UTAFITI: UPUNGUFU WA MBEGU ZA KIUME WATHIBITISHA KUWA BINADAMU TUTATOWEKA DUNIANI

Daktari Dkt. Hagai Levine wa nchini Marekani amesema kwamba binadamu tunaweza kutoweka kwenye uso wa dunia kama wanaume wataendelea kukumbwa na upungufu mkubwa wa mbegu za kiume kwa kiwango kilichopo sasa.
Watafiti waliochunguza matokeo ya tafiti zilizofanyika kwa zaidi ya miaka 200 kuhusu nguvu za kiume kwa wanaume wa mabara ya Amerika Kaskazini, Ulaya, Australia na New Zealand inaonesha uwezo wa nguvu za kiume umepungua kufikia nusu katika kipindi cha chini ya miaka 40.
Baadhi ya wataalamu wana wasiwasi juu ya taarifa hiyo kuhusu uwezo wa uzaaji kwa binadamu lakini mkuu wa utafiti huo, Dkt. Hagai Levine amesema kwamba ana “wasiwasi kuhusu hali hiyo” kuhusu kinachoweza kutokea baadae.
Uchunguzi huo ambao ni mkubwa zaidi kati ya yote iliyowahi kufanyika umekusanya matoeo ya tafiti 185 zilizofanyika kati ya mwaka 1973 na 2011.
Dkt. Levine ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya milipuko aliiambia BBC kwamba kama hali itaendelea kama ilivyo sasa basi binadamu tutatoweka kutoka kwenye uso wa dunia.

Upungufu wa nguvu za kiume umeongezeka

“Kama hatutabadili maisha yetu, mazingira na kudhibiti kiwango cha kemikali kwenye mazingira yetu, nina wasiwasi sana kuhusu kitakachotokea hapo baadae,” amesema.
“Bila shaka tutakuja kuwa na tatizo, na kuzingatia uwezo wa kuzaliana kwa ujumla, bila shaka kitakachotokea ni kutoweka kwa binadamu duniani.”
Wanasayansi ambao hawakuhusika kwenye utafiti huo wamesifu kiwango cha utafiti huo lakini wakasema kwamba yawezekana kwamba kusema kuwa binadamu tutatoweka ikawa ni mapema sana.
Dkt. Levine ambaye anatoka Chuo Kikuu cha Hebrew mjini Jerusalem amesema kuwa wameona kuna upungufu wa asilimia 52.4% kwa mbegu za kiume na upungufu wa asilimia 59.3% kwa uwezo wa mbegu za kiume kwa wanaume kwenye mabara ya Amerika Kaskazini, Ulaya, Australia na New Zealand.
Kwa upande mwingine, upungufu huu haukuonekana kuwa mkubwa katika mabara ya Amerika Kusini, Asia na Afrika, lakini watafiti wanasema kuwa yawezekana sababu ikawa ni tafiti chache zilizofanyika kwenye mabara hayo. Pamoja na hayo, Dkt. Levine ana wasiwasi kuwa ni suala la muda tu kwamba hali kwenye mabara hayo yenye kiwango kidogo cha madhara kuja kuwa kama yale yaliyoathiriwa zaidi.
Tafiti nyingi zilizowahi kufanyika zimeonesha matokeo kama hayo ya kupungua sana kwa mbegu za kiume katika nchi zenye maendeleo makubwa kiuchumi lakini wapinzani wa tafiti hizo wanasema kuwa matokeo hayo si ya kweli kwakuwa tafiti nyingine zimehusisha wanaume wachache sana au wanatoa matokeo kwa kuangalia wanaume wanaohudhuria kwenye kliniki za uzazi ambao kwa vyovyote lazima watakutwa na kiwango kidogo cha mbegu za kiume. Pia kuna wanaidai kuwa tafiti zinazoonesha tatizo la upungufu wa mbegu za kiume ni rahisi sana kuchapishwa kwenye majarida ya tafiti za kisayansi kuliko tafiti zinazoonesha kinyume chake.
Profesa Allan Pacey wa Chuo Kikuu cha Sheffield amesema kuwa: siku zote huwa siziamini tafiti nyingi zinazochapishwa kuhusu kiwango cha upungufu wa mbegu za kiume lakini utafiti huu uliofanywa na Dkt. Levine na wenzake umeondoa utata mwingi uliokuwa ukijitokeza kwenye tafiti zilizopita.”

Kuvuta sigara na unene kupita kiasi

Dkt. Levine amesema kuwa kuna uhitaji wa haraka wa kuhitaji jawabu la kwa nini kiwango cha mbegu za kiume kinashuka kwa kasi sana na kutafuta suluhu yake.
“Lazima tutafute jawabu – kwa mfano, udhibiti mzuri zaidi wa kemikali zinazotengenezwa na binadamu. Lazima tuongeze juhudi kubwa sana kuzuia uvutaji (wa sigara na vinginevyo) pamoja na unene kupita kiasi.”

Utafiti huu haukujihusisha na kuchunguza sababu za kupungua huku lakini watafiti wamesema kwamba kupungua kwa mbegu za kiume kulishawahi kuhusishwa na mambo kadhaa kama kemikali mbalimbali na dawa za kuua wadudu, dawa zinazotumika kwenye kilimo, uvutaji wa sigara na matatizo ya kuzidi kwa uzito wa mwili na unene. Hii inamaanisha kuwa kipimo cha wingi wa mbegu za kiume kinaathiriwa sana na kutokana na maisha ya kisasa.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post