TAASISI 1,500 ZAJIUNGA M PESA

Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya taasisi 1,500 hapa nchini sasa zinatumia huduma ya M Pesa inayotolewa na kampuni ya Vodacom kwa ajili ya kukusanya mapato, kulipia bili na huduma nyingine za kifedha, imefahamika.
Akizungumza na waandishi wa  habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema taasisi hizo zimejiunga na M Pesa kwa sababu ya ubora wa huduma zake.
“Nina furaha kuutangazia umma wa Watanzania kwamba hivi sasa zaidi ya taasisi 1,500 hapa Tanzania zinatumia huduma ya M Pesa kwa ajili ya kufanyia huduma mbalimbali za kifedha zikiwamo kulipia bili na kukusanya mapato,” alisema.
Kupitia huduma ya M Pesa, wateja wa Vodacom wanaweza kupokea na kutuma fedha kupitia simu zao za mkononi na pia wanaweza kutoa fedha na kuweka katika akaunti zao za benki za kawaida, wakiwa mahali popote ambapo huduma za Vodacom zinapatikana.
Kuwapo kwa huduma za M Pesa kumekuwa kwa msaada mkubwa kwa taasisi hizi ambazo zinahusisha kampuni na asasi zisizo za kibiashara, kwa sababu imepunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na mambo mengine, uwepo wa huduma ya M Pesa umewapa ahueni wateja au wadau wa taasisi hizo ambao sasa hawahitaji tena kupanga foleni kwa muda mrefu na kupoteza muda kwa sababu ya kulipia bili zao.
Mmoja wa wateja wa kampuni ya Vodacom na anayetumia huduma za M Pesa, Michael Bushoke, aliliambia gazeti hili jana kwamba siku hizi hahitaji kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu kwani anaweza kufanya chochote na akiwa popote.
“ Siku hizi M Pesa  imetusaidia sana. Hebu fikiria mtu umekaa nyumbani katika kochi lako ukiangalia mechi ya timu unayoipenda lakini wakati huohuo unaweza kuwa unalipia ada ya shule ya mwanao au huduma ya maji au umeme. Kusema kweli M Pesa imekuwa mkombozi mkubwa kwetu,” alisema.
Bushoke alimwambia mwandishi wa gazeti hili kwamba huduma za M Pesa zimekuwa muhimu hata katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili kwani sasa ni kawaida kusikia mtu akimwambia mwenzake naomba ‘uni- M Pesa’ akimaanisha anahitaji kutumia fedha kupitia namba yake ya simu ya Vodacom inayotumia huduma hiyo.
Kampuni ya Vodacom iliingia rasmi nchini Tanzania mnamo mwaka 2000 na ilikuwa ya kwanza kuanzisha huduma za kifedha kwa kupitia simu za mkononi wakati ilipoibua M Pesa mwaka 2008.
Wakati ilipoingia nchini wakati huo, hakuna aliyetegemea mapinduzi ambayo kampuni hiyo ingeyaleta hapa nchini lakini sasa huduma za kifedha kupitia kampuni za simu ni kubwa kiasi kwamba kiasi cha fedha kinachozunguka kwa mwaka kupitia huduma kama M Pesa hapa Tanzania kwa sasa ni sawa na asilimia 47 ya Pato la Taifa (GDP).
Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya kundi la kampuni za Vodacom lenye makazi yake nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo ya Afrika Kusini nayo ni sehemu ya kundi la kampuni za Vodafone lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, Vodacom kupitia M Pesa inashikilia asilimia 54 ya soko la huduma za kibenki kwa kupitia mawasiliano ya simu na kampuni nyingine ndiyo zinagawana asilimia iliyobaki.
Kutokana na mafanikio ambayo Vodacom imekuwa ikiyapata tangu ilipoingia nchini, mwaka 2013 ilitunukiwa tuzo ya kimataifa iliyoitambua rasmi kama Super Brand.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post