WANANCHI WATAKIWA KUTOA TAARIFA WANAPOONA MABANGO WANAYOTILIA SHAKA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na watu wenye Ulemavu, Janista Mhagama amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona mabango ya matangazo barabarani ambayo wanayatilia shaka.
Waziri Mhagama amesema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumzia uwepo kwa utitiri wa mabango ya ajira yanayoambatana na ahadi za uongo kwenye mishahara.
Amesema kuwa zipo sheria za uwekaji mabango barabarani zinazoongozwa na mamlaka husika zikiwemo Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Jiji na Miji ambazo huweka kanuni na taratibu za mabango hayo.
“Mamlaka husika zina wajibu wa kujiridhisha na kuhakikisha mabango yanayopewa ruhusa kubandika barabarani ni sahihi, yanatangaza ukweli na yanafuata maadili” amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa ikibainika kuwa mabango hayo yanakwenda kinyume na utaratibu waliokubaliana, mamlaka husika wana wajibu wa kuyafuatilia na kuyaondoa mabango hayo ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.
Aidha, Waziri huyo amezungumzia ukaguzi unaofanywa na wizara yake mahali pa kazi ambapo ameeleza kuwa wao hawafuatilii mabango bali huenda kufuatilia kama mwajiri anafuata sheria za kazi ikiwemo mikataba, mishahara, afya na kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi za jamii.
“Tunapokuta malalamiko ya wafanyakazi, au kukuta mwajiri hapeleki michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii, kuna adhabu za hapo kwa hapo kama vile kumtoza mwajiri pesa” amesema Waziri Mhagama.
Akizungumzia suala hilo la uwekaji mabango jijini Dar es salaam, Mstahiki Meya wa jiji la hilo, Isaya Mwita amesema kuwa utaratibu wa kuweka mabango upo kisheria katika halmashauri ila usumbufu mkubwa ni kuwa matangazo madogo madogo ambayo mengi yanawekwa kwenye karatasi za A4 ambayo yanabandikwa kwenye kuta za nyumba, nguzo za umeme na miti bila kufuata utaratibu.
“Kwa sasa tunafanya utaratibu wa kukutana na viongozi wa jiji wakiwemo madiwani, wenyekiti wa halmashauri, wenyekiti wa wilaya na wengine ili kuweka utaratibu wa kudhibiti matangazo hayo, pamoja na kuweka sheria ndogo ndogo, na hivyo kuwapunguzia kero wananchi ambao wanaumizwa na matangazo hayo” amesema Mwitta.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post