LOWASSA AWALILIA WENYE VYETI FEKI

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa jana  alizungumzia sakata la watumishi 9,932 wa umma wenye vyeti feki ambao wametakiwa kuondoka kazini mara moja na kunyimwa mafao yao kwamba ubinadamu haujatumika katika kuwafukuza kwa wakati mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lowassa alisema kuwa wapo walioitumikia serikali kwa muda mrefu, na kama wakifukuzwa tu pasipo kuliwa mafao yao basi itakuwa si ubinadamu.
“Siwatetei lakini wananyimwa mishahara na mafao, wapo waliotumikia kwa miaka 30 au 20. Nakubali kama wamekosea tena sana… Lakini mafao ya mtu, sasa hawa wataenda wapi, mtu ana familia. Hata kama walifanya makosa, moyo wa huruma ulihitajika. Sawa amekosa mimi sitetei kosa lao, bali natetea ubinadamu wake, hivi ingenifika mimi leo ungejisikiaje,” alisema.
Alisema anatoa pongezi kwa mambo mengi mazuri yaliyofanywa, lakini katika sakata la vyeti feki, wahusika inabidi wafikiriwe na kwamba shule nyingi zitakosa walimu sanjari na kukosekana kwa wakunga.
Alisisitiza kuwa pamoja na nia njema ya Serikali, lakini watumishi hao inabidi waangaliwe kwa sura ya huruma.
Aidha alizungumzia kuhusu kuzuiliwa kwa kongamano lililokuwa limeandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililopanga kuwashirikisha viongozi wa vyama vingine ikiwamo Chama cha Mapinduzi na lililolenga kujadili hali ya demokrasia nchini.
Akizungumzia zuio hilo, Lowassa alisema amesikitishwa na kitendo hicho alichodai kimefanywa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tunalaani kitendo hiki kwa lugha inayowezekana, hatua hii ni ya kuminya demokrasia. Nia yetu ilikuwa njema ya kuzungumzia demokrasia. Waandaaji wa kongamano hili waliweka picha yangu na ya Kinana (Abdulrahman Kinana­Katibu Mkuu wa CCM) tukionekana tumepeana vichwa lakini tuki­ smile (tukitabasamu) jambo ambalo ni very important (muhimu),” alisema Lowassa.
Lowassa alisema Tanzania ni moja na watu ni walewale hivyo hakuna tofauti kwa watu wa CCM na Chadema na kwamba kila mmoja kuwa na maoni tofauti hakuna dhambi.
Hata hivyo, Lowassa aliwataka CCM kutambua kuwa ipo siku nchi ya Tanzania itatawaliwa na watu (chama) wengine na siyo wao.
“Kama watashindwa kuondoka wakati wetu, wataondoka wakati wa wajukuu wetu,” alisema.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post