MAMBO SITA YA KUFANYIA MAZOEZI KABLA YA KWENDA KWENYE USAILI WA KAZI

Kama unaweza vizuri kujibu mambo kama “Tueleze historia yako,” “Kwanini unataka kufanya kazi hapa?” au “Mapungufu yako makubwa ni yapi?” basi ujue ushavuka hatua za mwazo za usaili wa kazi, lakini inawezekana kuna kundi la maswali ambalo bado hujaweza kuyajibu vizuri: kundi la maswali yanayolenga kujua tabia yako.
Maswali ya usaili ya kujua tabia yako yanahitaji uchague tukio fulani maalum kutoka katika historia yako kazini ili ujibu zaidi swali uliloulizwa na yawezekana haya ndio yakawa maswali magumu zaidi kuyajibu— kwa kawaida maswali ya usaili ni magumu, lakini kuambiwa utoe mfano kutoka kwenye maisha yako kunafanya usaili wote uwe mgumu zaidi.
Yafuatayo ni baadhi tu ya maswali ya aina hii na muongozo wa jinsi ya kuyajibu:
1. Tueleze mafanikio makubwa zaidi uliyowahi kuyapata na unayojivunia zaidi
Kwa swali la aina hii, jizuie kueleza jinsi ulivyofaulu vizuri katika matokeo yako ya Chuo Kikuu au ushindi uliopata kwenye michezo ya kazini kwako.
Kulijibu vizuri zaidi swali hili, unatakiwa uzungumzie jambo ambalo linakaribiana zaidi na kazi unayoifanyia usaili kadri ya inavyowezekana na ambayo inaweza ikaonesha vizuri mambo unayoweza kuyafanya kwa ufanisi na uwezo wako kazini.
Elezea tukio lolote ambapo kulitokea tatizo, elezea ukubwa na madhara ya tatizo hilo na ni jinsi gani uliweza kulitatua. Pia elezea faida za ziada zilizopatikana zaidi ya zile zilizopatikana mara baada ya kutatua tatizo hilo. Kwa mfano, kama ulitengeneza mfumo mpya utakaowasaidia waajiriwa wapya, elezea ni kwanini uliona kampuni yako ilitakiwa kuwa na mfumo kama huo, matatizo yapi yalikuwa yanasababishwa na kutokuwa na mfumo kama huo, ulifanya nini kutengeneza wa kwako na ni jinsi gani baada ya mwaka mmoja kwa mfano, matatizo yamepungua au kutoweka kabisa.
2. Tueleze kasoro kubwa uliyonayo
Moja ya makosa makubwa sana yanayofanywa na mtu anayefanyiwa usaili ni kujibu swali hili kwa kusema kwamba ‘kasoro’ pekee aliyonayo ni kwamba “Nafanya kazi kwa bidii sana” au “Napenda sana kusaidia wafanyakazi wenzangu” mpaka inakuwa kero kwa wengine.
Kuwa makini: wanaokufanyia usaili wana unachojaribu kufanya na washakaa na watu wengi sana waliotoa jibu la aina yako.
Pamoja na hayo, epuka sana kuzungumzia kosa kubwa sana ulilowahi kufanya. Kosa linalofanywa na wengi ni kwamba labda mtu atajaribu kukwepa kulijibu swali hili au kutoa mfano ambao unamfanya aonekane mwema sana; kumbuka kwamba umekwenda kufanya usaili huo ili waone kwamba utakuwa na manufaa kwao kama wakikuajiri.
Badala ya kufanya hivyo, jaribu kufikiria jambo lililowahi kutokea miaka mingi iliyopita. Muhimu zaidi ni kutozungumzia kosa au kasoro zenyewe moja kwa moja, bali kuonesha mafunzo uliyopata na yamekusaidiaje kuhakikisha kwamba hurudi makosa yako.
3. Tueleze unatatuaje matatizo
Wakati unajibu swali hili, hakikisha hutupii mtu lawama kwa majanga yoyote yaliyokukuta kazini. Hata kama walihusika kwenye matatizo hayo, bila shaka usingependa uonekane kama hupendi kushirikiana na wengine au kwamba hupendi kukubali makosa unayofanya.
Akili yako yote ielekeze kwenye jambo ulilofanya wewe na uelezee mazingira ya kosa hilo bila kutegemea upande wowote. Usishawishike kuanza kusema kwamba una bosi mkorofi au wafanyakazi wasio na ushirikiano: ingawa sote tuliowahi kuajiriwa tumekumbana na hayo yote mawili, mtu anayekufanyia usaili hana njia ya kuhakikisha kwamba unachosema kina ukweli wowote au kwamba unawatupia wengine lawama ulizostahili kuzibeba wewe mwenyewe.
Kwa mfano, unaweza kuamua kuzungumzia mradi uliowahi kuufanya peke yako au kwa kushirikiana na wengine mkiwa na kiasi kidogo cha bajeti ukilinganisha na wapinzani wenu kwenye soko na jinsi gani mliweza kufanya hilo lisiwe tatizo kabisa. Katika kuelezea namna ulivyoweza kusaidia kwenye hili, hakikisha unaelezea kwa undani ni kwa nini ilikuwa ngumu sana kwakuwa tatizo ulilotatua linavyozidi ukubwa ndipo faida yake inapokuwa kubwa zaidi.
4. Wakati gani umewahi kufanya kazi kubwa zaidi ya majukumu uliyopangiwa kuyafanya
Tulia kwanza kabla ya kujikuta unaanza kuropoka mambo unayoona yalikuwa na mafanikio kwako. Kwa sababu kabla hujaanza kuelezea jinsi gani umefanya kazi kubwa zaidi ya ulivyopangiwa kwanza inabidi ujue kinachomaanishwa ni nini.
Wengi wanaofanyiwa usaili wanapata tabu kujibu swali hili kwakuwa wanashindwa kueleza historia ya kazi hiyo. Kabla hujaanza kuzungumzia jinsi gani ulifanya kazi kubwa zaidi ya uliyopangiwa, kwanza elezea mipaka ya kazi yenyewe. Jaribu kuelezea mazingira ya kazi yalivyokuwa, malengo na ulichotakiwa hasa kukifanya.
Ni bora uzungumzie mradi ambao ulileta mafanikio kwa kampuni ambao labda ulikuwa ukifanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya mara moja kuhakikisha mambo yakamilike kabla ya muda mliopangiwa na kwa kiwango cha juu, au kwamba kama ulijitolea kumalizia kazi ambayo haikumalizwa na mwenzako. Mfano wowote utakaotaka kuutumia, hakikisha maelezo yako yaoneshe utayari wako wa kufanya kazi na kusaidia wenzio kazini.
5. Tueleze ilikuwaje ulipotofautiana na bosi wako
Kwa mara nyingine, kujibu swali kama hili, kutupa lawama au kuwasema watu wengine si jambo zuri kulifanya. Itafanya udharauliwe mapema sana kwakuwa yawezekana ukawa unamsema vibaya bosi wako kwa mtu ambaye anajuana naye.
Hili ni la kuchunga hasa unapofanyiwa usaili wa kazi inayofanana na ile unayofanya sasa: dunia ni ndogo sana. Mtu unayemsimulia yawezekana anasali kanisa moja, au anajuana na mtu anayehusiana na bosi wako. Badala yake, weka msisitizo kwenye kueleza ni jinsi gani kutofautiana na bosi wako kulifanya uongeze juhudi kazini badala ya kuacha hasira zikutawale.
Kimsingi, unatakiwa uweke wazi kwamba wewe na bosi wako mnaheshimiana na mna uhusiano wa karibu. Unatakiwa kuonesha kwamba unamhurumia bosi wako … na unaamini katika kuitekeleza na kuitimiza dira ya kampuni.
6. Una uzoefu gani kwenye uongozi?
Usishawishike kutaja kila nafasi ya uongozi uliyowahi kushika — badala yake, fikiria chache zilizokuwa na matokeo makubwa zaidi. Wengi watajikuta wakiorodhesha kila nafasi ya uongozi aliyowahi kushika, lakini inabidi ujue mapema kwamba uongozi unapimwa kwa mafanikio yaliyopatikana. Kwenye uongozi wako, watu wanatakiwa kuwa wamepata uzoefu zaidi au mafanikio zaidi kazini tofauti na walivyokuwa kabla hujaanza kuwaongoza.
Kwa kuongezea, itakusaidia sana kama utaweza kuonesha uzoefu wako kama kiongozi unaonesha ni jinsi gani unapokea mawazo mapya na kuyafanyia kazi. Usitaje kipindi ambacho uliambiwa ukaimu nafasi ya uongozi kutokana na mwenye ofisi kuwa safarini au nje ya ofisi kwa sababu yoyote.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post