MIZENGO PINDA ATAKA KIJIJI CHAKE KIBADILISHWE JINA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda ameiomba serikali kubadilisha jina la kijiji anachoishi kwani jina hilo si zuri na haliendani na aina ya wakazi wa eneo hilo kwani ni wachapakazi.
Pinda ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Zuzu ameiomba serikali kubadilisha jina hilo na kukiita kijiji hicho Zinje kwani neno Zuzu halina maana nzuri kwenye kamusi ya kiswahili na wakazi wa kijiji hicho ni wachapakazi.
Kiongozi huyo ambaye ni mkulima mkubwa ameyasema hayo wakati mbio za mwenge zilipofika kijiji hapo na kutembelea miradi ya kilimo na ufugaji anayoifanya yeye kwa kushirikiana na wakazi wengine wa eneo hilo.
Akitoa maombi hayo, Pinda alisema kwamba amependekeza jina la Zinje kwani aliliona ni zuri na linaendana na shughuli zinazofanywa na wakazi wa eneo hilo.
“Nimejaribu kutafuta neno hilo la zuzu na kuona lina maana mbaya, ndiyo maana nimeomba pabadilishwe na kuitwa Zinje ambayo ina maana fulani ndani ya eneo hili,” alisema Pinda
Akielezea maana neno Zinje, alisema, lina maana ya jiwe laini ambalo hupatikana maeneo hayo na wazee wa zamani walikuwa wakilitumia kutengeneza kiko cha kuvutia tumbaku.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambapo ndipo Pinda anaishi, Jordan Rugimbana alisema kuwa atalifanyia kazi ombi hilo.
Kuhusu shughuli zake za kilimo, Pinda anayelima nyanya, hoho, zabibu na pilipili pamoja na kujihusisha na ufugaji, alisema anamshukuru Mungu kwamba mambo yanakwenda sawasawa.
Kilimo ni jambo zuri kama kitafanyika kwa ufasaha na umakini mkubwa. Ni wakati sasa wa jamii kupewa elimu kuhusu namna bora ya kulima ili waweze kufaidika kutoka na kazi hiyo, alisema Pinda.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Amour Hamad Amour, alisema kuna kila sababu ya wananchi kwenda kujifunza suala la kilimo katika shamba darasa la kiongozi huyo.
Alisema Pinda anastahili pongezi kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kuendesha kilimo na kutoa mafunzo kwa wengine wanaopenda kujifunza kilimo na ufugaji wa nyuki na mifugo mingine.
Kutokana na jitihada zake za kilimo, ufugaji na kutoa elimu ya kilimo, Pinda alikabidhiwa cheti cha pongezi kama ishara ya kazi nzuri ya ufugaji na kilimo ambayo anaifanya katika shamba hilo.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post