MAAJABU: KUTANA NA MLEMAVU WA MACHO ANAYEJUA MAJIRA BILA KUANGALIA SAA

Unapohitaji kuangalia saa na kutambua majira, kwa Ramadhan Isuja, saa anayo kwenye fikra zake. Akiwa mlemavu wa macho, amejaaliwa uwezo wa kutambua majira kwa usahihi sambamba na majira ya kwenye saa.
Pengine ni kwa sababu hii, uongozi wa shule anayosoma ya Old Moshi ukampa majukumu ya kuwa mtunza muda.
Isuja (23) ambaye ni mtoto wa pili katika familia ya watoto watano, anasema alizaliwa akiwa na matatizo ya macho. Wazazi wake walijitahidi kumpatia matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi lakini hakuweza kupona.
Kutokana na ulemavu wake, wazazi wake hawakukata tamaa walimpeleka Shule ya Msingi Same yenye kitengo maalumu cha watoto wenye ulemavu ambako alihitimu na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari Old Moshi.
Kipaji cha kutambua majira
Kuhusu kipaji chake cha kufahamu majira ya saa, anasema kwa mara ya kwanza akiwa mdogo alimuuliza baba yake muda, alipomjibu anasema kuanzia hapo akapata uwezo wa kufahamu majira bila kukosea saa, dakika na sekunde.
Anapotaja muda, hatumii saa ya kawaida wala saa maalumu za watu wenye ulemavu. Isuja anasema huwa anajisikia vizuri akiulizwa na mtu yeyote muda, kwa sababu anaona ana kipaji cha kipekee, huku akiomba asaidiwe ili akiendeleza.
Katika taaluma, anapendelea zaidi masomom ya Jiografia, Kingereza na Uraia na kuwa matarajio yake ya baadaye ni kuwa mwanahabari hasa upande wa utangazaji.
“Hii kazi ya utangazaji naipenda kwa sababu ni njia nzuri na rahisi inayotumiwa kufikisha ujumbe kwa watu wengi. Nikiwa na muda huwa nasikiliza redio mbalimbali na ninavutiwa zaidi na watangazaji Chunga Ruza wa TBC na Peter Mrema wa redio Moshi FM.
Swaleh Alhami ni mlemavu wa macho, ambaye kama Isuja naye anasoma kidato cha tatu. Anamweleza Isuja kama mtu anayewashangaza wengi kwa uwezo wake huo wa kujua majira kwa usahihi.
Mkuu wa idara ya elimu maalumu katika shule hiyo, Beatrice Mtae anasema licha ya kuwa hana uwezo mkubwa wa masomo ya darasani, lakini ana uwezo katika kushirikiana na wenzake kwenye mijadala ya masomo na nje ya darasa.
Aliwahi kuwatabiria wenzake
Isuja sio tu ameonyesha uwezo huo wa kipekee bali pia ameshawatabiria wanafunzi wawili matokeo yao ya kidato cha sita na kidato cha nne, na yalipotoka yalikuwa sawa na alivyotabiri.
Kilio cha Isuja
Kama ilivyo kwa watu wengi wenye ulemavu, Isuja anaiomba Serikali iboreshe miundombinu ya wanafunzi wenye ulemavu, ili iwawezeshe kupata elimu kama wanafunzi wasio na ulemavu.
“Kwa kweli sisi wenye ulemavu tuna changamoto nyingi ukilinganisha na wenzetu wasio na ulemavu kwa sababu ya hali zetu. Kwa mfano, hizi mashine za kuchapa maandishi yetu wenye ulemavu wa macho ni chache na chakavu,’’ anasema.
Anaongeza: “Naiomba Serikali itusaidie kwa kutoa vifaa zaidi kwani kuwa na ulemavu haimanishi hatuwezi kufanya lolote.” Anasema mazingira ya shule ikiwamo miundombinu sio rafiki hasa maeneo ya kupita kutoka sehemu moja kwenda nyingine kuwa na mawe na wakati wa mvua udongo unanata na kusababisha wanafunzi wenye ulemavu wa macho na miguu kupita kwa tabu.
Kuhusu changamoto za wanafunzi walemavu, Mtae anasema shule pekee haina uwezo wa kuzitatua isipokuwa kwa kushirikiana na wadau na wapenda maendeleo.
“Mwaka huu Serikali imetuletea vifaa mbalimbali kwa ajili ya elimu maalumu vitasadia sana. Natoa wito kwa jamii ambayo hawajaona umuhimu wa kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu wakidhani wanapoteza rasilimali zao.
“Sio kweli, mtoto mwenye ulemavu akiwezeshwa anaweza kufanya makubwa hata kuliko sisi ambao hatuna ulemavu,’’ anasema.
Uongozi wa shule
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Amiri Koshuma anamzungumzia Ramadhani kama kipimo cha watu wengine wenye ulemavu ambao wakiwezeshwa wanaweza kujisaidia.
“Wazazi na jamii kwa jumla wahakikishe wanawapeleka watoto shule badala ya kuwafungia ndani,” anasema Koshuma.
Anasema katika shule hiyo kwenye matokeo ya kidato cha nne, mwanafunzi mwenye ulemavu wa macho, Martin Jackson aliibuka kinara kwa kupata alama za juu zaidi kitaifa katika somo la Uraia.
Chanzo: MWANANCHI
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post