MABASI YA MIKOANI NA DALADALA DAR ZATANGAZA MGOMO KUPINGA UAMUZI WA SERIKALI

Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (UWADAR) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA) wametangaza mgomo kuanzia siku ya Jumanne kupingana na mabadiliko ya sheria.
Wamiliki wa mabasi na daladala walikutana jana katika mkutano kujadili kwa kina muswada wa sheria ambapo wamelaumu kwa kutokushirikishwa katika maandalizi yake.
Mgomo huo utahusisha mabasi yote yaendayo mikoani na nchi za jirani na yanayosafirisha abiria jijini Dar es Salaam, maarufu kama daladala, kupinga mabadiliko ya sheria ambayo mamlaka ya usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeyafanya.

Muswada huo uliotungwa na SUMATRA unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni wiki ijayo kwa mara ya mwisho na kupitishwa kuwa sheria. Wamiliki wa Mabasi na daladala wamesema muswada huo utakuwa mwiba kwao.
Katika azimio hilo, Mrutu alisema wamiliki wa daladala wa Dar es salaam nao wameungana na wenzao wa TABOA na kuazimia kwa kauli moja kusimamisha huduma ya kusafirisha abiria kuanzia jumanne.
“Si makosa yetu, abiria wajue tumefikia uamuzi huu kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali kutokutujali na wametengeneza muswada wa kutukandamiza… Sheria hii ni mbaya kwetu na wasafiri pia na ikifanikiwa kupita basi watu wengi wataachana biashara hii” alisema Mrutu
Katibu Murutu aliwaomba wabunge wasikubali kuupitisha muswada huo kandamizi ambao alisema iwapo utapitishwa na kuwa sheria utayumbisha biashara ya usafirishaji.
Aliiomba serikali kutoa muda zaidi wa majadiliano na wamiliki wa mabasi na daladala ili kuondoa baadhi ya vifungu vya muswada huo ambavyo ni kandamizi kwa watu wanaofanya biashara hiyo.
Sheria hiyo mpya itaipa mamlaka serikali kutaifisha gari linapofanya makosa, adhabu ambayo ni kubwa sana kulinganisha na thamani ya gari na makosa ambayo yanatajwa kwenye muswada huo.
“Adhabu hii ya kutaifisha gari itaturudhisha nyuma badala ya kutujenga na ikumbukwe kuwa wengi tunaendesha biashara magari kwa mikopo ya benki. jingine tunalotaka ni kwamba kila gari liadhibiwe kwa makosa yaliyofanywa na gari hilo, na gari la kampuni moja lisiadhibiwe kwa kosa linalofanywa na gari jingine la kampuni hiyo, kwa sababu kila gari lina leseni yake tofauti” alisema Mrutu.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es salaam (UWADAR), Kismat Jaffar, aliunga mkono mgomo huo akisema kuwa daladala zote za Dar es Salaam hazitatoa huduma yoyote ya usafiri hadi maelekezo mengine yatakapotolewa.
“Msimamo wa TABOA ndio msimamo wa UWADAR, na sisi kuanzia jumanne tutasitisha huduma za usafirishaji wa abiria hadi hapo matatizo yaliyojadiliwa hapa yatakapopatiwa ufumbuzi, uonevu wanaofanyiwa wenye mabasi ya mikoani ni uonevu huohuo wanaofanyiwa daladala” alisema.
Aidha Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu, aliyetangaza maazimio ya mkutano huo alisema abiria hawapaswi kukata tiketi za mabasi ya Mikoani kuanzia jumatatu na aliomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post