POLISI WATOA KAULI KUHUSU MADAI YA WALEMAVU KUPIGWA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo limezungumzia kwa mara ya kwanza madai yaliyokuwa yakienezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Askari wa jeshi hilo walitumia nguvu iliyopitiliza walipokuwa wakikabiliana na walemavu wa viungo waliokuwa wamefunga barabara wakishikikiza kuonana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Jeshi hilo limesema kuwa halikutumia nguvu kupita kiasi kama inavyodaiwa lakini walitumia nguvu kulingana na watu waliokuwa wakifanya maandamano hayo.
“Hatujatumia nguvu ya kupita kiasi. Tumetumia nguvu kulingana na hali ya watu ambao walikuwa wanafanya maandamano hayo.”
Hayo yamesemwa leo na Naibu Kamishna wa Polisi ambaye ni Mkuu wa Operesheni za Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lakini kwa sasa anakaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu kazi mbalimbali ambazo zimefanywa na jeshi hilo.
Mkondya alitoa rai kwa wananchi kuwa, ulemavu sio kigezo cha kuvunja sheria na kwamba sheria zipo na wao wanazitekeleza kwa wananchi wote bila ubaguzi wowote, hivyo ni vyema wananchi wakatii sheria bila shuruti.
“Nataka nitoe rai kwa wananchi, ulemavu sio kibali cha wewe kuvunja sheria wala ulemavu haukupi wewe uhalali wa kuvunja sheria za nchi. Sheria za nchi zipo kwa mtu yeyote yule mzima au mlemavu, na hasa ambaye anazifunja kwa makusudi akijua.”
Naibu Kamisha Lucas alisema kuwa walemavu wale walifanya makosa ya kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa lakini pamoja na hivyo wakafunga njia. Alisema kuwa walipojaribu kuongea nao wafungue njia na pia wateua viongozi wa kushughulikia matatizo yao, walikaidi.
Kutokana na hali hiyo, Mkondya alisema walilazimika kutumia nguvu kidogo kuwaondosha eneo hilo na watu wengine wakaendelea na shughuli zao.
Kiongozi huyo amewataka walemavu kutii sheria za nchi kwani kazi za Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao, na kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa kwani nje ya hapo litakuwa halifanyi kazi yake.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post