RAIS MAGUFULI ATEMBELEA KIWANDA CHA DANGOTE, ATOA SIKU 7 KWA WAZIRI MUHONGO ATIMIZE MAAGIZO YAKE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya Nishati na Madini kumega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 05 Machi, 2017 wakati wa uzinduzi wa magari 580 ya kusafirishia saruji ya Kampuni ya Dangote uliofanyika kiwandani hapo na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Mmiliki wa kiwanda cha Dangote Alhaji Aliko Dangote.
Pamoja kuagiza kampuni ya Dangote ipatiwe eneo la kuchimba makaa ya mawe, Mhe. Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka kampuni ya saruji ya Dangote kuwasiliana moja kwa moja na Serikali pale inahitaji huduma yoyote badala ya kuwatumia watu wa kati ambao wamekuwa wakisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na bidhaa na hivyo kuathiri uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho.
Kabla ya kuzindua rasmi magari hayo Mhe. Rais Magufuli amepokea kero za madereva ambao walifanya usaili wa kuomba kazi ya kuendesha magari hayo tangu miezi miwili iliyopita, ambapo wamemueleza kuwa menejimenti ya kiwanda hicho haijawaita kazini mpaka leo licha ya kuwepo kwa malori mapya wanayopaswa kuendesha, huku Menejimenti ikiendelea kutumia malori ya watu binafsi kupitia kampuni za kati ambazo ndizo zimekuwa zikitumika kutoa huduma nyingi kwa kiwanda.
Kufuatia malalamiko hayo Mhe. Dkt. Magufuli amemshauri mmiliki wa kiwanda hicho Alhaji Aliko Dangote kuiangalia vizuri Menejimenti yake na kuitaka iachane na wafanyabiashara wa kati ikiwemo kampuni moja iliyotaka kupewa zabuni ya kupokea gesi kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kisha kuzalisha umeme na kuiuzia Dangote.
“Ndugu Alhaji Aliko Dangote, iangalie vizuri Menejimenti yako, inawatumia watu wa kati na ndio hao wanaosababisha matatizo, na mimi nimeshaiagiza wizara hakuna kuuza gesi kwa watu wa kati, tunataka tukuletee gesi wewe mwenyewe na uzalishe umeme wewe mwenyewe” amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Alhaji Aliko Dangote ameelezea kufurahishwa kwake na uwekezaji wa kiwanda hicho uliogharimu Dola za Marekani Milioni 650 na kwamba kiwanda hicho kitakachozalisha tani Milioni 2 za saruji mwaka huu kinatarajia kufikia uzalishaji wa tani Milioni 3 mwaka ujao, kuzalisha ajira 20,000 huku kikiwa kimesaidia kupunguza bei ya saruji nchini kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/-.
Alhaji Aliko Dangote ameongeza kuwa tangu kampuni yake ianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/- na kwamba imeamua kununua magari ya kusafirisha saruji ili iweze kusambaza saruji hiyo nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi wataimudu.
Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema licha ya kuzalisha ajira, tangu kampuni hiyo ianze shughuli zake imeshalipa kodi kiasi cha Shilingi Bilioni 46.139 na kodi inatarajiwa kuongezeka kadiri uzalishaji unavyopanda.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezindua kituo cha kupooza umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kilichopo mjini Mtwara ambacho kinajengwa kwa fedha na wataalamu wa TANESCO kwa gharama ya Shilingi Bilioni 16, mradi ambao utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi na hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Lindi.
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO kwa kazi nzuri wanayofanya iliyowezesha usambazaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia asilimia 46 ya nchi nzima, lakini ametoa maagizo kwa TANESCO kuwakatia umeme wote wenye madeni bila kujali kama ni taasisi ya umma ama binafsi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amesali ibada ya Diminika ya kwanza ya Kwaresma katika Kanisa la Watakatifu wote, Jimbo Katoliki la Mtwara ambako amechangia Shilingi Milioni 1 na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Kanisa na ukarabati wa Kanisa na amewataka wananchi wa Mtwara kushikamana kuiombea nchi na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na Taifa zima.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote mara baada ya kuwasili kiwandani hapo kwa ajili ya kuzindua magari 580 ya kusafirisha saruji nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote mara baada ya kumkabidhi barua ya malalamiko kutoka kwa madereva wanaolalamikia utoaji wa ajira hizo kiwandani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia katika viwanja hivyo vya kiwanda cha Dangote kabla kuzindua magari 580 ya kiwanda hicho yatakayosafirisha saruji nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Magari makubwa ya kusafirishia Saruji kiwanda hapo. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego March 5, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote mara baada ya kukagua kiwanda chake cha Saruji mkoani Mtwara.
Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote akimuonesha Rais Dkt. Magufuli sehemu ya Kiwanda hicho pamoja na vifaa vyake mkoani Mtwara.
Rais Dkt. Magufuli akizungumza jambo na mmiliki huyo wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote.
Rais Dkt. Magufuli akizungumza jambo na mmiliki huyo wa Kiwanda akiwa na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Alhaji Aliko Dangote wakipeperusha bendera kuashiria uzinduzi rasmi wa Magari hayo 580.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiweka jiwe la msingi Mradi wa Kituo cha kupooza umeme kwa ajili ya kuusambaza katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo March 5, 2017
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria kuzindua kituo cha kupooza umeme kwa ajili ya kuusambaza katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na wafanyakazi wa TANESCO mara baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo cha kupooza umeme kwa ajili ya kuusambaza katika mikoa ya Lindi na Mtwara kilichopo mkoani Mtwara.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kabla ya kuweka jiwe la msingi la kituo cha kupooza umeme kwa ajili ya kuusambaza katika mikoa ya Lindi na Mtwara kilichopo mkoani Mtwara.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika kituo hicho cha kupooza umeme
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ibada ya jumapili ya kwanza ya kwaresma katika kanisa la Katoliki la Watakatifu Wote jimbo la Mtwara March 5, 2017
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwatakia heri waumini wa kanisa la Katoliki la Watakatifu Wote jimbo la Mtwara
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na waumini hao wa kanisa la Katoliki la Watakatifu Wote jimbo la Mtwara
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na wanafunzi wa Shule za Sekondari mara baada ya kusali katika kanisa la Katoliki la Watakatifu Wote jimbo la Mtwara
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
05 Machi, 2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post