BILIONI 5.4 ZATOLEWA KUKOPESHA VIJANA


MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, James Kajugusi, amesema jumla ya Sh. bilioni 5.4 kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, zimekopeshwa kwa vikundi vilivyosajiliwa katika halmashauri mbalimbali nchini, ambavyo vinajihusisha na shughuli za uzalishaji mali kwa kipindi cha 2013/14.

Akizungumza na Nipashe juzi mjini hapa katika maonyesho ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, Kajugusi alisema kiasi hicho kilitolewa kama mkopo kwa vikundi vya vijana ambao wamejiunga kwa ajili ya uzalishaji mali kuanzia kundi la watu watano na kuendelea wenye umri wa miaka 15 hadi 35.

Alisema katika mikopo hiyo, vijana walitakiwa kujiunga katika vikundi na kusajiliwa kama taasisi zinazohusika pamoja na kujiunga kwenye Saccos za halmashauri ili kupatiwa mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali.

“Vijana wanatakiwa kujiunga katika vikundi vyao ambavyo vimesajiliwa, pia ili waweze kupata mkopo wanatakiwa kuandika andiko la mradi wanaotaka kuufanya kama ufugaji, kilimo, kuanzisha kiwanda au duka la dawa na vinginevyo,” alisema Kajugusi.

Aidha, alisema Idara ya vijana huyachambua maandiko mradi na kupata yanayonyesha uhalisia wa kitu ambacho kinakwenda kufanyika.

“Mkopo huu tunaotoa ni wa miaka miwili, hivyo sasa tunaangalia mradi ambao vijana wameandika kwenda kuutekeleza kama unaweza kufanyika kwa kipindi hicho na kuweza kurejesha mkopo, maana unaweza kuona mtu anataka kufanya mradi ambao unahitaji miaka mingi, hivyo ni vigumu kupata mkopo,” alisema Kajugusi.

Aliongeza, hadi hivi sasa wameshavifikia vikundi 3,500,000 nchini, ambavyo vimeanzishwa kwa malengo tofauti vikiwamo vinavyohitaji mikopo na visivyohitaji.

Hata hivyo, alisema lengo la serikali kutoa mikopo kwa vijana, kuwajengea uwezo wa kutokuwa na woga katika kukopa pamoja kuwawezesha wawe wafanyabiashara wakubwa wa baadae katika taifa.

“Tunatoa mikopo kupitia Saccos za halmashauri mbalimbali nchini, lakini mkakati wa serikali ni kuanzisha benki ya taifa ya vijana ambayo itahudumia hawa vijana waliopo sasa kwenye mfuko wetu ili watakapoondoka kwa utaratibu wa umri, waweze kuitumia benki hiyo,” alisema. 
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post