RAIS MAGUFULI AWAPIGA KIJEMBE WANAOMKOSOA WAKATI AKIZUNDUA UJENZI WA RELI YA KISASA

Rais Dkt Magufuli amewakosoa Watanzania ambao wao kila kukicha ni kupiga kelele na kukosoa uongozi wake badala ya kujishughulisha katika shughuli za maendeleo zitakazoisaidia nchi kujikwamua kutoka kwenye umasikini.
Aidha, amesema yeye ni dereva makini wa lori na anafahamu anapotaka kulifikisha lori lake, hivyo hasumbuliwi na kelele za abiria ambao hata hawajui wanapotakiwa kufika.
Mimi ni dereva makini, kenye lori langu nimepakia watu wanaoimba, wengine wanaongea, wengine wamelala chini, baadhi wanaangalia walipotokea na wengine pembeni, lakini kwa dereva makini hawaangalia abiria wake wanasema nini au wanaangalia wapi, anachotakiwa ni kuangalia mbele ili afikishe lori salama, alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa itakayoanzia Dar es Salaam hadi mkoani Morogoro. Hafla hiyo imefanyika leo Pugu jijini Dar es Salaam.
Akihutumia wananchi na wageni waliojitokeza  katika hafla hiyo, Rais Dkt Magufuli amesema ujenzi huo utakuwa ni wa kihistoria kwani umeanza kwa kufadhiliwa na fedha za ndani tofauti na miradi mingi inayoendelea nchini.
Akitaja faida za ujenzi wa reli hiyo ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kwenda kwa spidi wa 160km/h, Rais Magufuli alisema kwanza itasaidia katika kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo. Treni hizo zitakapoanza kazi katika awamu hii ya kwanza zitakuwa na uwezo wa kubeba tani 35, ambapo njia hiyo itakuwa ni ya usalama, nafuu na haraka zaidi.
Mbali na hilo, itasaidia kuimarisha barabara kwani kwa sasa barabara nyingi zinaharibika kutokana na malori mengine kusafirishia mizigo mizito, lakini reli hiyo ambayo pia itatumika kusafirisha mizigo itapunguza idadi ya malori yanayosafirisa mizigo barabarani. Pia ujenzi huo utatoa ajira kwa wananchi ambapo wakati wa ujenzi ajira takribani laki 6 zinatarajiwa kutolewa na ikikamlika ajira takribani milioni 1 zitatolewa katika sekta mbalimbali.
Aidha, Rais Magufuli amesema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa utasaidia kuinua sekta nyingine kama vile sekta ya viwanda, sekta ya kilimo kwa kusafirisha bidhaa kwenda viwandani lakini pia kwenda sokoni.
Wakandarasi wamesema ujenzi wa reli hiyo utachukua miezi 30, lakini Rais Magufuli amewataka kuhakikisha kuwa unakamilika kabla ya muda huo kwani watanzania wanataka kuanza kuitumia mapema. TZS trillioni 2.8 zitatumika katika ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo pia mwakilishi wa Benki ya Dunia, Mama Janeth Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa kamati za bunge, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na ujumbe wake pamoja na makapuni mbalimbali yatakayohusika na ujenzi wa reli ya kisasa.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post