STUDIO MPYA ZA KISASA ZA TBC KUJENGWA MJINI DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Mei, 2017 amefanya ziara katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amekagua miundombinu ya shirika hilo na kuzungumza na wafanyakazi.
Mhe. Rais Magufuli amejionea jinsi miundombinu ya shirika hilo inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni na amesema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya ya studio za kisasa za kurushia matangazo katika makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ambaye hivi karibuni ametoa Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Mwezi Oktoba 2016,zilizofikia shilingi Bilioni 1 na milioni 285.
Mhe. Rais Magufuli ametaka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.
“Msemaji wa Serikali mkubwa ni TBC1 na Redio ya Taifa, nyinyi hamuwezi mkawa kama vyombo vingine ambavyo vina malengo yao ya kufanya biashara, nyinyi kazi yenu ni kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania bila kubagua vyama vyao, bila kubagua dini zao, bila kubagua makabila yao, huo ndio uwe msimamo mkuu.
“Mmetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, hilo ni lazima niseme,  hata vipindi vyenu ukiviangalia ni vizuri vinaeleza mpaka maisha ya vijijini, na mimi ni shabiki mkubwa sana wa TBC, lakini tatizo lenu mnashindwa kwenda na wakati wa sasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliyekuwepo katika ziara hiyo kuuangalia Mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bw. Tao Zhang na kuishukuru IMF kwa kuendelea kuwa wadau wa maendeleo wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemueleza Bw. Tao Zhang kuwa Tanzania inatekeleza mpango wa pili wa maendeleo utakaoiwezesha kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo ameiomba IMF kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu, uwekezaji katika viwanda na kuwahamasisha wadau wengine kuwekeza hapa nchini.
Kwa upande wake Bw. Tao Zhang amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kusimamia uchumi wa Tanzania na amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua vizuri tangu miaka 20 iliyopita ukichagizwa na uwepo wa sera nzuri na mipango imara ya mageuzi, na kwamba anaamini kuwa uongozi mzuri wa Mhe. Rais Magufuli akishirikiana na wadau wa maendeleo wataendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi duniani.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Mei, 2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post