RAIS MAGUFULI AFUTA CHAGUZI KATIKA KATA 41 NA KUELEZA SABABU

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefuta uchaguzi wa ndani ya chama hicho katika kata 41 kati ya kata 4,420 zinazoshiriki katika uchaguzi huo, kutokana na kubaini kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi na kuagiza mchakato kurejewa upya.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alipozungumza na waandishi wa habari ambapo alisema hizo ni salama kwa viongozi wengine wanaotaka kugombea ndani ya chama hicho kwamba hawatapita kwa njia za ujanja ujanja.
“Hii ni awamu ya kwanza tunapeleka ujumbe kwa sababu wanaCCM wanataka CCM mpya inayosimamia haki, haya ni maelekezo na yanapaswa kuzingatiwa ili kurejesha hali ya uchaguzi katika eneo husika katika namna inayoheshimu Katiba na Kanuni ya Uchaguzi na Uongozi na Maadili,” alisema Polepole.
Aidha, Polepole alisema kwamba baadhi ya viongozi wameanza kupanga safu za watu wao katika uchaguzi huo kitu ambacho hawakubaliani nacho, lakini pia kuwekwa kwa viongozi ambao ni mapandikizi kutoka nje ya CCM.
Akitaja sababu nyingine iliyopelekea kufutwa kwa chaguzi hizo, Polepole alisema baadhi ya viongozi walishindwa kusimamia kikamilifu mali za chama katika maeneo yao. Wengine wamefutiwa uchaguzi kutokana na viongozi walioomba dhamana kutokuwa wakazi wa maeneo waliyogombea huku wengine wakiwa hawajatendewa haki katika mchakato mzima.
Sababu nyingine ni baadhi ya chaguzi kuwa na kiongozi mmoja tu katika nafasi za uongozi zinazoombwa na baadhi ya vikao vyenye dhamana ya kutoa mapendekezo kutoa taarifa za uongo kuhusu waomba dhamana na kupotosha vikao vya juu.
Polepole alisema baada ya chaguzi hizo walipokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali na wakayafanyia kazi hivyo wameamua kufuta chaguzi hizo ili kuhakikisha viongozi halali wanapatikana.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana baada ya kupokea maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM, John Pombe Magufuli na kushauriana nae kuhusu malalamiko ya wanachama wao, wamefikia uamuzi wa kufuta chaguzi hizo.
Miongoni mwa kata ambacho chaguzi zake zimefutwa na nafasi wanazotakiwa kurudia ni Kata ya Buguruni (Mwenyekiti na Katibu), Kata ya Liwiti (Katibu), Kata ya Kariakoo (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Manzese (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), kata za Makuburi, Mabibo na Kigamboni.
Nyingine ni Kiburugwa, Mchafukoge, Gerezani, Segerea (Mwenyekiti na Katibu), Pugu Stesheni (Mwenyekiti, Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Mianzini, Kata ya Pugu (Katibu Mwenezi), Kata ya Ndugumbi, Kata ya Kilungule, Kata ya Makumbusho, Kata ya Kitunda (Katibu na Katibu Mwenezi), Kata ya Ukonga na Kata ya Msasani.
Kata nyingine ni kutoka mikoa mingine ni kata zote 18 za Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara, Kata ya Seria kwa vijana Wilaya ya Kondoa Mjini Mkoa wa Dodoma nafasi ya Katibu pamoja na Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Hadi sasa chaguzi za CCM ndani ya Shina, Tawi na Kata tayari zimefanyika ambapo kati ya mashina mapaya 222,126 tayari 220,801 sawa na asilimia 99.3 yameshafanya chaguzi.
Kati ya Matawi mapya 23,246 tayari 22,447 sawa na asilimia 97 yameshafanya chaguzi.
Kwa upande wa Kata, tayari kata 3,726 sawa na asilimia 84.3 zimeshafanya chaguzi hizo huku Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji chaguzi zikiwa zimeshimamishwa kwa muda.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post