TAARIFA YA ZIARA YA MAZINGIRA YA WAZIRI MAKAMBA KATIKA HALMASHAURI YA KOROGWE, TANGA

Taarifa ya siku ya tano ya ziara maalum ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Mhe January Makamba katika mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania inayolenga kutambua changamoto za kimazingira katika mikoa hiyo na kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuweka mahusiano bora zaidi katika utunzaji wa Mazingira kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mtaa, watu binafsi na taasisi za mazingira.
WhatsApp Image 2017-03-25 at 9.09.35 AM
Akimaliza ziara yake katika mkoa wa Tanga Waziri Makamba ameshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Halmashauri ya Mji wa Korogwe akiongozana na viongozi, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Korogwe.
Baada ya zoezi la upandaji miti Waziri Makamba amepokea taarifa ya mazingira ya Halmashauri ya Korogwe ambayo pamoja na mambo mengine imeainisha changamoto mbalimbali za mazingira zikiwemo uwezo mdogo wa Halmashauri kuzoa na kutupa taka ngumu pamoja na uzoaji na utupaji wa majitaka, ongezeko la watu katika maeneo yanayozunguka misitu na vyanzo vya maji kama mto Pangani hivyo kuongeza shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo jambo linalopelekea kuhatarisha utunzwaji wa vyanzo hivyo.
Akizungumza na viongozi, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Korogwe katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Waziri Makamba amesisitiza utunzwaji wa mazingira huku akisisitiza Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais zimedhamiria kuweka hifadhi ya mazingira katikati ya ajenda zake za maendeleo.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira ni muhimu na hata shughuli za msingi za kibinadamu kama kilimo haziwezi kufanikiwa kama ukataji miti utaendelea, na hata ufugaji hautakuwepo kwasababu hakutakuwa na mvua hivyo mazao hayatastawi na malisho ya mifugo yatakosekana.
WhatsApp Image 2017-03-25 at 9.10.00 AM
“Vyanzo vya maji na mito, hali si nzuri, maji yamepungua, mito iliyokuwa inatiririsha maji mwaka mzima imekuwa ya msimu na iliyokuwa ya msimu imekauka, tusiwe na huruma na mwaharibifu wa vyanzo vya maji, huyu ni mhaini/gaidi wa mazingira yetu aliye tayari kuharibu vyanzo kwa manufaa yake huku akiharibu ustawi wa watu wengi” Alisisitiza Waziri Makamba.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa kamati za ulinzi na usalama zikutane angalau mara moja kwa ajenda ya Mazingira na hata askari wakifanya doria suala la mazingira liwepo vivyo hivyo katika vikao na mikutano ya viongozi wa serikali za mitaa ajenda za mazingira zipewe kipaumbele.
Akijibu suala la upungufu wa wakaguzi mazingira amesema kuwa Serikali tayari imepata wakaguzi wa mazingira 200 ambao watasambazwa nchi nzima na watapatiwa mafunzo kabla ya kusambazwa kwenye vituo vya kazi. Katika changamoto ya uchimbaji mchanga ameeleza kuwa katika Bunge lijalo wizara yake itawasilisha mwongozo wa kitaifa wa kusimamia shughuli za uchimbaji mchanga nchi nzima lakini kabla ya hapo inapaswa kuhakikisha
suala la uchimbaji mchanga linakomeshwa.
Akiwa anamaliza ziara yake katika mkoa wa Tanga Waziri Makamba ametoa miche 10000 ya miti kwaajili ya Halmashauri ya Korogwe huku pia akitoa mifuko 200 ya sementi kwaajili ya kuchangia shughuli za maendeleo katika Halmashauri hiyo.
WhatsApp Image 2017-03-25 at 9.10.13 AM
Baada ya kuhitimisha shughuli katika mkoa wa Tanga Waziri Makamba ameanza ziara katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo amewasili katika Wilaya ya Same na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bi Rosemary Staki ambaye aliwasilisha taarifa ya mazingira ya wilaya. Katika taarifa hiyo Bi Rosemary ameianisha changamoto mbalimbali zinazoiikabili wilaya hiyo ambayo ina uoto wa nusu jangwa (semi-arid) kuwa ni pamoja makorongo yanatokana na mvua kubwa toka milimani, uchomaji misitu hasa misitu ya asili Chome, shughuli za ufugaji holela na kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja uchimbaji wa madini usiozingatia kanuni za utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Vilevile Bi Rosemary amemweleza Waziri Makamba juu ya tishio lililopo katika eneo la Ndolwa kata ya Mamba-Miamba ambapo kuna dalili za kutokea kwa maporomoko ya ardhi ambapo amemwomba Waziri kuchukua hatua za haraka ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza siku za mbeleni.
Akiwa wilayani Same Waziri Makamba amepata wasaa wa kutembelea na kukagua shughuli za uhifadhi na utunzaji
wa mazingira katika eneo la hifadhi ya Mkomazi ambapo kabla ya shughuli za ukaguzi alipokea taarifa fupi ya mazingira ya hifadhi hiyo. Waziri Makamba amejionea changamoto kadha wa kadha zinazoikumba hifadhi hiyo ikiwemo uingizwaji mifugo katika eneo la msitu wa hifadhi ya Chambogo lakini pia ameelezwa juu ya changamoto za uchomaji mkaa pamoja uchomaji moto mashamba wakati wa kuandaa ambapo moto huo hufika na kuunguza sehemu za misitu ya hifadhi.
Waziri Makamba pia amefika katika eneo la Shule ya msingi Majevu ambapo amejionea makorongo makubwa yaliyosababishwa na kasi ya maji ya mvua kutoka milimani, makorongo yanayotishia uwepo pamoja na usalama wa wanafunzi na walimu wa shule hiyo. Katika hatua za haraka na muda mfupi za kuokoa shule hiyo Waziri Makamba ameahidi kuchangia nusu ya gharama zinazohitajika (Shilingi Milioni 3.5 kati ya 7 zinazohitajika ) huku nusu nyingine (Milioni 3.5) zikitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Same wakati Mikakati ya kupata takibani Shilingi Milioni 60 zinazohitajika kwa hatua za muda mrefu ili kurekebisha sehemu zilizo na maporomoko ikiendelea kufanyiwa kazi.
WhatsApp Image 2017-03-25 at 9.09.49 AM
Baada ya shughuli za ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Same Waziri Makamba pamoja na viongozi wa Wilaya wameshiriki katika majumuisho ya ziara nzima ambapo Waziri makamba ameahidi kufanyia kazi kwa wakati maandiko yote aliyokabidhiwa likiwemo lile la kupendezesha mazingira ya wilaya ya Same lakini pia akiahidi kuweka jitihada za kuisaidia hifadhi ya taifa mkomazi inayohitaji misaada wa kimazingira pamoja kutangazwa zaidi ambapo ameahidi kufikisha ujumbe kwa Waziri mwenye dhamana ya utalii.
Kuhusu usalama wa watu wanaoishi katika eneo la miteremko ya milima Mamba Miamba, ambalo lilipata maafa makubwa ya maporomoko ya ardhi mwaka 2008, na ambayo kwasasa pia yanaonyesha hatari ya kurudia, Waziri Makamba amesema kwa mamlaka aliyopewa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 51 na 52, atalitangaza eneo hilo kuwa eneo nyeti la kimazingira (Environmentally-Sensitive Area). Tangazo hilo la kisheria litalazimisha watu wanaoishi na kufanya shughuli katika eneo hilo kuondoka. Hata hivyo, ametanabaisha kuwa kwa kiasi kikubwa utashi wa wakazi wa eneo hilo kukubali kuondoka katika eneo hilo bila kushurutishwa kwa kufahamu juu ya athari zilizo mbele yao utachangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa hatua hiyo.
WhatsApp Image 2017-03-25 at 9.09.45 AM

JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post