MAMBO HAYA YATAKUSAIDIA KUONDOA SUMU MBALIMBALI MWILINI

Na Fadhili Paulo
Mwili unaweza kupatwa na sumu au takataka zisizohitajika kwa namna mbalimbali, ama kupitia mazingira tunayoishi (viwanda, migodi), au kupitia vyakula na vinywaji ambavyo tunatumia kila siku.
Sumu au taka pia zinaweza kuingia mwilini kupitia dawa mbalimbali hasa tunazotumia kujitibia magonjwa mbalimbali. Mwili huzalisha sumu hizi pia kila mara kunapofanyika mmeng’enyo wa chakula mwilini mwako.
Baadhi ya ishara zitazokuonesha kuwa mwili wako una sumu nyingi ni pamoja na uchovu sugu, maumivu ya maungio, msongamano puani, kuumwa kichwa kila mara, tumbo kujaa gesi, kufunga choo au kupata choo kigumu, kukosa utulivu, matatizo mbalimbali ya ngozi ikiwamo chunusi, pumzi mbaya, mzunguko wa hedhi usio sawa, kuishiwa nguvu, kushindwa kupungua uzito na kupenda kula mara kwa mara.
Baada ya kujua ishara hizo, zifuatazo ni njia za kuondoa sumu hizo mwilini:
Fanya mlo wako mmoja wa siku kuwa matunda pekee
Amua moja ya mlo wako kwa siku uwe ni matunda bila chakula kingine zaidi. Unaweza kuamua kiwe chakula cha asubuhi ama cha jioni kuwa ni matunda pekee. Kwenye sahani yako unajaza matunda tu ya aina mbalimbali. Sahani ijae na ule hayo tu kama ndio mlo wako na kuimaliza unaweza kunywa juisi ya matunda au maji pekee.
Kula vyakula vya asili zaidi kuliko vya viwandani
Kama unataka kuepuka sumu au takataka nyingine kirahisi kuingia katika mwili wako, basi pendelea zaidi kula vyakula vya asili vinavyopikwa nyumbani kuliko kula vyakula vinavyosindikwa kwenye makopo, vya dukani au vya kwenye migahawa (fast foods).
Fanya masaji
Kwa bahati mbaya Watanzania wengi hawajui kwamba masaji ni sehemu tiba au ni dawa pia kwa magonjwa mengine mengi mwilini. Wengi tunaichukulia masaji kama kitu cha starehe tu, lakini unaweza kutumia masaji kama njia mojawapo ya kuondoa sumu mwilini na utafanikiwa kwa muda mfupi sana.
Kunywa maji mengi kila siku
Sababu kubwa ya watu wengi kutengeneza sumu au taka nyingi mwilini mwao ni kutokunywa maji mengi kila siku. Maji ni uhai, bila kunywa maji mengi kila siku ni sawa na kwenda dukani bila hela mfukoni. Haijalishi upo mazingira gani kama ni ya baridi au joto, ni lazima unywe maji ya kutosha kila siku iendayo kwa Mungu.
Mwili unahitaji glasi 8 hadi 10 kila siku. Watu wengi wanahangaika namna ya kuondoa sumu na kusafisha miili yao bila kujua maji ya kunywa pekee yanatosha kwa kazi hiyo.
Kumbuka asilimia 94 ya damu yako ni maji, asilimia 85 ya ubongo wako ni maji, hivyo, ili kusafisha damu na mwili kwa ujumla ni lazima unywe maji ya kutosha kila siku.
Acha chai ya rangi na kahawa
Kama tayari imethibitika una sumu au taka nyingi mwilini, unashauriwa uache kunywa chai ya rangi na kahawa. Badala yake hamia kwenye kutumia chai yenye tangawizi, mdalasini au mchaichai.
Chai ya rangi na kahawa vina kafeini ambayo kwanza huyasukuma maji nje ya mwili kwa haraka na kuuacha mwili bila kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kazi zake. Kafeini pia ni mojawapo ya aina ya dawa za kulevya katika kundi ya dawa zinazosisimua mwili (stimulants).
Fanya mazoezi ya viungo
Inashangaza sana kuona Watanzania wengi hawaoni umuhimu wa kufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi ya viungo ni jambo la lazima kama ilivyo chakula. Iwe unaumwa au huumwi, iwe una uzito kuzidi au wa kawaida, hakikisha unapata muda wa mazoezi.
Mazoezi yanakusaidia kukufanya ujisikie vizuri na hivyo kukuondolea mfadhaiko (stress) kirahisi zaidi. Sambamba na hilo, mazoezi ni dawa tosha na nzuri ya kuondoa sumu mwilini haraka zaidi. Hakikisha jasho la kutosha linakutoka na iwe ni jambo la kila mara.
Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi (faiba)
Umesikia mara nyingi kwamba unahitaji kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa ajili ya kuwa na afya bora, mmeng’enyo wa chakula wenye afya na hata kukusaidia kupunguza uzito.
Kama mpaka sasa ulikuwa hujui pengine ni kuwa vyakula hivi vyenye nyuzinyuzi ni vizuri pia katika kusafisha mwili na kuondoa sumu au takataka mbalimbali.
Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi ni pamoja na parachichi, ndizi, peasi, karoti pilipili hoho, mchele wa brown (wanaoshauriwa kutumia watu wenye kisukari), maharage meusi, njegere, tende, viazi vitamu, tufa (apple), machungwa, ugali wa dona na mkate wa unga wa ngano ambao haujakobolewa.
Kufunga
Kama ulikuwa hujui namna nyingine rahisi ya kuondoa au kupunguza sumu mwilini ni kufunga kula kabisa kutwa nzima.
Ukifunga kula, mwili unalazimika kuvitumia vile vilivyomo ndani yake bila kushughulika kuvisaga vingine vipya vinavyokuja. Kunapokuwa hakuna shughuli ya kusaga na kumeng’enya chakula kipya ndipo mwili unapoweza kuondoa sumu na taka nyingine kirahisi zaidi.
Amua kufunga kwa kutokula kabisa mara mbili kwa wiki ili kupunguza au kuondoa sumu mwilini.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post