SHAIRI : NI MSIBA WA TAIFA, MEI SITA YA MAJONZI

Nawasha yangu kurunzi, Nianze andika utenzi 
Moyoni nina majonzi, Mwili wajawa na ganzi 
Ghafla nashusha pumzi, Kumshukuru Mwenyezi 
Ni Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Ghafla simu nafungua, WhatsApp naingia 
Taarifa zimeenea, Picha za Kusisimua 
Ajali imetokea, Ni Mlima wa Rhotia 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Gari limetumbukia, Wanafunzi limeua 
Thelathini na kadhaa, Na walimu wao pia 
Dereva hajabakia, Tanzia kote Tanzia 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Hao wanafunzi wetu, Hao ni watoto wetu 
Hao ni walimu wetu, Hao wote ndugu zetu 
Hao ni Kizazi chetu, Poleni wana Karatu 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Pole kwa wao wazazi, Walojawa na majonzi 
Moyoni tuna Simanzi, Machoni tuna Machozi 
Hiyo kazi ya Mwenyezi, Amefanya kwa Mapenzi 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Kwa pamoja tunalia, Tunalia Tanzania 
Hii kwetu ni Tanzia, Huzuni imetujaa 
Tuzidi kuwaombea, Peponi pakufikia 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Tunapita Hii Dunia, Hakuna ato bakia 
Wao wametangulia, Sisi tutawafuatia 
Kikubwa kujiandaa, Kwa Mungu kutubia 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Walichanua kama maua, Wamezima kama taa 
Kifo ni mlango pia njia, Na sote tutaupitia 
Kikubwa kujiandaa, Kwa ibada zenye kufaa 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Lucky Vicent leo Simanzi, Kuwapoteza wanafunzi 
Kwao tuliwapa mapenzi, Pamoja bora malezi 
Kuwarudisha Hatuwezi, Tumshukuru Mwenyezi 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi

Mwisho nitoe pole, Kwake mkuu wa shule 
Wazazi wa watoto wale, Watanzania pia Pole 
Njia yetu ni Ile Ile, Hatutaishi milele 
Huu Msiba Wa Taifa, Mei Sita Ya Majonzi.

Eee Mwenyezi Tunakuomba Utupe moyo wa subira na Uvumilivu katika kipindi Hiki kigumu, pia Tunakuomba Utupe mwisho mwema
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Azilaze Roho Za Marehemu Mahali Pema Peponi Aamin

Shairi hili limetoka Whatsapp
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post