MASHTAKA 7 ALIYOSOMEWA YUSUF MANJI AKIWA HOSPITALI YA MUHIMBILI

Jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilihamia kwa muda katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuweza kumsomea mashtaka Yusuf Manji aliyekuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Manji pamoja na wenzake watatu wakiwa hospitalini hapo walisomewa mashtaka saba ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa kufuatia tuhuma zinazowakabili za kukutwa na jora za vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Tsh 200 milioni na mihuri
Watuhumiwa wengine wanaokabili na mashtaka pamoja na Manji ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43).
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali Tulumanywa Majigo alidai kuwa, Juni 30, 2017 katika eneo la Chang’ombe A, Dar es Salaam watuhumiwa wote wanne walikutwa wakiwa na bunda 35 za vitambaa vinavyotumiwa kutengeneza sare za JWTZ zenye thamani ya Tsh 192.5 milioni na kwamba mali hiyo ilipatikana kinyume na sheria.
Katika shtaka la pili, Julai Mosi watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa kukutwa na mabunda manane yanayotumika kutengeneza sare za JWTZ zenye thamani ya Tsh 44 milioni mali ambayo haikupatikana kihalali.
Katika shtaka la tatu, Juni 30 watuhumiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kukutwa na muhuri unaosomeka “Mkuu 121 Kikosi cha JWTZ” bila kuwa na uhalali wa kumiliki kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.
Akisoma shtaka la nne, Wakili wa Jamhuri alisema Juni 30 watuhumiwa wote walikutwa na muhuri unaosomeka “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupola Dodoma” kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa taifa.
Shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao ni kuwa, Juni 30 walikutwa na muhuri wa JWTZ unaosomeka “Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.O Box 224 Korogwe” kitendo kinachohatarisha usalama wa taifa.
Wakili akiwasomea shtaka la sita alidai kuwa, Juni 30 watuhumiwa walikutwa na namba ya usajili SU 383 ambayo ilipatikana kinyume na sheria.
Katika shtaka la mwisho, Julai Mosi watuhumiwa hao walikutwa na Jeshi la Polisi wakiwa na namba za usajili wa gari SM 8573 iliyopatikana kwa njia isiyo halali.
Baada ya watuhumiwa hao kusomewa mashtaka hayo hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) hakuipa mamlaka ya kuisikiliza.
Mawakili wa upande wa utetezi waliitaka mahakama hiyo kutopokea hati hiyo ya mshataka kwani haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo huku wakilalamikia wateja wao kushikiliwa kwa zaidi ya saa 48 bila dhamana kitendo walichodai ni nio ovu ya Jeshi la Polisi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 19 itakapotajwa tena.


JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post