HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUPIGA MARUFUKU WANANCHI KUJENGA KATIKA MAENEO YASIYOPIMWA

KATIKA kukabiliana na ujenzi holela nchini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameziagiza halmashauri zote nchini kupiga marufuku wananchi kujenga katika maeneo yasiyopimwa.
Pamoja na hayo, Waziri huyo amewahakikishia Watanzania kuwa wizara yake itaendelea kutekeleza mwongozo wa Rais John Magufuli wa kutenda haki kwa Watanzania wote bila ya kuangalia itikadi ya vyama.
Aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akijumuisha majadiliano ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Alizitaka halmashauri hizo zisiruhusu watu kujenga katika maeneo yasiyopimwa kwa kuwa tayari serikali imetengeneza mazingira ya kuwezesha wananchi kuweza kumudu kumiliki maeneo yaliyopimwa.
“Kwa sababu kilio cha wananchi cha kupunguza tozo tumefanya na gharama za upimaji zitapungua sana, hivyo hakuna sababu ya mtu kuendelea kuvamiavamia pamoja na kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Lukuvi alisema kutokana na kilio cha uhaba wa watumishi wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, wizara hiyo inatarajia kufanya mabadiliko ya watumishi kwa kuangalia maeneo yenye watumishi wengi na kuwapeleka kwenye maeneo yasiyo na watu kabisa.
Alisema wizara hiyo itashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kulitatua tatizo hilo. Alisema katika zungukazunguka yake amegundua kuwa kuna wilaya zimependelewa kwa kupangiwa watumishi wengi na kutolea mfano wilaya za Ilemela na Nyamagana katika mkoa wa Mwanza ambazo zina watumishi wasioupungua 100 huku wilaya zingine zikiwa hazina hata mtumishi mmoja wa ardhi.
Alisema watumishi hao na wengine waliopo watasambazwa katika maeneo mbalimbali ili kuwa na uwiano wa watumishi. “Kabla ya kuajiri wafanyakazi wapya tutaangalia uwiano wa jinsi walivyopangwa ili wawekwe vizuri na kazi za dharura ziweze kufanyika.”
Aidha, alisema wizara hiyo pia itafuatilia vibali vya kuajiri kwa Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora, chini ya Waziri wake, Angela Kairuki na kupanga upya watumishi wa wizara hiyo ya ardhi.
Kuhusu kusuasua kwa kupimwa kwa viwanja nchini kutokana na upungufu wa vifaa, Lukuvi alisema tayari wizara hiyo imeagiza vifaa vipya vya upimaji wa viwanja ambavyo ni vya kisasa.
“Tumeishaagiza vifaa na tumetangaza katika magazeti tutavisambaza tena kwa Teknolojia mpya kwa sababu sasa tunatumia Satelite na vifaa vya mapokezi ya Satelite tumewaonesha, sasa tutakuwa na vifaa vipya na tutawaelekeza maofisa wenu kwani hawajui jinsi ya kuvitumia,” alisema.
Alisema vifaa hivyo vina uwezo mkubwa wa upimaji ambapo wilaya moja inaweza kupimwa kwa muda wa siku tano tu, kwani kifaa kimoja kina uwezo wa kupima kilometa 30 na hutumiwa na watu wawili au watatu tu,” alifafanua.
Alisema vifaa hivyo vitasambazwa katika kila wilaya ili kuhakikisha utaratibu huo wa upimaji viwanja unafanyika kwa haraka na kusisitiza kuwa tayari wameanza kuteua watendaji katika kanda ili waweze kufanya kazi hiyo ya upimaji na maeneo yatakayopimwa kwa haraka ni Dar es Salaam na Dodoma.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, alisema wizara hiyo ina mpango wa kuajiri watumishi 291 kati yao, 91 watapelekwa kwenye mabaraza ya ardhi ili kuboresha eneo la usuluhishi wa matatizo ya ardhi.
Alisema mipango kabambe 26 inaendelea kutengenezwa ili kuboresha eneo la mipango miji nchini. Kuhusu wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kuingilia mabaraza ya ardhi, waziri huyo alifafanua kuwa mabaraza hayo yana uhuru kamili hivyo hayahitaji kuingiliwa na mtu yeyote.
Bajeti ya wizara hiyo, ilipitishwa bila kupingwa bungeni jana, ambapo iliomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 70.7, kati ya fedha hizo Sh bilioni 45 matumizi ya kawaida na Sh bilioni 25 matumizi ya maendeleo.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

SHARE THIS

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post