BALOZI IDDI AZINDUA MTANDAO WA MABALOZI WA USALAMA BARA BARANI ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akionyesha cheti maalum baada ya kuweka saini yake cha kuthibitisha uzinduzi rasmi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Zanzibar { RSA } hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar, wa kwanza kutoka kulia ni Naibu Kamishna wa Kikosi cha Usalama Bara barani Tanzania DCP Mohamed Mpinga, Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud, Waziri wa Ujenzi Balozi Ali Karume na Kamishna wa Polisi Zanzibar { CP } Hamdan Makame.
Balozi Seif akimkabidhi cheti Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } Bibi Narsa Mohamed kutokana mchango mkubwa uliotolewa na vyombo vya habari vya Shirika hilo wa suala la usalama bara barani.
Balozi Seif akikabidhi cheti maalum kwa Mlezi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani wa Kanda ya Pwani inayounganisha Tanga na Bagamoyo Bwana Nurdin Ali kutokana na mchango mkubwa wa Taasisi hiyo uliosaidia kupunguza ajali za vyombo vya moto Bara barani Tanzania Bara.Picha na – OMPR – ZNZ.

Press Release:-

Matukio ya uvunjifu wa sheria za usalama Bara barani bado yanaendelea kuoteza nguvu kazi ya Taifa wakiwemo Vijana wazee na watoto huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu na wengi kuendelea kuwa mayatima katika maisha yao yote.

Akizindua rasmi Mtandao wa Mabalozi wa wa Usalama Bara barani Zanzibar hapo ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf Balozi Seif Ali Iddi alisema hali hiyo imeendelea pia kuleta hasara kwa Taifa kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu ya Bara bara na vifaa vyengine.

Balozi Seif alisema ajali za bara barani bado zimekuwa ni tishio kwa maisha ya wannchi kutokana na baadhi ya madereva ama kwa makusudi kutotii sheria na taratibu zilizowekwa katika kufuata matumizi sahihi yaliyowekwa bara barani.

Alisema baadhi ya madereva hao wamekuwa na tabia ya kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa kasi bila ya kujali watumiaji wengine mbali mbali kama watoto ambao nao wana haki ya matumizi ya bara bara hizo.

Balozi Seif alionyesha masikitiko yake kutokana na baadhi ya madereva husababisha ajali za kizembe kutokana na ustaarabu wa kisasa ulioingiza wa kuendesha chombo cha moto na huku wanazunguza na simu wakati mataifa mengine Duniani hili wanalihesabu kuwa kosa kubwa bara barani.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi wa kuanzishwa kwa dhana hii ya mabalozi wa usalama Bara barani hapa Zanzibar ni wa busara na kuwa wakati muwafaka ambapo Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada za kukabiliana na ajali za bara barani.

Akizungumzia upande wa gari za Dala dala Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kipo kilio kikubwa cha abiria kutokana na vitendo vya madereva na makonda vya kutowafikisha katika vituo vyao walivyopangiwa.

Alisema mambo hayo yanawasumbua abiria hasa wale wenye mahitaji maalum walemavu ambayo yanakwenda kinyume na sheria za usalama bara barani pamoja na kanuni zake.

Balozi Seif alieleza kwa kutumia utaratibu wa Mabalozi wa Usalama Bara barani wakati umefika wa kukabiliana na matukio kwa kuwapa Taarifa kwa wakati na kuchukuliwa hatua dhidi ya watu wote wanaohusika kuvunja sheria za Nchi.

Jeshi la Polisi usalama Bara barani pamoja na mamlaka nyengine ni vyema likashirikiana kwa karibu na Mabalozi wa Usalama Bara barani kwa kusimamia vyema dhana hii kwa kutumia mikakati tofauti itakayowanasa wapinda sheria za usalama bara barani.

Alisema kupaza sauti, kukemea pamoja na kuchukuwa hatua nyengine kwa wale madereva watukutu kutasaidia kuondoa udumbufu na kero zinazotokana na tabia hiyo mbaya ndani ya Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilinasihi jeshi la Polisi kujenga utamaduni wa kuficha siri kwani ni dhambi kubwa iwapo taarifa za uvunjaji wa sheria bara barani zinazotolewa na Mabalozi kwa jeshi kutolewa kwa wavunja wa sheria hizo.

Balozi Seif alifafanua kwamba huo ni usaliti wa wazi na kamwe hautokubalika kwa sababu ni adui wa maendeleo.

Mapema akitoa Tarifa Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Nd. Justafa Mussa alisema Mtando huo wa Kiraia umeanzishwa kwa lengo la kulisaidia Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama bara barani kupambana na na makosa yanayotokana na bara bara.

Nd. Mustafa alisema dhana hiyo ya Mabalozi wa usalama bara barani inafaa kuungwa mkono ya washirika mbali mbali huku wakielewa kwamba jukumu la kulinda usalama wa raia linamuhusu na kumgusa kikla mwana Jamii.

Alisema wanajumiya hao tayari wameshaanza kutoka mafunzo kwa wanafunzi katika maskuli mbali mbali nchini sambamba na kuwataka wana jamii kutowaonea haya madereva na makonda wajeuri.

Naye Mlezi wa Mabalozi wa usalama Bara barani Msaidizi Kamishna wa Jeshi la Polisi { ACP } Mkadam Khamis Mkadam alisema ajali nyingi zinazotokea Bara barani kutokana na vitendo visivyotii usalama bara barani.

ACP Mkadam alisema kikosi cha usalama Bara bara kimekuwa kikibuni mbinu mbali mbali za kusimamia usalama sambamba na kupunguza ajali kwa kiwqango kikubwa kadri inavyowezekana.

Alisema ajali za bara barani zilizotokeza mwaka 2016 zilifikia mia 604 na kusababisha vifo vya watu 147 wakati mwaka 2017 uliripotiwa ajali mia 517 zilizosababisha vifo vya watu 133 kukiwa na upungufu wa vifa vya watu 14.

Uzinduzi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Zanzibar ulioambatana na michezo ya kuigiza yenye mnasaba na tukio hilo umeshuhudiwa na wanamtandao wa Mabalozi wa usalama Bara barani kutoka Tanzania Bara wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Usalama Bara barani Tanzania ACP Mohamed Mhina.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

19/4/2017.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post