RAIS MAGUFULI AWARUHUSU MACHINGA WAFANYE BIASHARA KWENYE KITUO CHA MABASI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa Mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 27 Julai, 2017 baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kuelekea Jijini Dar es Salaam kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu na kumueleza kero ya kunyanyaswa na Manispaa ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro SACP – Ulrich Onesphory Matei kuhakikisha Askari Mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo na amewataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewataka watu wote waliobinafsishiwa viwanda mbalimbali katika mkoa wa Morogoro kuvirejesha Serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.
“Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa mazao Mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na amewataja wakulima wa Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka  waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
27 Julai, 2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post