MAKAMBA AELEZA DOSARI ALIZOZIBAINI NEMC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari Makamba.
WIKI iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari Makamba alivunja Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lakini baadaye uamuzi wake huo ulitenguliwa na mamlaka za juu. Je, kwa nini aliamua kuchukua hatua ya kulivunja baraza hilo? Fuatilia hapa:
SWALI: Nini umuhimu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira?
JIBU: Kama mnavyofahamu Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ni muhimu sana katika kuhakikisha ustawi wa mazingira na mustakabali wa maendeleo endelevu ya nchi yetu. Tunapoelekea kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, usimamizi wa mazingira lazima uwe imara na urahisishe na kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa viwanda, miradi mbalimbali na uwekezaji katika sekta zote ili kwenda kwa kasi na weledi unaotakiwa.
SWALI: Utendaji wa NEMC unalalamikiwa na kuna tuhuma za rushwa, malalamiko hayo yamehusu nini hasa?
JIBU: Utendaji wa NEMC ni kweli umekuwa unalalamikiwa na umekuwa ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi. Siku za hivi karibuni pamekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje na wananchi wengi pia. Malalamiko hasa yamehusu mambo yafuatayo, ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA); tuhuma za rushwa katika mchakato wa ukaguzi na tathmini ya athari kwa mazingira; mazingira ya rushwa katika kutengeneza vyeti ambavyo havijafuata mchakato stahiki; kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja na kuwatisha ili watoe chochote; kutumia makampuni binafsi ya watumishi wa NEMC kufanya kazi za ukaguzi/ uhakiki wa ndani ya NEMC kwa kisingizio cha kutokuwa na watumishi wa kutosha; kuwaelekeza wawekezaji kwa makampuni ya kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) ambayo yanamilikiwa au yenye ubia na watumishi wa NEMC hivyo bila kujali mgongano wa kimasilahi, mambo ambavyo hayaruhusiwi kwenye utumishi wa umma; kuwarundikia maandiko ya miradi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) watumishi wachache wakati wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hii katika makampuni ambayo baadaye huwapatia malipo yasiyo halali. Baadhi ya wenye makampuni ambako miradi hii hupelekwa ni watumishi wa NEMC ambao wameacha au wameachishwa kazi.
SWALI: Kama hali ni hiyo wizara imefanya nini kurekebisha?
JIBU: Kwa kipindi kirefu, tumejitahidi kurekebisha hali hii na kumejitokeza nafuu lakini bado hali haijafikia pale nilipotarajia.
SWALI: Unadhani hali hiyo imesababishwa na nini?
JIBU: Nimefuatilia kwa karibu na kugundua kuwa matatizo mengi haya na mengine ya msingi yanasababishwa hasa na usimamizi usio imara wa bodi na pia watendaji wakuu wa NEMC.
Swali: Unasema nini kuhusu uwekezaji wa viwanda? Tunaambiwa kuna urasimu mkubwa wa kuanzishwa viwanda nchini.
JIBU: Kufuatia maamuzi ya Bunge na maelekezo ya mheshimiwa rais kuhusu kuharakisha na kurahisisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), tunatangaza hatua zifuatazo: Miradi yote inayohusu ujenzi wa viwanda, baada ya mwekezaji kuwasilisha taarifa hitaji la ujenzi wa kiwanda kwa NEMC, ruhusa ya ujenzi wa kiwanda itatolewa ndani ya siku tatu za siku za kazi wakati mchakato wa EIA unaendelea bila kuzuia wala kuchelewesha ujenzi wa kiwanda. Iwapo kutajitokeza changamoto, zitarekebishwa wakati wa mradi unaendelea na iwe ni sehemu ya “environmental management plan – EMP”. Kutakuwa na Dawati Maalum la Miradi ya Viwanda pale NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais ili kushughulikia kwa haraka maswali ya masuala yote yanayohusu ujenzi wa viwanda.
SWALI: Nani atagharamia tahmini ya kimkakati za mazingira kama kuna mtu anataka kujenga viwanda?
JIBU: Maeneo yote yanayopangwa kujengwa viwanda, baada ya kujulikana, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, zitagharamia Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira (TAMK) – Strategic Environmental Assessment (SEA). Suala hili litaondoa haja ya kila kiwanda kufanya EIA kamili. Viwanda vidogo vitakavyojengwa katika maeneo hayo maalum havitahitaji Cheti cha EIA labda kwa sababu maalum ambazo zitatolewa na NEMC, na waziri lazima aridhie kwanza. Kwa msingi huo, tunasisitiza wizara husika zitenge maeneo ya ujenzi wa viwanda ili sisi tuyafanyie tathmini ya mazingira ya pamoja kwa eneo lote. Miradi yote midogo na ya kati inayohusiana na viwanda vya kilimo na mifugo na uvuvi (small and medium scale agro processing industries) katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo yatasamehewa gharama za kufanyiwa TAMK. Taarifa za miradi hii zitatolewa kwa afisa mazingira wa eneo husika ili kuhakikisha wawekezaji wanasaidiwa kuzingatia kanuni bora za mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi hii. Kama kuna haja ya baadhi ya miradi kufanyiwa tathmini wakati wa utekelezaji, fedha za kazi hiyo zitatolewa na serikali kama sehemu ya OC.
SWALI: Ni miradi ipi itakuwa inapelekwa NEMC kuombewa cheti?
JIBU: Kuanzia sasa miradi itakayopelekwa NEMC kuombewa Cheti cha EIA ni ile ambayo tayari imefanyiwa kazi na washauri elekezi (consultants). Hapatakuwepo na haja ya kusajili mradi NEMC kwanza. NEMC itaweka maafisa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na maeneo mengine muhimu ili kuhakikisha suala la kuwa na cheti cha mazingira linakuwa sehemu ya hatua za awali pale ambapo mwekezaji au mwenye mradi anapoanza kuomba vibali vingine. Aidha, utaratibu huu utatangazwa katika magazeti yote muhimu na vyombo vingine vya habari.
MWANDISHI: Asante sana kwa ushirikiano wako.
 MAKALA: ELVAN STAMBULI NA SIFAEL PAUL | UWAZI | GLOBAL PUBLISHERS
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post