NI MTU GANI ANASTAHILI KUPEWA SHAHADA YA UDAKTARI WA HESHIMA?

Kila mwaka, maelfu ya watu duniani huvaa majoho na kwenda kutunukiwa shahada zao za uzamivu (Ph.D.) Kwa wengi, sherehe hizi zinafata baada ya mtu kuwekeza miaka kadhaa ya kusoma kwa bidii, kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa masomo na kudaiwa ada.
Wengine wanaibuka tu siku hiyo ya kuhitimu na majoho yao bila kupitia tabu yoyote ya kimasomo ambayo wenzao wameipitia mpaka kustahili kuvalishwa majoho hayo na kuhitimu shahada zao. Wakiungana na wanafunzi hao, wanamichezo waliowahi kuwa na sifa ulimwenguni pamoja na wafanyabiashara mashuhuri au Marais wa nchi kama — Jakaya Kikwete, Mike Tyson, Oprah na Bill Gates — wameonekana kwenye vyuo mbalimbali wakipokea shahada  ya “heshima” ya uzamivu. Tofauti na wanafunzi waliosoma kupata elimu zao, watu hawa ambao ni kioo kwa jamii hutunukiwa shahada hizi bure kabisa: vyuo vikuu huwaruhusu kuuepuka utaratibu wote wa masomo unaotakiwa kumuwezesha mtu kupata shahada hii. Ingawa shahada hizi ni za heshima tu, na si kimatumizi, swala la watu kupewa shahada hizi halikuanza hivi karibuni.
Chuo Kikuu kutoa shahada ya heshima kwa mtu ni ishara ya chuo hicho kuonesha ishara ya kutambua mafanikio ya juu kabisa yaliyopatikana kwenye sekta, tasnia au nchi kutokana na mchango wa mtu husika. Chuo husika pamoja na jamii nzima vinatakiwa kuitambua shahada hiyo kama uthibitisho wa mafanikio ya mtu.
Shahada ya heshima inatunukiwa kutokana na mafanikio makubwa kabisa yaliyopatikana kutokana na mchango wa mtu fulani, hasa inapothibitika kuwa mchango wa mtu huyo katika taaluma, sekta au nchi husika ni mkubwa zaidi ya mchango ambao watu wenye taaluma hiyo wanaweza kuutoa. Hata hivyo, shahada hizi hazitunukiwi kwa watu kwa sababu za kisiasa au kiwango cha utajiri cha mtu.
Miongoni mwa sababu zinazoweza kufanya mtu atunukiwe shahada ya heshima na Chuo Kikuu:
  • Kwakuwa vyuo vikuu vina uhusiano wa karibu na jamii, ni jambo la busara kwao kutoa shahada za heshima kwa watu walioonesha kutambua mchango wa chuo husika kwa jamii. Mtu anayetunukiwa shahada ya heshima lazima awe anaunga mkono malengo na mchango wa chuo hicho kwenye jamii.
  • Shahada hii inaweza kutunukiwa kwa mtu aliyetoa mchango mkubwa kwa chuo au jamii, ingawa yawezekana mtu huyo asiwe mashuhuri.
  • Shahada hii pia hutolewa kwa mtu bila kujali kiwango cha umuhimu wa mtu kwenye jamii mradi mchango wake uwe ni wa umuhimu mkubwa unaostahili kutambuliwa kwa heshima ya juu na pia iwapo mchango wake utaendelea kulinufaisha Taifa kwa muda mrefu zaidi.
  • Chuo Kikuu mara nyingi hutoa shahada ya heshima kwa mtu ambaye alishawahi kusoma chuo hicho ingawa si lazima sana, lakini shahada hii haitunukiwi kwa mtu aliyeajiriwa na chuo hicho.
  • Uteuzi wa mtu anayetakiwa kutunukiwa shahada ya heshima unatakiwa uoneshe uhusiano uliokuwapo kati ya mtu husika na chuo kinachotakiwa kumpa shahada hiyo, kwakuwa chuo ndio kinachoonesha kutambua mafanikio yaliyotokana na juhudi za mtu huyo.
Pamoja na sababu hizo, ni vyema ikajulikana wazi kuwa udaktari wa heshima huwa hauombwi, ni chuo husika kupitia seneti yake huangalia kazi zilizofanywa na mtu kama zina umuhimu mkubwa katika Taifa kiasi cha kumfanya atunukiwe shahada hii ya heshima, lakini si kwa kuomba.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post