AGIZO LA MAGUFULI LATEKELEZWA, MALARIA KUWA HISTORIA NCHINI MIAKA MITANO IJAYO

LITA zote 100,000 za dawa ya kuua mazalia ya mbu zilizokuwa zimerundikana katika ghala la kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia cha viuadudu kilichopo mjini Kibaha zimechukuliwa na Halmashauri kama ilivyoagizwa na Rais Dkt. John Magufuli hivi karibuni.
Kaimu Meneja wa kiwanda hicho, Samwel Mziray alisema jana kuwa agizo hilo la Rais Magufuli limetekelezwa na Wakurugenzi ndani ya kipindi kifupi.
Dkt. Nicholaus Banzi, mtaalam wa udhibiti wa ubora wa kiwanda hicho akionesha baadhi ya shehena ya dawa iliyo tayari kwa matumizi
Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Pwani, Rais Magufuli alitembelea kiwanda hicho na kuagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wakachukue dawa hizo zenye thamani ya Sh. bilioni 1.32 alizoziagiza Wizara ya Fedha na Mipango ilipe.
Ijumaa ilikuwa siku ya mwisho kwa Wakurugenzi kutekeleza agizo hilo.
“Hadi kufikia jana (Jumapili) mikoa 14 ambayo imeathirika zaidi na Malaria tayari ilikuwa imeshachukua dawa zote zilizokuwa ghalani,” alisema Mziray. “Kila Halmashauri imepata lita 500 na mikoa 12 iliyobakia itatakiwa kuanza kuchukua ifikapo Julai 10.
“Tunamshukuru sana Rais wetu John Pombe Magufuli kwa kuonyesha mfano na kununua mwenyewe dawa kupitia Wizara ya Fedha.”
Alisema kama ikitumika vizuri, katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ugonjwa wa Malaria unaweza kuwa historia nchini kutokana na dawa hiyo isiyo na madhara kwa binadamu, mimea na hata wanyama wa aina zote.
Alisema kiwanda kinaendelea kuzalisha dawa zenye ubora ili kumuunga mkono Rais na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mapambano dhidi ya Malaria nchini.
Mziray alisema Halmashauri zote zitapata muongozo wa namna ya kutumia dawa hizo kupitia kitengo cha kudhibiti Malaria cha wizara hiyo na hivyo wananchi hawapaswi kuwa na uoga pindi dawa hizo zitakapokuwa zikinyunyizwa kwenye madimbwi na mazalia mengine ya mbu katika maeneo wanayoishi.
Sehemu ya mitambo ya kisasa ilivyofungwa kiwandani hapo
Alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha dawa lita milioni sita kwa mwaka na wanatarajia asilimia 80 ya dawa hizo zitatumika nchini na asilimia 20 zitauzwa nje ya nchi.
Malaria bado ni ugonjwa hatari nchini na ukitajwa kusababisha vifo vya wastani wa watu 80,000 kila mwaka.
Jumatatu iliyopita Kaimu Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto –Idara Kuu ya Afya, Catherine Sungura, alisema dawa hizo zingegaiwa Halmashauri za mikoa 14 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria.
Kwa mujibu wa Sungura, mikoa iliyokuwa ianze kupata mgao huo, na kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwenye mabano ni Kagera (41%), Geita (38%), Kigoma (38%), Ruvuma (23%), Tabora (20%) na Mtwara (20%).
Mingine ni Mara (19%), Morogoro (14%), Shinyanga (17%), Lindi (17%), Pwani (15%), Mwanza (15%), Katavi (14%) na Simiyu (13%).
HT @ Nipashe
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post