MORATA: JEMBE LA CONTE!

Straika wa Chelsea, Alvaro Morata.
WAKATI Real Madrid ikisema bei ya straika wake Alvaro Morata, 24, inakadiriwa kuwa pauni milioni 60 (Sh bilioni 172), ilionekana kama haitaki kumuuza mshambuliaji huyo chaguo la pili nyuma ya Karim Benzema.

Lakini Chelsea imekubali kulipa kiasi hicho cha fedha ili imsajili Morata kwani tayari Kocha Antonio Conteamekorofishana na straika wake Diego Costa, hivyo Morata anakuwa mbadala wa Costa.

Usajili wa Morata Chelsea unakuja baada ya Conte kumkosa Romelu Lukaku kutoka Everton ambaye alisajiliwa na Manchester United na tayari ameanza kuonyesha umuhimu kikosini.
Alvaro Morata akiwa katika pozi.

Alhamisi wiki hii, Morata alikwenda London kwa ajili ya vipimo vya afya ili kukamilisha usajili wake Chelsea na majibu yakawa poa.

Mapema wiki hii zilizagaa video za Morata zikimuonyesha akiaga wenzake katika mazoezi ya Real Madrid na kuthibitisha kwamba wakati wake wa kuondoka umewadia.

AMSHUKURU ZIDANE
Morata ni muungwana kwani mapema wiki hii, alinukuliwa akimshukuru Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane kwa ushirikiano aliompa kikosini pia aliwashukuru mashabiki waliotaka abaki Madrid.

“Namshukuru Zidane, ni kocha bora ambaye kila mchezaji angetaka kufanya naye kazi niliishi naye vizuri na pia niwashukuru mashabiki walionitakia heri muda wote Madrid,” anasema Morata.

Msimu uliopita Morata raia wa Hispania alifunga mabao 20 licha ya kucheza asilimia 34 tu ya mechi zote za Madrid. Alifunga mabao 15 katika ligi yaani bao moja nyuma ya yale yaliyofungwa na straika wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann.

YUPO FASTA KULIKO BALE
Aprili mwaka huu, takwimu zilizotolewa na jarida moja la michezo la Hispania, lilimweka Morata kuwa miongoni mwa wachezaji wenye kasi katika kikosi cha Madrid akimzidi Gareth Bale.

Morata alishika nafasi ya tatu nyuma ya beki Nacho Fernandez na kiungo Mateo Kovacic. Hata Bale alishika nafasi ya nne.

MZURI HEWANI KULIKO COSTA
Kama ukipima kuhusu uchezaji wa mipira ya juu kati ya Costa na Morata, Morata anaonekana yupo vizuri kwa kucheza mipira ya juu ya aina zote kuliko Costa.

Mchezaji mwenzake wa kikosi cha zamani cha vijana cha Madrid, Lucas Vazquez amesema alikuwa straika wa timu hiyo hadi Morata alipojiunga na timu hiyo naye akabadili nafasi.

Vazquez amewahi kunukuliwa akisema, alihama nafasi kutokana na Morata kufanya vizuri katika upigaji vichwa na akajiona yeye hana nafasi katika ushambuliaji wa kati na akahamia pembeni.

ANAIFUATA CHELSEA CHINA
Hadi juzi Alhamisi Morata alikuwa London akimalizia baadhi ya taratibu za uhamisho wake akiwa ametokea katika kambi ya Madrid huko Marekani.

Straika huyo anatarajiwa kwenda China wikiendi hii na kuna uwezekano akaichezea Chelsea dhidi ya Bayern Munich Jumatano ijayo kabla ya kuivaa Inter Milan siku tatu baadaye.

NI UHAKIKA SASA
Morata anasema: “Nakwenda katika timu ambayo kocha wake ameweka matumaini yake makubwa kwangu. Nina furaha kubwa.

“Niseme tu, sifikirii kama nitarejea Madrid, ni ngumu mno kurudi nyuma kwa hili linaloendelea sasa na kile ninachokifikiria.

“Ni wazi kwamba lengo langu ni kuondoka, siwezi kuwa kimya tena ni lazima niondoke.”

CHAGUO SAHIHI
Kocha wa zamani wa Middlesbrough, Aitor Karanka aliyewahi kufanya kazi na Morata akiwa kocha msaidizi Madrid wakati wa Jose Mourinho, anasema: “Ni mtu sahihi kwa Ligi ya England, kwa sababu ana nguvu, anajua kupambana, mzuri akiwa na mpira, mzuri hewani.
“Na jambo muhimu kwa mchezaji kijana kama yeye, ni kutakiwa kuongeza kiwango chake kila siku na hili ndilo jambo la msingi.”
Hata hivyo, Karanka ameonya kumfananisha Morata na Costa.
“Morata ni tofauti na Costa. Costa ni mpambanaji, muda wote anapambana, Morata ni tofauti. Sitaki kusema Morata ni mzuri au mbaya mbele ya Costa lakini anaweza kufanya vitu tofauti.”
LONDON, England | Championi Jumamosi
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post