NAY WA MITEGO AKUBALI KUTEKELEZA USHAURI WA RAIS DKT MAGUFULI

Mwanamuziki Emmanuel Elibariki maarufu kama Nay wa Mitego ameahidi kutekeleza ushauri wa Rais John Magufuli wa kuongeza maneno yenye ujumbe katika wimbo wake wa ‘WAPO’ ambao umeibua mjadala mkubwa nchini.
Alizungumza hayo jana mara baada ya kutoka kuzungumza na Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe katika ofisi za wizara hiyo mjini Dodoma.
Ney pia aliwataka wasanii wenzake kutokuwa na woga katika kutunga nyimbo zao, ila tu wasikiuke mipaka ya uhuru wao.
“Waswahili wanasema usikatae wito kata maneno, kwa bahati nzuri maneno aliyoniambia waziri yamekuwa ni ya kutia moyo. Namshukuru Rais kwa kuwa muelewa” alisema.
Ney ambaye alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma kuwa wimbo wake unaikashifu serikali, na wimbo huo kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) aliachiliwa huru baada ya agizo la Mh. Rais kupitia Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe.
Nay alisema kuwa alishangazwa na kitendo cha mtu maarufu kama yeye kukamatwa kwa mtindo ule, ilihali Polisi wangeweza kumuita na yeye kwenda bila tatizo.
Hata hivyo aliwashukuru watanzania wote kwa kumpa ushirikiano katika wakati wote.
Akizungumzia kuhusu ‘remix’ ya wimbo wake, Nay alisema kuwa, atawashirikisha wasanii wengine na kuwaomba watanzania ambao wana maneno wanayotaka yaongezwe wafanye hivyo kwa sababu wimbo ni wao.
“Nawasihi wasanii wenzangu tupendane, ukisikia kuwa kuna mwenzako amepata matatizo, usifurahie, bali tuungane kusaidiana. Pia nawataka wasiwe waoga wala wasivuke mipaka” alisema.
Kwa upande wa waziri Dkt. Harrisom Mwakyembe alisema kuwa hakumuita mwanamuziki Nay kwa sababu ya kumtisha au kumuonya, bali kama mlezi wake.
“Ujumbe wangu kwake na kwa watu wengine wa tasnia hii ya muziki ni kuwa, Tanzania ni nchi inayoheshimu utawala wa sheria, watu wana uhuru wa kusema lakini pia una mipaka yake” Alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa inapotokea matatizo kama yaliyojitokeza kwa msanii Nay, wahusika wasichukue hatua kabla ya kufanya mashauriano.
Akimalizia Nay wa Mitego alisema marudio ya wimbo huo yatakamilika baada ya wiki moja au mbili kutokea sasa.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post