SABABU ZINAZOIFANYA MIGUU YAKO KUPASUKA NA NAMNA YA KUITIBU

Kuwa na miguu au visigino vilivyopasuka (gaga au machacha) ni moja ya sababu inayoweza kuonyesha kuwa katika mwili kuna upungufu wa virutubisho kadhaa, vitamini au madini.
Japo wengi wetu tumekuwa na mitazamo kwamba, visigino kupasuka ni ishara ya mtu kutojali usafi wa miguu. Yawezekana ikawa ndiyo sababu lakini hiyo siyo sababu pekee inayochangia kupasuka kwa visigino vya miguu.
Kwa kawaida, ngozi zetu huwa zina unyevunyevu ambao huiwezesha ngozi ivutike au kutanuka pamoja na kusinyaa bila ya kutokea madhara yoyote kama vile kuchanika. Pamoja na ngozi kugawanyika katika sehemu tatu ( sehemu ya nje – Epidermis, sehemu ya kati – Dermis na sehemu ya ndani –  Endodermis), ni sehemu ya nje, epidermis, ambayo ipo karibu na unaweza kuigusa au inaweza kuathirika na ukaiona kirahisi. Hii ni kwa sababu inagusana moja kwa moja na mazingira yetu.
Kupasuka kwa miguu (magaga) hutokea katika ngozi ya nje na hii hutokana na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu apasuke visigino ni pamoja na:
Ngozi kuwa kavu sana
Hii ni sehemu ya nje ya ngozi ambayo inawezekana mtu kwa asili yake akawa na ngozi kavu na hivyo kuifanya ishindwe kustahimili kutanuka au kusinyaa na hivyo kupelekea ipasuke.
Kuiweka miguu katika maji kwa muda mrefu na baadae kutoipaka mafuta ya kulainisha ngozi, hii husababisha ile asili ya ngozi pamoja na mafuta katika ngozi yapotee na kuiacha ngozi ikiwa kavu sana.
Kuwa na uzito mkubwa
Mtu unapokuwa na uzito mkubwa husababisha presha kubwa iwe katika miguu unapokanyaga na endapo ngozi yako haitokuwa na uimara wa kutosha itasababisha visigino vipasuke.
Upungufu wa virutubisho mwilini
Mfano madini ya Zinc, vitamini E pamoja na mafuta, omega 3 ambavyo huifanya ngozi yako kuwa na unyevuunyevu unaoiwezesha kutanuka na kusinyaa pasipo madhara yoyote. Ukosefu wa virutubisho hivyo husababisha ngozi kupoteza uimara wake na kuifanya ipasuke kirahisi.
Kuvaa viatu ambavyo nyuma vipo wazi, back-opened shoes or sandals
Viatu vyenye uwazi nyumahuulazimisha mguu au upande wa kisigino katika mguu utanuke zaidi na hivyo kuuweka mguu hatarini kupasuka.
Baadhi ya magonjwa kama vile kisukari na magonjwa ya homoni (thyroid diseases).
Magonjwa haya huingiliana na mfumo wa mwili na pia huathiri afya ya ngozi.
Umri mkubwa
Kwa kawaida mtu anapokuwa na umri mkubwa sana, hata utendaji kazi wa mifumo mbalimbali katika mwili wake hupungua kiufanisi, hivyo hata kinga ya mwili pamoja na afya ya ngozi pia hupungua.
Mtu kutozingatia usafi wa miguu yake kwa kiwango kinacho stahili
Moja ya madhara yanayoweza kutokea kwa mtu kupasuka visigino ni kupata maambukizi ya magonjwa, infection. Hii ni endapo miguu itachanika kiwango cha kufikia ngazi ya kati ya ngozi, dermis, na kupelekea damu zianze kutoka sambamba na maumivu makali. Kupitia hiyo mipasuko mtu anaweza kupata maambukizi ya magonjwa.
Mambo yanayoweza kufanyika ili kuzuia au kutibu tatizo la kupasuka visigino ni pamoja na:
  • Kuzingatia ipasavyo usafi wa miguu na mwili kwa ujumla.
  • Kuepuka kutembea katika sehemu zisizo sawa, rough surfaces, bila kuvaa viatu, hii itaepusha miguu kuchanika.
  • Kwa miguu iliyopasuka tayari, ifanyie usafi miguu yako na kisha tumia mafuta ya mzaituni kupaka katika mipasuko, vaa soksi na viatu vya kufunika ili miguu iendelee kuwa na unyevu, wakati wa usiku pia fanya hivyo huku ukilala miguu imevalishwa soksi baada ya kuipaka mafuta.
  • Ambatanisha vitu vifuatavyo katika mlo wako, vyakula venye madini ya calcium, zinc na iron. ( Maziwa, mboga za majani, mafuta ya mimea, nyama, maharage pamoja na samaki wa maji baridi).
  • Kuepuka kusimama kwa muda mrefu pamoja na kutoiweka miguu katika maji kwa kipindi kirefu. Kama unafanya zoezi la ufuaji, jitahidi kuilinda miguu yako isiwe katika sabuni kwani sabuni nyingi za kufulia huvunjavunja mafuta yaliyo katika ngozi na kuiacha ikiwa kavu sana na kuifanya ipasuke.
  • Jitahidi walau mara moja kwa wiki, kuiweka miguu yako katika maji ya vuguvugu, hii husaidia kuongeza mzunguko wa damu katika miguu na hivyo kuendelea kuimarisha afya ya ngozi yako.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post