WASIFU WA MGOMBEA PEKEE WA CUF UBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI

HISTORIA YAKE
Twaha Taslima ni wakili wa kujitegemea na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Tanzania na ni kiongozi mwandamizi wa Chama Cha Wananchi CUF. Alizaliwa tarehe 20 Aprili 1953 katika kijiji cha Ibwera, Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mkoa wa Kagera.
Taslima alianza elimu yake katika Shule ya Msingi Kwatwe na baadaye kuhamia Shule ya Msingi Myamahoro – Bukoba Vijijini baadaye alikwenda katika Shule ya Sekondari ya Grewal na kuhitimu kidato cha nne kabla ya kusoma Shule ya Sekondari Bukoba na kuhitimu kidato cha sita.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, Taslima aliajiriwa moja kwa moja na Idara ya Mahakama kama “Karani wa Mahakama na Mfasiri”. Aliifanya kazi hii mahakama Kuu ya Tanzania mpaka ilipoanzishwa mahakama ya Rufaa.
Taslima alijiunga na Taasisi ya Regent nchini Uingereza kwa masomo ya juu ya kiingereza na kutunukiwa Stashahada ya Lugha ya Kiingereza mwaka 1974. Alirejea nchini Tanzania na kuanza kazi za ujenzi wa taifa kwa miaka 11.
Kuanzia mwaka 1979 – 1993 amefanya kazi na Shirika la Utalii Tanzania akiwa kama Ofisa Sheria na akapandishwa cheo na kuwa Katibu Msaidizi wa Shirika (Shirika hilo lilivunjwa rasmi mwaka 1993).
Wakati anafanya kazi Shirika la Utalii Tanzania, pia alijiunga na Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo ya Mzumbe (IDM), siku hizi ikiitwa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambako alisomea sheria na kuhitimu stashahada ya Sheria mwaka 1988.
Kutokana na ufaulu mzuri, Taslima alipata udahili wa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ambako alipata shahada ya Sheria (L LB) mwaka 1993.
Baada ya kuhitimu shahada yake ya Sheria, Taslima alifanya kazi kama Katibu wa kitengo cha Sheria katika Shirika la Kukuza Huduma za Viwanda (Industrial Promotion Service) lililoko jijini Dar Es Salaam, kati ya mwaka 1993 na 1994.
Baadaye mwaka 1995 hadi 1998, Taslima alifanya kazi kama katibu wa Idara ya Sheria na Ofisa Msimamizi wa Rasilimali watu katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar Es Salaam na kipindi hichohicho alikuwa mhadhiri wa muda mfupi katika masomo ya Sheria za Biashara katika Chuo hicho.
Taslima alisajiliwa rasmi kuwa Wakili wa kujitegemea mwaka 1996 na alianzisha kampuni ya uwakili ijulikanayo kama Taslima Law Chambers ambayo inafanya kazi jijini Dar Es Saalam ikiwa na tawi moja kanda ya ziwa. Kampuni hii imefanikiwa kutoa ajira kwa mawakili 8 akiwemo yeye mwenyewe huku ikiwa na wafanyakazi wengine zaidi ya watano.
Kwa zaidi ya miaka 20, Taslima amekuwa wakili wa Chama Cha Wananchi CUF akisimamia kesi mbalimbali za chama hicho upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, lakini pia akijihusisha katika kusimamia kesi za vyama mbalimbali vya siasa ili kuendelea kujenga msingi wa upatikanaji wa haki kwa watu wanaotafuta mabadiliko katika nchi.
Kisiasa, Taslima amekuwa mwanachama mtiiifu wa Chama cha Wananchi CUF tokea mwaka 2000 hadi sasa na zaidi ya yote katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 amekuwa akichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, na tena mwaka 2009 akachaguliwa katika chombo hicho na mwaka 2014 akachaguliwa kwa mara ya tatu. Taslima amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF tangu Septemba 2015 hadi Agosti 2016.
Taslima ameoa na ana watoto.
MBIO ZA UBUNGE
Taslima ni mwanasiasa mzoefu kwa upande wa Ubunge. Alishiriki uchaguzi wa kwanza wa Ubunge mwaka 2002 katika jimbo la Bukoba Vijijini baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Sebastian Kinyondo (CCM) aliyefariki mwezi Agosti mwaka 2001 akiwa jijini Nairobi alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura.
Katika Uchaguzi huo mdogo, Taslima aligombea kwa tiketi ya CUF na kuchukua nafasi ya pili nyuma ya mshindi wa jumla, Naziri Karamagi wa CCM.
Mwaka 2005 Taslima aligombea ubunge katika jimbo la Bukoba Vijijini kwa tiketi ya CUF akishindana na Nazir Karamagi wa CCM kwa mara ya pili. Taslima aliibukia katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 35 ya kura zote dhidi ya asilimia 62 za Karamagi.
Taslima aligombea tena ubunge Bukoba Vijijini kwa mara ya tatu mwaka 2010, alitokea wa tatu kwa asilimia 7 ya kura zote.
Mwaka 2012 alijitosa katika kinyang’anyiro cha Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika kundi la vyama vya upinzani. Alipigiwa kura nyingi na kushinda nafasi hiyo na hadi nifanyapo uchambuzi huu, yeye ni mbunge wa bunge hilo hadi kipindi chake kikamilike mwaka 2017.
HITIMISHO
Taslima ni Wakili ambaye amekuwa na mchango mkubwa sana katika Chama cha Wananchi CUF, siasa za Tanzania na ametoa mchango mkubwa kwenye bunge la EALA miaka mitano iliyopita. Anastahili kuchaguliwa tena kwa hali na mali.
Uchambuzi huu umenukuliwa kutoka wenye chapisho la Gazeti la Mwananchi la Mwezi Mei 2015 lililohusu watu wenye sifa za kugombea Urais wa Tanzania. Mchambuzi ni Julius Mtatiro, Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB : juliusmtatiro@yahoo.com, +255787536759.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post