VODACOM YACHANGIA MATRILIONI KWENYE UCHUMI WA TANZANIA

Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imechangia zaidi ya shilingi trilioni nne  za Tanzania katika uchumi wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu tu, ripoti ya kampuni ya kimataifa ya KPMG imeonyesha.
Ripoti ya KPMG ilifanya utafiti katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 hadi mwaka 2015 ambapo ilisema shughuli za Vodacom pekee zilisaidia kutoa ajira rasmi 500 na zisizo rasmi zaidi ya 22,000 katika kipindi hicho kifupi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, mwakilishi wa KPMG, Lullu Krugel,  alisema kiasi hicho cha fedha, shilingi trilioni nne, ni sawa na asilimia mbili ya Pato la Taifa la Tanzania (GDP) kwa mwaka.
Ripoti hiyo ya aina yake, ilieleza kwamba kiwango hicho cha fedha kimepatikana baada ya kupiga hesabu ya kiwango cha kodi za aina mbalimbali kilicholipwa na Vodacom katika kipindi hicho, ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa zilizozalishwa na misaada mbalimbali iliyotolewa na kampuni hiyo kwa jamii ya Watanzania.
Tangu kuingia kwake hapa nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, Vodacom imekuwa mmoja wa walipa kodi wakubwa hapa nchini, ikichukua nafasi za kuwa mlipa kodi kinara miongoni mwa makampuni ya mawasiliano hapa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, alizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti ya KPMG na kusema kwamba kampuni hiyo inaelekea kwenye kutoa mchango zaidi kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Ferrao alisema kwa kadri kampuni yake inavyoona, Tanzania kwa sasa inaelekea katika matumizi makubwa zaidi ya data na kwamba hilo ni eneo ambalo Vodacom imejipanga kulitumia zaidi.
“Katika miaka ya karibuni, Watanzania wengi zaidi wameanza kutumia vifaa kama vile simu na kompyuta kwa ajili ya kutafuta taarifa taarifa na maarifa mbalimbali yanayopatikana kupitia mitandaoni. Kwa sasa Vodacom inaona kuna fursa kubwa ya ukuaji katika eneo hili,” alisema bosi huyo wa Vodacom Tanzania.
Kiasi hicho cha fedha kilichotajwa na KPMG kama mchango wa Vodacom katika uchumi wa Tanzania kimehusisha pia michango mbalimbali ambayo hutolewa na Vodacom katika sekta ya michezo na burudani.
Kwa mfano, kwa zaidi ya miaka minne sasa, Vodacom imekuwa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya mchezo wa mpira wa miguu hapa Tanzania ambayo yenyewe hutoa fedha na vifaa vya michezo kwa timu zote zinazoshiriki katika ligi hiyo.
Pia, kupitia Vodacom Foundation, kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada katika maeneo makubwa manne ambayo kusaidia sekta ya afya, kuinua wateja wake kiuchumi, misaada katika elimu na pia kusaidia wakati taifa linapopata janga lolote.
Katika eneo la afya, zaidi ya huduma hiyo ya fistula, Vodacom Foundation pia imeanzisha mradi maalumu wa kutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi (SMS) kwa wanawake wajawazito kwa ajili ya kuwapa taarifa muhimu kuhusu wao na watoto walio tumboni.
Katika kuinua akinamama kiuchumi, Vodacom Foundation imesaidia yatima na wanawake wajasiriamali kwa kuwapa uwezo wa kujiingizia kipato na hivyo kushiriki katika kujenga uchumi wa Tanzania, imefahamika.
Kupitia huduma ya MWEI (M-Pesa Women Empowerment Initiative) na kituo cha Watoto Yatima cha Mwandaliwa, Vodacom Foundation imeweza kusaidia makundi mawili ya watu ambao katika hali ya kawaida, wangeweza kuwa masikini na wasio na msaada kwa sehemu kubwa ya maisha yao.
Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya kundi la kampuni za Vodacom lenye makazi yake nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo ya Afrika Kusini nayo ni sehemu ya kundi la kampuni za Vodafone lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post