MAAZIMIO 8 YALIYOPITISHWA NA BUNGE KUHUSU SAKATA LA TEGETA ESCROW

Wakati Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe anawasilisha ripoti ya sakata la Tegeta Escrow Bungeni mwaka 2014, kamati hiyo ilipendekeza mambo manane yafanyike baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa fedha zilizogawanywa kwa watu mbalimbali zilikuwa za umma.
Miongoni mwa mapendekezo ambayo kamati ilitoa ilikuwa ni kukamatwa kwa Mkurugenzi wa PAP, Harbinder Singh Seth pamoja na wengine watakaogundulika kuhusika katika sakata hilo. Azimio hili la kwanza lilitekelezwa jana ambapo Seth pamoja na mfanyabishara James Rugemarila walifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka 6 ya uhujumu uchumi.
Katika sakata hili atakumbukwa aliyekuwa Mbunge katika bunge la 10, David Kafulila ambapo alisimama kidete katika sakata hili na kusema kuwa fedha za Escrow zilikuwa ni mali ya umma.
Hapa chini ni maadhimio 8 yaliyopitishwa na Bunge mwaka 2014 baada ya ripoti ya kamati kusomwa bungeni.
1. Bwana Harbinder Singh Seth na wengine
Bunge linaazimia kwamba, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.
2 Mitambo ya IPTL
Bunge linaazimia kwamba, Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme wa IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.
3 Mapitio ya Mikataba ya Umeme ( Azimio la Kamati teule ya Richmond)
Bunge linaazimia kwamba, Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti la Mwaka 2015/2016, Serikali iwasilishe Taarifa ya Utekelezaji wa Mapitio ya Mikataba ya Umeme;
4 Kitengo cha Rushwa kubwa
Bunge linaazimia kwamba; Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU, kwa lengo la kuanzisha Taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibidi vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
5 Majaji
Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania. (Makofi)
6 Benki ya Stanbic na Benki Nyingine
Bunge linaanzimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni Taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of Money Laundering Concern).
7 Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu na Bodi ya TANESCO
Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri Mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
8. William Ngeleja, Victor Mwambalaswa na Andrew Chenge
Bunge linaazimia kwamba, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao kwenye Kamati husika za Kudumu za Bunge.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post