SHAIRI : MAPENZI YANAKANGANYA HATUJUI YATOKAKO, HATUJUI YATOKAKO

Ninapiga Bismillah, kwa jina lake Mwenyezi
Aliyetukuka Mola, Wa pekee aso mwenzi
Nitajaribu inshallah,kuelezea mapenzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Naliona swali gumu, Lilokosa jibu wazi
Lataka mtaalamu, Alojaliwa ujuzi
Pia mie ninahamu, Kuyaelewa mapenzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Ninamkumbuka babu, Wa zamani marehemu
Aliyetoa jawabu,   Kusema kila sehemu
Mapenzi kitu ajabu,Na hasa kwa binadamu
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Mpende akupendaye, Ndio raha ya mapenzi
Yule akuchukiaye,  Takufanyia ushenzi
Ni msemo wake yeye,Alonena toka enzi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Nimejaribu uliza, Kwa waliofunga ndoa
Waweze kuniongoza,Nami nipate kuoa
Nikaambiwa tongoza,Mambo yatakuwa poa
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Wanaume tuna tabu, Tutafutao ni sisi
Waeza pata aibu, Kwa tamaa kama fisi
kwanza piga mahesabu, Usitake vya upesi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Mapenzi yakuridhisha, Kuyapata si rahisi
Kwa kweli inatutisha, Na kutupa wasiwasi
Maana ndio maisha, Ya kila mtu binafsi
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Unaeza kudhania, kwamba umeshampata
Mzuri kupindukia,Na wala aso matata
Mara ukashitukia,Mwengine kamfuata
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Duniani kuna mambo, Siku hizi mpaka pesa
Wanazipenda warembo,Ni mtindo wa kisasa
Usije jitoa chambo, Mwishowe ukamkosa
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Tabia zao mabinti,Huwa wana lao lengo
Ukifanya utafiti, Utakuta ni waongo
Kwanza atakudhibiti, Baadaye ni maringo
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Sio hapa tu mjini, Mapenzi yatuadhibu
Mpaka na vijijini, Utaona maajabu
Madawa wanaamini, Waganga na matabibu
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Hujasikia walimu, Waitumiao dini?
Mapenzi kuyafahamu,Kuelewa kwa undani
Wakamvuta Saumu,  KWa kufukiza ubani
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Nimetatizwa na swali,Lako we kaka Omari
Isitoshe usijali,    Nazidi kutafakari
Jibu lake si kamili, Wasemavyo ni kadari
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
Japo moyo waumia, Usichoke kusubiri
Ni kweli umekawia,Vumilia kijasiri
Ipo siku nakwambia,Utampata mzuri
Mapenzi yanakanganya,Hatujui yatokako
HAMZA A. MOHAMMED

kama ulikosa swali la shairi hili soma hapa MAPENZI NI KITU GANI?
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post