MAKAMU WA RAIS AZINDUA MRADI WA MAJI TABORA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua mradi mkubwa wa maji  Vijijini ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 28 na utahudumia wananchi 42,000 katika wilaya SABA za mkoa wa TABORA.
Uzinduzi wa mradi huo mkubwa na wa aina yake katika mkoa wa Tabora umetekelezwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA) kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika halfa ya Uzinduzi wa Mradi huo katika Kijiji cha Mabama wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa nia ya Serikali ni kuona wananchi wa mkoa wa Tabora wanapata maji safi na salama karibu na maeneo yao kama hatua ya kukomesha tatizo sugu la maji kwa wananchi wa mkoa huo.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata maji safi na salama kwa muda wote hivyo jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha tatizo sugu la maji safi la salama katika baadhi ya maeneo nchini linapata ufumbuzi wa kudumu.
Kuhusu utekelezaji duni wa baadhi ya miradi ya maji nchini, Makamu wa Rais ameonya kuwa Serikali kamwe haitawavumilia watumishi au wakandarasi ambao watatekeleza miradi ya maji ya wananchi kwa kiwango hafifu na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema kuwa Serikali kwa ushirikiano na wahisani mbalimbali wamekuwa wakitoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo hasa miradi ya maji lakini kumekuwepo na tabia ya baadhi wa watendaji wa Serikali kutumia vibaya fedha hizo na kusema kuwa muda wa watendaji hao kuiba fedha hizo umeshaisha na watakaobainika kufanya hivyo watawajibishwa ipasavyo ili kuwa fundisho kwa watu wengine.
Aidha, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amewahimiza wananchi wa mkoa wa Tabora kuutunza ipasavyo mradi huo ili uweze kuwanufaisha kwa muda mrefu wananchi wote wa mkoa huo.
Katika Hotuba yake Makamu wa Rais amewataka Viongozi wa mkoa wa Tabora kupambana ipasavyo na watu wanaoharibu mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji kama hatua ya kuhakikisha maeneo yanahifadhiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo wa Maji Vijijini utahudumia vijiji 31 katika wilaya Saba za mkoa wa Tabora.
Waziri Lwenge ameeleza kuwa mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Tabora kwa sababu mkoa huo ni moja ya mikoa kadhaa hapa inayokabiliwa na ukame mkubwa.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano itaendeleo kuweka mipango na mikakati mizuri inayolenga kuhakikisha wananchi nchini wanapata maji safi na salama ili kuboresha maisha yao na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japan imetekeleza mradi huo maji ambao utanufaisha maelfu ya wananchi wa Tabora kutokana na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Japan.
Balozi Masaharu Yoshida amesema kuwa upatikanaji wa maji ni jambo la msingi na muhimu kwa ajili ya usalama wa binadamu na utasaidia wananchi katika shughuli za uzalishaji badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Balozi huyo pia ameahidi Serikali ya Japan itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania kufutana na matakwa ya Serikali kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha na ustawi wa taifa na wananchi kwa ujumla.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Tabora.
29-Apr-17
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post