VODACOM FOUNDATION YAKWAMUA KIUCHUMI WANAWAKE, YATIMA

Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Vodacom Foundation imesaidia yatima na wanawake wajasiriamali kwa kuwapa uwezo wa kujiingizia kipato na hivyo kushiriki katika kujenga uchumi wa Tanzania, imefahamika.
Kupitia huduma ya MWEI (M-Pesa Women Empowerment Initiative) na kituo cha Watoto Yatima cha Mwandaliwa, Vodacom Foundation imeweza kusaidia makundi mawili ya watu ambao katika hali ya kawaida, wangeweza kuwa masikini na wasio na msaada kwa sehemu kubwa ya maisha yao.
Katika MWEI, Vodacom imekuwa ikitoa mikopo ya kifedha kwa wanawake mbalimbali nchini pasipo kuweka riba, na hivyo kuwawezesha wengi kutumia fedha hizo kufanya biashara na shughuli nyingine za uchumi zenye kuongeza  kipato.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi binafsi ya Finscope miaka michache iliyopita, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 11 ambao hawana akaunti benki au aina yoyote ya huduma ya kifedha na kwa wanawake hali ni mbaya zaidi kuliko wanaume.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Vodacom Foundation nchini Tanzania, Rosalynn Mworia, jumla ya kiasi cha shilingi milioni 470 zimetolewa kwa wanawake 7,931 kutoka wilaya 50 nchini kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi.
“ Kama mnavyofahamu, kabla ya ujio wa huduma ya M Pesa hali ilikuwa mbaya sana hapa Tanzania kwa maana ya watu kutopata huduma za kifedha. Tulianzisha MWEI ili kujaribu kuongeza ushiriki wa akinamama, ambao wako nyuma kimaendeleo kuliko akinababa, kwenye shughuli za kimaendeleo.
“ Nina furaha kwamba sasa maelfu ya akinamama nchini kote wamejiunga katika mpango huu ambapo wanakopeshwa fedha bila riba yoyote tofauti na kama wangechukua kwenye asasi yoyote ya kifedha. Bila riba, maana yake wanaweza kupata faida haraka na hili linawasaidia kiuchumi,” alisema Mworia.
Katika kituo cha kulelea yatima cha Mwandaliwa Orphanage kilichopo Mbweni jijini Dar es Salaam, Vodacom Foundation imegharamia uanzishwaji wa miradi midogo kama ya ufundi cherehani na ufugaji wa kuku kwa ajili ya kuongeza kipato.
Mworia aliliambia gazeti hili kwamba imekuwa kawaida kwa watu wengi kutoa msaada wa kifedha pekee kwa makundi ya wahitaji lakini wao wamekuja na ubunifu tofauti katika utoaji wao wa misaada.
“ Kuna msemo mmoja maarufu wa Kichina unasema ukimpa mtu samaki kila siku, unamsaidia kwa siku hiyo lakini ukimfundisha mtu kufuga samaki, umemsaidia kwa maisha yake yote.
“ Sasa kile kituo kiko jirani na baadhi ya shule na taasisi nyingine ambazo zinahitaji sare kwa ajili ya wanafunzi na wafanyakazi wake. Watoto wa kile kituo wamefundishwa kuhusu ushonaji na ufugaji na wanatumia ujuzi wao huo kutengeneza fedha,” alisema Mworia.
Hadi sasa, Vodacom Foundation imetumia takribani shilingi milioni 20 katika kufundisha watoto ujuzi huo wa ushonaji na ufugaji na pia katika kuanzisha miradi hiyo itakayokisaidia kituo hicho kujiendesha chenyewe pasipo kutegemea misaada ya wafadhili.
Mwisho
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post