POLISI WASHIKILIA WATU 43 KWA VIROBA NA MIHADARATI

POLISI mkoani Kilimanjaro inawashikilia watu 43 kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbroad Mutafungwa alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti, kati ya Machi 5 na Machi 10, mwaka huu.

Alisema jeshi hilo linaendelea na msako wa kukamata watu wanaojihusisha na uuzaji wa pombe za viroba na kufanikiwa kukamata watu 31 wakiwa na katoni 1,529 za pombe za aina mbalimbali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki, paketi mbili za pombe hizo pamoja na vifungashio 167.

Kuhusu dawa za kulevya, alisema wamekamata watu 12 wakiwa na misokoto 216 na gramu 253 za bangi, mirungi kilo 64 na gramu 810 pamoja na miche 1,258 ya mirungi.

Akielezea jinsi baadhi ya watuhumiwa walivyokamatwa, alisema Machi 7, mwaka huu katika eneo la Kiriniiko, Same, askari polisi walimkamata Emmanuel Lameck (32) ambaye ni dereva wa gari aina ya Scania yenye namba T 645 ABJ/T 699 DDC na utingo wake Said Salum (26) wakisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.

Alisema watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na bunda 176 za mirungi ambayo ni sawa na kilo 61, walihifadhi kwenye mifuko ya sandarusi, ikisafirishwa kutoka Moshi kwenda Tanga.

“Mbinu ya kutumia magari makubwa ya mizigo na kuhifadhi dawa kwenye cabin ya dereva ni ngumu kuijua, lakini kwa jinsi tulivyojipanga kwenye vita hii hakuna mbinu mpya itakayotumiwa na wasafirishaji hao tutashindwa kuibaini,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Aidha, alisema kati ya Februari 28 na Machi 9 mwaka huu, katika maeneo tofauti mkoani hapa, wamewakamata watu watatu waliokutwa na bastola.

Alisema watuhumiwa hao ni mkazi wa Mamba Mwika, Stephen Mbando (45) alikamatwa akiwa na bastola aina ya Browning yenye risasi tisa, moja ilikuwa tayari kutumika, mkazi wa Kichwa cha Ng’ombe, Isaya Fideles (30) alikutwa na bastola aina ya Chinese na mkazi wa Kahe, Yahaya Semboje (32) alikutwa na bastola isiyokuwa na namba.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post