WATENDAJI SERIKALINI WATAKIWA KUTOJIINGIZA KWENYE MAGENDO YA KARAFUU

 NA HAJI NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk: Ali Mohamed Shein, amewataka watendaji wa serikali kisiwani Pemba, kutojiingiza kwenye biashara haramu ya magendo ya karafuu, na badala yake wawe wasimamizi wakuu wa kutotoroshwa kwa zao hilo la taifa.

Alisema msimu mwengine wa uchumaji wa zao la karafuu unakuja, hivyo kila mmoja awe mlinzi wa biashara hiyo kwa mwenzake, na wasiwe sehemu ya kurahisisha uvuushaji wa karafuu, kwa njia ya magendo na hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa atakaebainika.

Dk Shein alieleza hayo, ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi Chakechake, alipokuwa akizungumza na watendaji wakuu wa serikali kisiwani Pemba ikiwe ni sehemu ya ziara ya siku tano kisiwani humo.

Alisema serikali kwa msimu ujao,imejipanga vyema kuzuia magendo ya karafuu, hivyo lazima kila mmoja atekeleze wajibu wake wa kuzuia biashara hiyo ya magendo hayo.

Alieleza kuwa, msimu uliopita wapo baadhi ya watendaji walikuwa na sura ya kuhusika na magendo ya karafuu, na kisha kuvutana wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo halipendezi.

“Msimu wa karafuu unakuja, sasa nyinyi watendaji wa serikali lazima mshirikiane kuhakikisha hakuna mtendaji anaeshiriki biashara hii haramu ya magendo ya karafuu’’,alifafanua.

Kuhusu karafuu za mikoa ya Morogoro na Tanga Tanania bara zinazoingia kisiwani Pemba kwa njia ya magendo, alisema bado serikali inaendelea na msimamo wake, wa kutozinunua karafuu hizo, kwa vile zinaweza kuharibu ubora wa karafuu za Zanzibar.

Alisema bado karafuu ya Zanzibar inahadhi kwenye soko la dunia na hata bidhaa zake, hivyo iwapo watazikubali karafuu hizo kununuliwa na ZSTC ubora utapotea.

“Nilipokea maombi kwa wenzangu juu ya kuzikubali karafuu za nje ya Zanzibar, lakini tunaendela kuzikataa, maana hazina ubora kama za kwetu’’,alifafanua.

Akizungumzia uhaba wa madaktari kwenye hospitali na vituo vya afya Dk Shein alisema, hata hao wachache waliopo kazini, wamekuwa wazito kutekeleza wajibu wao jambo ambalo halileti taswira nzuri kwenye matibabu.

Alisema utendaji wa kazi wa madaktari umeshuka kwa kiwango kikubwa, na kisha kujificha kwenye kiza cha uhaba wa madaktari na kukosekana kwa usimamizi imara.

“Kweli serikali na wizara husika inaelewa kuwa kuna uhaba wa madaktari Unguja na Pemba, lakini hao waliopo wamekosa uzalendo na usimamizi haupo wa kutosha’’,alieleza.

Kuhusu maneo kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imegomewa na mashirika mbali mbali ya fedha, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Ali Mohamed Shein, amesema hakuna nchi wala shirika lolote la fedha duniani, lililoigomea Zanzibar katika kuwasaidia miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alisema hakuna, benki yoyote ya kimatifa ilioiacha mkono Zanzibar na wanaendelea kupokea misaada mbali mbali ya baadhi ya nchi kadhaa na mashirika mengine huingia Zanzibar kimnya imnya.

Alisema sio sahihi juu ya maneno yanayosemwa kuwa, wafadhili mbali mbali wa kimataifa wameigomea serikali ya Zanzibar kutoa ufadhli wao, jambo ambalo sio sahihi hata kidogo.

Alisema bado Zanzibar inaomarafiki wa kweli, kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya nchi husika na wakati mwengine hata kukopeshwa fedha kutoka nchi za nje

“Bado marafiki wetu kama ADB, IMF, Seikali ya China na nyengine wanaendelea kutusaidia kwa kasi kubwa na hata katika bajeti zilizopita walitusaidia”,alifafanua.

Kuhusu utendaji wa kazi, amewataka watendaji hao kuziacha ofisi zao na kwenda kwa wananchi moja kwa moja, ili kutambua kwa kina matatizo yanayowakabili.

“Nampongeza sana Mkuu wa wilaya ya Chakechake, amekuwa mfano mzuri anakwenda kwa wananchi moja kwa moja, kujua nini kinachowasibu na wengine waige mfano huo’’,alifafanua.

Katika hatua nyengine rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, amewataka watendaji hao kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari ili kutangaaza kazi wanazozifanya kwa wananchi.

“Waelezeni wananchi mlichokifanya kwa kuvitumia vyombo vya habari, maana ndio vinavyowaunganisha nyinyi na wananchi, hawa waandishi msiwakimbie’’,alieleza.

Baadhi ya watendaji hao wa serikali kisiwani Pemba, wamempongeza rasi huyo wa Zanzibar kwa kufikia mwaka mmoja wa utawala wake wa kipindi cha awamu ya pili na kuahidi kuendelea kushirikiana nae.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Omra Khamis Othaman kwa niaba ya Mkuu wa mkoa mwenzake wa kusini, alisema wamekuwa na ushirikiano mzuri na maafisa wadhamini, jambo linalosababisha kurahisisha utendaji wao wa kazi.

Nae Mkuu wa wilaya ya Chakechake Salama Mbarouk Khatib alisema, kikwazo kikubwa kilichomo ndani ya wilaya yake kwa sasa, ni kuongezeka kwa migogoro ya ardhi pamoja na uhaba wa madaktari kwa hospitali zilizomo ndani ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mdhamini Shirika la taifa la biashara la ZSTC Pemba, Abdalla Ali Ussi tatizo lililop kwa wakulima wa zao la karafuu kisiwani humo ni kuibuka kwa wizi wa karafuu.

“Wakulima wamekuwa wakilazimika kulala kwenye mashamba yao, maana karafuu zikianza kupea huibiwa, sasa hili ni tatizo maana na sisi ZSTC soko la dunia litashuka hadhi’’,alifafanua.

Dk Shein yupo kisiwani Pemba kwa zaiara ya siku tano, ambapo pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kutembelea ukarabati wa barabara ya Madenjani- Mzambarau takao, ujenzi wa chuo cha amali Daya Mtambwe, kuzungumza na waalimu pamoja na kamati za chama. Habari kwa hisani ya ZanziNews
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post