ORODHA YA MAWAZIRI WALIOONGOZA WIZARA YA NISHATI NA KASHFA ZILIZOWAONDOA

Ni dhahiri kuwa kuteuliwa kuwa waziri na kufanikiwa kuiongoza wizara kwa mafanikio mazuri, si jambo rahisi kwa sababu kila wizara ina changamoto zake za kuhakikisha unafanikiwa. Lakini kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini, hii inahitaji pengine malaika kuweza kufikia malengo ambayo taifa inayataka.
Kwa miaka ya hivi karibuni imeonekana kuwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ni kama kutupwa katika ya Simba wenye njaa, hivyo itategemea utashi wako wa kupambana na kuweza kutoka salama.
Hii imetokana na mawaziri wengi walioshika wizara hiyo kuondolewa kabla ya muda wao kufikia mwisho tena wakiondolewa baada ya kukumbwa na kashfa mbalimbali.
Ukiangalia nyuma tangu awamu ya mwisho ya uongozi wa Rais wa awamu ya tatu, Mzee Benjamin Mkapa utaona kuwa ni waziri mmoja tu aliyeondoka katika wizara hiyo bila kuwa na kashfa. Mbali na Waziri George Simbachawene, mawaziri wengine ambao wameiongoza wizara hiyo hawakutoka salama.
Pengine ugumu wa kuongoza wizara hiyo unatokana na ukweli kuwa inahusika na rasilimali zenye fedha sana duniani na hivyo vishawishi vinakuwa vingi kiasi kwamba unashindwa kuvikwepa. Hapa chini ni orodha ya mawaziri walioiongoza wizara hiyo tangu miaka miwili ya mwisho ya Rais Mkapa pamoja na kashfa mbalimbali zilizowaondoa madarakani.
Katika awamu ya mwisho ya uongozi wa Mzee Mkapa, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa ni Daniel Aggrey  Ndhira Yona aliyeongoza wizara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo aliishia kufungwa jela. Yona alishtakiwa pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Basil Pesambili Mramba kuhusu makosa mbalimbali.
Miongoni mwa makosa waliyoshtakiwa nayo ni, kwanza, kutoa zabuni  na  kuingia  mkataba  na  kampuni  ya MS  ALEX  STUWART kufanya  kazi  ya ukaguzi  wa  madini  yanayozalishwa  kinyume  na  sheria. Pili, kuongezea  mkataba  wa  ukaguzi  wa  madini  kampuni  hiyohiyo ya  Alex  kwa  miaka  miwili zaidi  kuanzia  tarehe  14 Juni 2005  hadi  tarehe  23 Juni 2007 bila kufuata utaratibu. Tatu, Machi  na  Mei 2005  mawaziri  hao  wawili kwa  nia  mbaya  walizuia  taratibu  halali  za  kimkataba  zilizopendekezwa  na  mwanasheria  mkuu  pamoja  kamati  ya  serikali  ( Government  Negotiating  Team GNT)  iliyokuwa  imeteuliwa  kwa  kazi  hiyo na nne, mwaka  2003  na 2007 kwa  nafasi  zao  waliisababishia  serikali  hasara  ya  Tshs 11, 752, 350, 148/=  ikiwa kama  kodi (income & withholding tax) .
Januari 2006 hadi Oktoba 2006 Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa chini ya Ibrahim Msabaha aliyeteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete. Msabaha aliondolewa kwenye wadhifa huo kufuatia kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyotisika nchini.
Oktoba 2006 hadi mwaka 2008, wizara hiyo ilikuwa chini ya Waziri Nazir Karamagi ambaye alichukua nafasi ya Msabaha. Lakini kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, naye aliondolewa kwa kashfa ya Richmond.
Tangu mwaka 2005, waziri aliyedumu kwa muda mrefu kwenye Wizara ya Nishati na Madini ni William Ngeleja aliyehudumu kuanzia mwaka 2008 hadi 2012. Lakini naye jinamizi la wizara hiyo halikumuacha baada ya kuondolewa kwa kile kilichodaiwa alikuwa waziri mzigo hivyo hawezi kumsaidia Rais.
Baada ya Ngeleja kuondoka mwaka 2012, nafasi yake ilijazwa na Prof. Sospeter Muhongoaliyeaminika angeisaidia wizara hiyo kutokana na kiwango chake kikubwa cha elimu. Lakini ilipofika mwaka 2015, aliondolewa kufuatia kashfa ya Tegeta Escrow ambayo ilimkumba pia aliyekuwa waziri, William Ngeleja pamoja na viongozi wengine.
Wakati Rais Kikwete akimalizia mwaka wake wa mwisho madarakani, Januari 2015 alimteua George Simbachawene kuongoza wizara hiyo ambapo alishika madaraka hadi Disemba 2015 wakati Rais Dkt Magufuli alipoingia madarakani na kumhamishia Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Katika baraza la mawaziri la kwanza, Rais Dkt Magufuli alimrejesha tena Prof. Muhongo kushika wizara hiyo ambapo amekaa madarakani tangu Disemba 2015 hadi Mei 24, 2017 baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake kufuatia kashfa kwenye sekta ya madini.
Bado haijafahamika kuwa ni nani atateuliwa tena kujaza nafasi hiyo ambayo imekuwa ni ngumu sana kuongoza. Kitendawili kingine ambacho kipo mbele kwa sasa, ni nani atakayesoma bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni kwa mwaka wa fedha 2017/18 kutokana na kutokuwa na waziri.
Kanuni za Bunge zinataka waziri ndiye asome bajeti bungeni, na si Naibu Waziri au mtendaji mwingine yeyote wa Wizara. Baadhi ya waliotoa maoni yao wamesema kuwa huenda Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene akasoma kutokana na kuwa amewahi kuongoza wizara hiyo, lakini wengine wanasema, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Kabudi huenda akasoma bajeti hiyo.
Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kusomwa bungeni Alhamisi na Ijumaa (Juni 4 & 5) mwaka huu, huku mjadala wa madini ukitarajiwa kuchukua nafasi kubwa.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post