RC GAMBO AKIUKA MAAGIZO YA MAKAMU WA RAIS IGAWAJI WA RAMBIRAMBI

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amekiuka maagizo ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan baada ya kugawa fedha za rambirambi Tsh 23.2 milioni kwa familia za watoto watatu walionusirika katika ajali ya basi la wananfunzi wa Lucky Vicent iliyotokea mwezi Mei 6 mwaka huu wilayani Karatu.
Akizungumza ofisini kwake wakati wa kukabidhi fedha hizo, Gambo alisema kwamba serikali na wadau mbalimbali walichangia fedha kwa ajili ya rambirambi kutokana na ajali hiyo iliyopelekea vifo vya wanafunzi 32 ambapo alisema fedha hizo zilitumika katika shughuli nzima za mazishi na zilizobaki ndio anazikabidhi kwa manusura hao.
Wakati hayo yakitokea jana, maagizo wa Makamu wa Rais yakisomwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye alimuwakilisha wakati wa kuwapokea watoto hao walipokuwa wakirejea kutoka Marekani, alimuagiza RC Gambo kutoa Tsh 20 milioni katika fedha hizo kuchangia mfuko wa elimu wa Stemm ambao unakusudia kuwasomesha wanafunzi hao walionusurika katika ajali hadi chuo kikuu.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa kugawa fedha kwa familia za watoto hao watatu licha ya kuagizwa na Makamu wa Rais achangie mfuko wa elimu, Gambo alisema kwamba serikali huwa inafanya kazi kwa maandishi na ofisi yake haikuwa imepokea taarifa yoyote kuhusu fedha hizo.
Aidha, alisema kwamba yeye ndiye aliyemuomba Mghwira akawapokee watoto hao kwa niaba yake kwa sababu alikuwa nje ya mkoa kwa shughuli nyingine.
Kuhusu hotuba aliyoisoma Mghwira akieleza kwamba ni kwa niaba ya Makamu wa Rais, Gambo alisema yeye hajui kama ilikuwa na kiongozi huyo na kwamba mwenye majibu sahihi kuhusu hotuba hiyo ni  Mghwira.
Katika mgawanyo huo, kila familia ya mtoto mmoja ilipata kiasi cha Tsh 7,750,000 na kuambiwa kwamba wataamua wao namna ya kuzitumia na kwamba serikali haihusiki na kuwapangia namna ya kuzitumia.
Familia za watoto walizokabidhiwa fedha hizo ni Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Shadia Awadh ambao walirejea nchini Agosti 18 baada ya kukaa Marekani kwa miezi mitatu wakipatiwa matibabu.
Wazazi wa watoto hao waliuomba uongozi wa Mkoa wa Arusha kuingilia kati baada ya kuwapo dalili kwamba watoto wao huenda wakazuiwa na uongozi wa Shule ya Lucky Vicent kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utakaofanywa mapema mwezi wa tisa mwaka huu.
Akijibu maombi hayo, RC Gambo alimuagiza Ofisa Elimu wa Mkoa wa Arusha kufuatilia suala hilo kwani kama wazazi wamekubali, haoni sababu ya watoto hao kuzuiwa kufanya mtihani huo.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post