.
Kesi hiyo iliyokuwa dhidi ya kijiji cha Lingato ya mwaka 2015 ilikuwa katika mahakama ya ardhi Temeke ikiwa na namba 147 ya mwaka huo.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post