RAIS MAGUFULI NA WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA WAKUBALIANA KUKUZA ZAIDI UHUSIANO NA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI

Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi na kukabiliana na umasikini wa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe. Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Miongoni mwa maeneo ambayo Mhe. Hailemariam Dessalegn amesema atatilia mkazo ni ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo ameahidi kuwatuma wataalamu kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na Wataalamu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji kazi na kuikuza ATCL.
“Shirika letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani Afrika, lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege zake zinatua katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya Ethiopia, hivyo nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje washirikiane na ATCL kuweka mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na kuiwezesha kufanya kazi kwa faida” amesema Mhe. Hailemariam Dessalegn.
Pia amesema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza na wananchi wamefanya mazungumzo rasmi, wamesema wamekubaliana kuwa Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn ameahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa uitwao Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha megawatts 6,470 za umeme.
“Mhe. Waziri Mkuu tutafurahi sana kushirikiana nanyi katika suala la uzalishaji wa nishati ya umeme kwa sababu hata sisi tunaweza kuzalisha umeme mwingi katika maporomoko ya maji ya Stiegler’s Gorge yaliyopo katika mto Rufiji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi hao wamekubaliana kushirikiana kufanya mapinduzi ya kilimo na mifugo, hasa ikizingatiwa kuwa Ethiopia inaongoza kwa idadi kubwa ya ng’ombe barani Afrika na Tanzania inashika nafasi ya pili na kwamba juhudi hizo zitakwenda sambamba na kujenga viwanda vingi vitakavyoongeza thamani ya mazao.
“Naamini kuwa tukishirikiana katika kilimo na mifugo, tutaweza kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao ikiwemo ngozi na nyama na tutatumia mashirika yetu ya ndege kuyafikia masoko mbalimbali duniani na hivyo kukuza uchumi na kuwaongezea wakulima wetu kipato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana kwa kubalishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na gesi, elimu na  mawasiliano hususani simu.
Mhe. Rais Magufuli amesema ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Hailemariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba 3 ambayo ni Mkataba wa Mkakati wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia, Mkataba wa kuanzishwa Kamisheni ya Pamoja ya Kuduma kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia.
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na akiwa uwanjani hapo amepigiwa mizinga 19, amekagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake na ameshuhudia burudani ya ngoma za asili.
Jioni hii, Mhe. Hailemariam Dessalegn atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na kumpokea mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal One jijini Dar es Salaam March 31,2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal One jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn wakati nyimbo za mataifa mawili (Tanzania na Ethiopia) zikipigwa mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal One jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn akishuka kwenye jukwaa kwenda kukagua gwaride la Heshma lililoandaliwa kwa ajili yake.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn akikagua Gwaride la heshma lililoandaliwa kwa ajili yake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn Ikulu jijini Dar es salaam
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn akipiga ngoma mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam, Pembeni yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpigia makofi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akizungumza na Wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn akifurahia jambo wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza na Wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn akizungumza na Wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya mkutano wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimtambulisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Eng. John Kijazi kwa mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn Ikulu jijini Dar es Salaam.
Shamra shamra zikiendelea wakati wa kuwasili Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 2 jijini Dar es Salaam

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Machi, 2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post