MWANAMUZIKI NCHINI INDIA APIGA GITAA AKIWA ANAFANYIWA UPASUAJI WA UBONGO

Mwanamuziki mmoja nchini India alikuwa akipiga gitaa wakati anafanyiwa upasuaji wa ubongo ili kuwasaidia madaktari kutibu misuli inayotakiwa kufanya kazi bila kuamriwa na ubongo (involuntary muscle spasms) katika vidole vya mikono yake.
Mwanamuziki huyo, Abhishek Prasad alikuwa anapiga gitaa hilo kila wakati ambao madaktari walikuwa wakichoma baadhi ya misuli kwenye ubongo wake ili kutibu ugonjwa wa mishipa ya fahamu ambao unatokana na ubongo kutotuma taarifa sahihi kwenye misuli na kuifanya ikakamae kwa muda mrefu ambao kitaalamu unajulikana kama “musician’s dystonia”.
Ugonjwa huu husababisha misuli kukakamaa na kuuma, kujikunja na kutetemeka mara kwa mara au kukaa bila mpamgilio.
Baada ya kufanyiwa upasuaji, Prasad aliiambia BBC kwamba sasa anaweza kupiga gitaa lake kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa kabla ya upasuaji huo.
“Waliponichoma mara ya sita hivi vidole vyangu vikaachia kabisa. Nilikuwa nimepona kabisa wakati upasuaji unaendelea kufanyika,” alisema Prasad baada ya madaktari kutoa nyuzi kichwani kwake Alhamisi katika hospitali iliyopo jijini Bangalore, kusini mwa India.
Ugonjwa huu ulikuwa unasababisha ashindwe kuweza kuvichezesha vidole vitatu vya mkono wake wa kushoto na kufanya ashindwe kupiga gitaa vizuri.
“Mwanzo nilidhani vidole vinakakamaa kwa sababu ya kuzidisha mazoezi lakini nilipumzika na kukuta hali ni ile ile nilipoanza tena, hakukuwa na tofauti yoyote ya vidole kuachia. Baadhi ya madaktari waliniambia kuwa mishipa ilikuwa imechoka kutokana na kufanya kazi na wakanipatia dawa za kutuliza maumivu, vitamini na kuanzishwa mazoezi ya viungo,” alisema.
Alisema kuwa kukakamaa huko kwa vidole kulikuwa kunatokea akiwa anapiga gitaa tu, lakini mtaalamu wa mishipa ya fahamu alilijua tatizo hilo kwa usahihi kabisa kwamba ana ugonjwa huu miezi tisa iliyopita.
“Nilishauriwa nifanyiwe upasuaji wa ubongo lakini niliogopa sana. Ila daktari wangu, Sharan Srinivasan alinifanya niwe na ujasiri wa kukubali,” alisema.
Mwanamuziki huyo amesema kuwa anakumbuka kila kitu kilichokuwa kinafanyika ndani ya chumba cha upasuaji. Alisema kwamba anakumbuka madaktari walianza kwa kumfunga kifaa kichwani kwa ‘screw’ nne ili wakate na kufunua fuvu la kichwa kabla ya kufanya kipimo cha MRI.
“Kipimo hicho kilisaidi kujua vifaa vya kufanyia upasuaji viingizwe ndani ya ubongo kiasi gani ili kurekebisha soketi kichwani.”
Prasad akielezea alivyokuwa akijisikia wakati wa upasuaji huo alisema: alikuwa akisikia “kama jenereta limewashwa kichwani mwangu wakati nafanyiwa upasuaji, lakini sikupata maumivu.”
Daktari Bingwa aliyeongoza Upasuaji huo Dkt. Srinivasan alisema kuwa “kwenye upasuaji huo mgonjwa hapati maumivu kabisa kwa sababu upasuaji uliofanyika kwa kuwekewa dawa ya usingizi kidogo.”
Akaendelea kuwa baada ya hapo madaktari walitoboa tundu lenye upana wa milimita 14 na kuingiza kifaa maalumu ndani ya fuvu na kwenye sehemu “inayotakiwa ambayo ilikuwa umbali wa sentimita 8 hadi 9 ndani ya ubongo.”
“Alikuwa yupo macho kabisa, hajalala kabisa kwa muda wote tuliokuwa tunamfanyia upasuaji na majibu aliyapata pale pale mezani alipokuwa anafanyiwa upasuaji kwa sababu vidole vyake vilianza kuwa kawaida akipiga gitaa lake,” alisema daktari.
Baada ya upasuaji huo, Prasad alisema “mkono wangu wa kushoto na mguu wa kushoto haina nguvu kidogo, lakini nitapona ndani ya mwezi mmoja kisha nitaanza mazoezi kwa kasi.”
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post