RAIA WA AFRIKA KUSINI APANDISHWA KIZIMBANI DAR KWA KUTOA VITISHO

Raia mmoja wa Afrika Kusini, Menolaos Tsampos (61), leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akishtakiwa kwa makosa ya kutishia kwa mtandao, kuishi nchini kwa muda wa miaka minne bila kibali na kutumia paspoti yenye visa ya kugushi.
Mshtakiwa huyo aliyefikishwa katika mahakama hiyo leo kabla ya kusomewa mashtaka alitishia kuwapiga waandishi wa habari waliokuwa wakimpiga picha. Tsampos aliyekuwa chini ya ulinzi wa Polisi alikuwa akijaribu kurusha mateke na ngumi akijaribu kuwazuia waandishi wa habari wasimpige picha.
Mtuhumiwa huyo amesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ambapo amekana mashtaka yote na amerudishwa rumande hadi hapo upande wa mashtaka utakapothibitisha uhalali wa Visa yake na makazi yake ya kudumu.
Wakili wa serikali, Nassoro Katuga akisoma hati ya mashtaka hayo amedai kuwa, Juni 22, mwaka huu ndani Dar es Salaam, mshtakiwa kwa kutumia mfumo wa kompyuta, alimuandia barua pepe Costa Gianna Koulos, yenye maneno ya vitisho kwa nia ya kumsababishia Koulos hisia za uoga.
Aidha, mahakama hiyo imeambiwa kwamba, Julai 20 mtuhumiwa huyo alimuandikia barua pepe nyingine Koulos yenye maneno ya vitisho na kumpa masaa 48 kumtaka wakae na kumaliza tofauti walizonazo vinginevyo atamfanyia kitu kibaya.
Katika shtaka jingine, Agosti 7 mwaka huu akiwa katika Kituo cha Polisi cha Kati, Tsampos alikutwa akiwa na pasi ya kusafiria yenye namba M00101612 ikiwa na visa ya kughushi.
Wakili Katuga ameendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba 246184272,  raia wa Afrika Kusini, Julai 6, mwaka huu alikamatwa akiishi nchini bila ya kuwa na kibali maalumu.
Mshtakiwa amekanusha kutenda makosa hayo na amerudishwa rumande baada ya mahakama kuutaka upande wa utetezi kufanya uchunguzi na kuhakikisha kama kweli mshtakiwa anaishi mbezi kama ana visa yake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 16, mwaka huu.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post