CHADEMA KUPEPERUSHA BENDERA NUSU MLINGOTI NCHI NZIMA

Kufuatia msiba wa mmoja wa waasisi wa CHADEMA, Mzee Philemon Ndesamburo, Katibu Mkuu wa Chama, Dokta Vincent Mashinji ametangaza kuanza kwa maombolezo nchi nzima ikiwa ni pamoja na bendera za chama kupepea nusu mlingoti kama ishara ya kuenzi na kuthamini mchango wa mwasisi huyo katika harakati za kuanzisha, kujenga Chadema na mageuzi nchini.
Dokta Mashinji amesema maombolezo hayo yanaanza mara moja na kwamba chama kinatoa fursa kwa wanachama wake, wapenzi na wote walioguswa na msiba huo kufika Makao Makuu ya Chadema Kindondoni Jijini Dar es salaam kutoa salaam zao za pole na kusaini kitabu cha maombolezo.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu Dokta. Mashinji amesema “kutokana na msiba huu mzito wa Mzee wetu ambao tumeupokea kwa mshtuko mkubwa katika kuonesha kuguswa sio tu kwa Chadema bali wote wanaopenda mabadiliko nchini, bendera zetu zitapepea nusu mlingoti hadi safari ya kumpumzisha katika makazi yake ya milele itakapokuwa imekamilika.”
Akimzungumzia Mzee Ndesamburo, Katibu Mkuu Dokta Mashinji amemtaja kama mmoja wa waasisi na kiongozi wa kisiasa aliyesimamia kwa vitendo sera za Chama chake za kutaka maendeleo ya kijamii na kubakia kuwa mfano wakati wote wa uhai wake kwa kuweka mbele msukumo wa umoja wa kitaifa.
“Alishiriki kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kidemokrasia. Mwaka 1995 kuelekea uchaguzi mkuu alikuwa mmoja wa waanzilishi wa UDETA (Umoja wa Demokrasia Tanzania), baadae alikuwa sehemu ya kuanzisha UKAWA, mwaka jana amekuwa sehemu ya kuanzisha UKUTA. Haya yote unayaona ni maisha ya kuhakikisha umoja katika taifa letu,”ameongeza Dokta Mashinji.
Katibu Mkuu Dokta Mashinji amesema kuwa taarifa zaidi kuhusu msiba huo, hasa ratiba ya mazishi, zitaendelea kutolewa kwa kushirikiana na kushauriana na familia.
Akimzungumzia Mzee Ndesamburo namna atakavyokumbukwa hasa na vijana na viongozi wa kisiasa wa wakati huu, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Zanzibar, Salum Mwalim amesema kuwa Mzee Ndesamburo atabakia kuwa kielelezo cha dhamira ya dhati ya mpigania mageuzi aliyejitoa kwa hali, mali na nafsi yake yote.
“Dhamira yake ilikuwa ya kweli na ya dhati kabisa, alishiriki kuanzisha Chama, akapigania na kuwa mshirika wa hatua zote za mafanikio ya chama na mageuzi nchini. Hakukata tamaa wala hakukinai mafanikio ambayo yamekuwa yakipatikana kwani kwake jambo kubwa lilikuwa ni kuona Chadema inashika dola na inawapatia Watanzania mabadiliko ya kweli,” amesema Mwalim.
Mwalim aliongeza, “alikuwa na kila sababu ya kukaa pembeni au kuwa tu mchangiaji lakini aliweza kuunganisha nguvu zake za kiuchumi na dhamira yake ya mageuzi iliyolenga kuleta mabadiliko katika maisha ya watu na imekuwa hivyo hadi mauti yalipomkuta akiwa katika hatua za kusaidia wafiwa wa shule ya Lucky Vincent huku akiwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa.”
Kwa upande wake mmoja wa waasisi wa chama, Mzee Victor Kimesera, ambae amekuwa na Mzee Ndesamburo tangu wakati wa kukianzisha Chadema, amemwelezea Mzee Ndesamburo kama mtu aliyechangia mawazo na fedha kukifikisha Chadema kilipo hivi sasa.
Mzee Kimesera amesema haikuwa rahisi kwa wakati huo kwa mfanyabishara wa ngazi ya Mzee Ndesamburo kujiweka wazi kudai mabadiliko huku akitoa mali zake, lakini yeye alifanya kwa kuwa aliamini katika kuwapatia Watanzania mabadiliko kupitia mfumo wa vyama vingi huku akijua kufanya hivyo kungeweza kuhatarisha biashara zake.
Imetolewa leo Alhamis, Juni 1, 2017 na
Tumaini Makene*
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post