LOWASSA AMSHANGAA RAIS MAGUFULI

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameshangazwa na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kuweka zuio la shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara ilihali yeye akiendelea kufanya mikutano hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi, tena kwa kutumia rasilimali za taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mikocheni, jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema wakati Rais Magufuli akizuia wanasiasa hasa wa upinzani kuendesha shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara, yeye binafsi amekuwa akijinufaisha na zuio hilo kwa kufanya mikutano hiyo tena akiifanikisha kwa kutumia rasilimali za taifa.
“Namshangaa amekuwa akitumia vyombo vya serikali …. hata usafiri kufika katika maeneo ya mikutano na kuendesha mikutano hiyo ya kisiasa lakini amekuwa akituzuia sisi wengine tunaotumia rasilimali binafsi na za vyama vyetu kuendesha shughuli hizo hizo za kisiasa. Hiyo ni demokrasia ya wapi?” alihoji Lowassa wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyehudhuria mkutano huo uliofanyika Mei 13, 2017, mchana.
Kauli hiyo ya Lowassa ni majibu kwa agizo la Rais Magufuli alilolitoa Juni mwaka jana, akipiga marufuku vyama vya siasa kufanya shughuli za siasa mpaka baada ya miaka mitano. Katika kufafanua agizo lake hilo, Magufuli alidai kuwa lengo ni kuwapa nafasi wananchi wafanye kazi za uzalishaji.
Magufuli alitoa kauli hiyo Ikulu Dar es Salaam, Juni 23, 2016, baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva.
“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayetekeleza. Kila nchi hata zile zilizobobea kwenye demokrasia unapokwisha uchaguzi unakuwa ni wakati wa kazi. Haiwezekani mkawa kila siku ni siasa watu watalima saa ngapi?  Kila siku ni siasa, ni vema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na watatupima kwenye hilo,” alisema
Katika hatua nyingine, akijibu swali kuhusu kuzuiwa kwa kongamano la demokrasia na siasa za ushindani lililopangwa kufanyika katika ukumbi wa Anatouglou jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wake, Lowassa alijibu kwa utani akiashiria ni uamuzi uliotokana na uongozi usiokuwa na viwango sahihi vya busara na elimu, akisema; “…ni uongozi wa kibashite”. Bashite ni jina ambalo Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amekuwa akilihusisha na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ikidaiwa kwamba mkuu huyo alibadili jina kutoka Daudi Albert Bashite hadi Paul Christian Makonda ili kufanikisha ndoto zake za kielimu, bado madai hayo hayajapata kujibiwa na Makonda mwenyewe licha ya kudumu kwa miezi kadhaa sasa.
Lowassa alipaswa kuongoza kongamano hilo la demekorasia ambalo lilipaswa kushirikisha watoa mada mbalimbali ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, mwanahabari nguli nchini, Jenerali Ulimwengu na wanasiasa wengine kutoka chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), ikitarajiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole angeshiriki. Hata hivyo, kongamano hilo lilishindikana baada ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, ghafla, kudai ukumbi husika utatumika kwa ajili ya shughuli za serikali, kinyume cha kibali cha awali cha kuruhusu kongamano husika kufanyika.
Mbali na hayo, Lowassa pia alielezea kushangazwa kwake na hatua ya Rais Magufuli kutohudhuria msiba wa wanafunzi 32 wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha, akisisitiza kwamba ulikuwa msiba mzito wa kitaifa uliostahili kuhudhuriwa na mkuu huyo wa nchi, na kwa hiyo, wananchi wa Arusha wamesikitishwa na kitendo chake hicho.
Wanafunzi hao walifariki katika ajali ya gari eneo la Rhotia, mkoani Arusha baada ya basi walilokuwa wakisaifiria kutumbukia katika korongo lililopo mlima Rhotia,Karatu, kilomita takriban 25 kutoka katika lango (geti) la Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na takriban kilomita 150 kutoka mji wa Arusha.
“Kwa niaba ya wananchi wa Arusha, nasema tumesikitishwa sana na kitendo cha Rais Magufuli kushindwa kuhudhuria msiba ule wa kitaifa,” alisema Lowassa.
Aidha, Lowassa aliishauri serikali kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha mfululizo kwa wiki kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Miongoni mwa maeneo ambayo athari za mvua hizo zimekuwa kubwa ni pamoja na Lushoto, mkoani Tanga, ambako baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wamepoteza makazi yao.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post