MWALIMU AHAMISHA WANAFUNZI NA KUISHI DARASANI

UVINZA: Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kandaga, Wiliadi Kitani amehamia shuleni hapo na kuishi katika moja ya chumba cha madarasa ya kusomea wanafunzi.
Mwalimu Kitani amekataa kuondoa makazi yake katika chumba hicho, hadi hapo ujenzi wa vyumba vya walimu vitakapokamilika. Alipohojiwa kuhusu yeye kuhamia kwenye darasa, alikiri kufanya hivyo lakini hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani sana tukio hilo.
Mwalimu huyo alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na adha ya kutembea umbali mrefu kutoka na kwenda shule kutokana na kupanga chumba mtaa wa mbali. Ili kupata nafasi ya kuishi, Mwalimu Kitani aliwahamishia wanafunzi wa darasa la kwanza katika chumba cha darasa la tatu na wale wa darasa la tatu wakahamishiwa chumba cha darasa la saba.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kandaga, Steven Ntazi alisema kuwa uamuzi wa mwalimu huyo kuhamia kwenye chumba cha darasa ni kinyume na agizo la Kamati ya Shule ya Machi 20, lililowakatalia walimu watatu kuhamia kwenye madarasa wakisubiri vyumba vya walimu vikamilike.
“Jambo hili limetusikitisha kwa sababu limefanyika kama shinikizo la kutulazimisha kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu zilizofikia kwenye lenta, licha ya ukweli kuwa hakuna bajeti hiyo mwaka huu,” alisema Ntazi.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Alberto Edward alisema juhudi za kumtaka mwalimu huyo kuhama kwenye chumba cha darasa na kupisha wanafunzi zimegonga mwamba licha ya kubembelezwa.
Mratibu wa Elimu Kata ya Kandaga, Emmanuel Mbanda alisema, baada ya kupokea malalamiko ya walimu kukaa mbali na shule kiasi cha kutembea umbali mrefu aliwasilisha suala hilo mbele ya kamati ya shule iliyotafuta nyumba za kupanga eneo la karibu na shule, lakini Mwalimu Kitani alikataa.
“Nimefikisha suala hili ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kwa hatua zaidi”  alisema Mbanda.
Chanzo: Mwananchi
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post