RAIS MAGUFULI AWAPA MAJUKUMU MABALOZI WAPYA WALIOJITAMBULISHA KWAKE LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Agosti, 2017 amepokea hati za utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni;
  1. Nguyen Kim Doahn – Balozi wa Vietnam hapa nchini.
  2. Prof. Ratlan Pardede – Balozi wa Indonesia hapa nchini.
  3. Mwadhama Askofu Mkuu Marek Solcynski–Balozi wa Vatican hapa nchini.
  4. Dkt. Detlef Wachter – Balozi wa Ujerumani hapa nchini.
  5. Richard Tumisiime Kabonero – Balozi wa Uganda hapa nchini.
Akizungumza na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo ambazo ni marafiki wa muda mrefu na washirika wa maendeleo wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kutilia mkazo diplomasia ya uchumi kwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na huduma za kijamii.
Kwa upande wao Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapokea na wameahidi kuhakikisha uhusiano wa nchi zao na Tanzania unaendelezwa na kuimarishwa zaidi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Benedict Martin Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Mhe. Benedict Martin Mashiba anachukua nafasi ya Mhe. Victoria Richard Mwakasege ambaye amestaafu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2017
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post