MAITI 15 ZAOPOLEWA ZIKIWA KWENYE VIROBA

Kuwapo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kuingiwa na hofu ya kuja kutakiwa kuisadia polisi katika uchunguzi wa mauaji hayo, pindi wanapogundua na kutoa taarifa za maiti hizo. Hofu hiyo imesababisha baadhi ya wavuvi kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema kuwa miili iliyookotwa ni mitatu na haikuwa kwenye viroba. “Hadi sasa taarifa za miili mingi kama hiyo kuokotwa nazisikia tu,” alisema Kamanda Mkondya. “Hao watu watueleze nasi tutachukua hatua, hatuna taarifa za miili iliyofungwa kwenye viroba au sandarusi. “Miili mitatu iliyookotwa Kunduchi iko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na haijatambuliwa, wananchi wafike kuitambua.”

Lakini wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maeneo hayo ya uvuvi jana, wavuvi walisema wamepokea taarifa kutoka wenzao wa eneo la Kizimkazi, Zanzibar, kwamba huko nako pia zimeokotwa maiti tano. Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema siku mbili zilizopita ziliokotwa maiti tano katika eneo la Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Dar es Salaam. Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba miguuni, kichwani na tumboni. “Zote zilikuwa zimeharibika na sura hazitambuliki,” alisema na kueleza kuwa zilichukuliwa na polisi baada ya kutaarifiwa. Alisema polisi waliochukua miili hiyo ni wa mkoa wa Kinondoni kutoka vituo vya Kawe ambayo ni wilaya ya kipolisi na Wazo Hill.

“Jamaa zetu wa Feri waliokota maiti sita wiki mbili zilizopita (na) kati yake mbili zimefungwa pamoja na katika hizo moja ni mwanamke. “Tulichozoea wavuvi ni kuokota maiti za wavuvi wenzetu ambaye alizama au kupotea, na zinakuwa na nguo zake za kawaida, lakini hizi ni za kuandaliwa.”

Kwa mujibu wa wavuvi hao, maiti hizo zinatoka maeneo ya ama Dar es Salaam, Pwani, Lindi au Mtwara. Walipoulizwa wamejuaje, walisema bahari ina pepo kuu mbili ambazo ni za Kaskazini na Kusini na kwamba kila mmoja unavyopiga ndivyo vitu au maiti inaweza kusafiri na kukutwa katika eneo fulani. Kwa mujibu wa chanzo hicho, upepo wa sasa hivi unavuma kutoka kusini kwenda Kaskazini, hivyo maiti hizo zisingeweza kuwa zinatokea Tanga ama Kenya, kwa mfano. “Hakuna kinachotoka Kaskazini kuja kusini, ukiona kimekuja huko kimevushwa na upepo kutoka kusini kuja huku,” alisema mmoja wa wavuvi.
HT @ Nipashe
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post